Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

img-20161217-wa0002
Nguzo zetu kuu zikiwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu wao wamefanya nini?
Kila tunapopanga kufanya mambo makubwa, wapo watu wanaojitolea kutushauri namna mambo hayo ni makubwa, au hatuwezi au tutashindwa.
Unakuta hata hujamwomba ushauri lakini yeye anajitolea kukupa ushauri huo ambao kwa sehemu kubwa unakatisha tamaa.
Kwa bahati mbaya zaidi, anayetoa ushauri huo anakuwa ni mtu wa karibu sana. Na ukijidanganya kumsikiliza, unajikuta unakubaliana naye.

Sasa kabla hujapokea ushauri wa mtu yeyote, kabla hujatoa nafasi ya kutafakari kile mtu anakuambia, kwanza jiulize swali hili; YEYE AMEFANYA NINI?
Jiulize yeye anakupa ushauri wa kuacha kufanya kitu fulani, ambacho ni kikubwa, lakini yeye ni kipi kikubwa ameshafanya kwenye maisha yake?
Kama hakuna kikubwa ameshafanya, basi hupaswi kumsikiliza na maneno yake ya kukatisha tamaa, hata kama ni mtu wako wa karibi sana.
Huachi kumsikiliza kwa sababu unamdharau, bali unaacha kumsikiliza kwa sababu taarifa zake juu ya jambo hilo siyo sahihi.

Na kwa wale ambao wameshafanya makubwa, wanapokupa ushauri wa kukatisha tamaa, siyo uupokee na kuacha kufanya, badala yake utumie kuhakikisha unaepuka yale maeneo hatari.
Kwa vyovyote vile, mtu awaye yote asikuzuie wewe kutekeleza ndoto za maisha yako.
Ni wewe pekee utayaishi maisha yako, usikubali mwingine akupangie anavyotaka yeye.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz