Watu wamekuwa wakisema kwamba dunia haina usawa, kwamba kuna watu wanaoanzia kwenye hali nzuri kuliko wengine, hilo ni sawa. Lakini kuna eneo moja ambalo kuna usawa kabisa duniani. Eneo hili ni la muda, kila mtu hapa duniani ana masaa 24 kwa siku, na hakuna mwenye nguvu ya kumdhulumu mwenzake masaa hayo 24 ya siku.

Pamoja na masaa haya kuwa sawa kwa kila mtu, jinsi tunavyoyatumia tunatofautiana. Kila mtu anachagua namna anavyoyatumia masaa yake ya siku.

Sasa ukiwaangalia watu waliofanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa, tofauti ya kwanza kabisa unaiona kwenye matumizi yao ya muda. Wale ambao wamefanikiwa wanatumia muda wao vizuri, wale ambao hawajafanikiwa hawajui hata muda wao wanautumiaje, japo kila siku wanalalamika hawana muda.

Mwandishi Kevin Kruse amefuatilia maisha ya mabilionea 7, washindi wa olimpiki 13, wanafunzi wenye ufaulu wa juu 29 na wajasiriamali wenye mafanikio 239 na kupitia maisha yao amegundua siri 15 wanazotumia kwenye muda wao. Anatushirikisha siri hizo 15 kwenye kitabu chake ambacho ninakwenda kukuchambulia kwenye makala ya leo. Karibu uzijue siri hizi, uweze kuzitumia ili kunufaika na masaa yako 24 ya siku.

SIRI YA 1; Muda ni kitu chenye thamani kubwa na adimu.

1. Watu waliofanikiwa hawafikirii muda kama masaa, badala yake wanafikiria muda kama thamani. Wanajua muda una thamani kubwa kuliko kitu kingine chochote hapa duniani. Wanajua wakipoteza fedha wanaweza kuzipata tena, ila wakipoteza muda ndiyo umepotea.
Upe muda wako thamani kubwa na ujali, ndipo mafanikio yako yalipo.

2. Kwa kuwa muda ni adimu na kwa kuwa ukishapotea hauwezi kurudi tena, kuwa bahili wa muda wako. Usikubali kabisa watu wachezee muda wako kama wanavyojisikia wao wenyewe, utunze muda wako na uweke kwenye yale ambayo ni muhimu kwako.

SOMA; KITABU CHA NOVEMBER; Time Warrior(Shujaa Wa Muda)

SIRI YA 2; Jua jukumu muhimu kwako na lifanye kwanza kabla ya mengine.

3. Kila siku vipo vitu vingi vya kufanya na muda wako. Usipokuwa na kipaumbele kwenye mambo unayofanya, unashangaa siku inaisha na huoni kipi kikubwa umefanya. Watu waliofanikiwa wanajua majukumu muhimu zaidi kwao na wanayafanya hayo kwanza kabla hawajafanya kitu kingine kwenye siku yao. Ianze siku yako kwa kufanya yale muhimu.

4. Ipangilie siku yako kabla hujaianza, panga kila kitu utakifanya saa ngapi na kwa muda gani. Unapoianza siku bila ya kuipanga, unajikuta mambo mengi yanajitokeza na yanachukua muda wako.

SIRI YA 3; Tumia kalenda kupanga siku yako, usitumie orodha ya mambo ya kufanya.

5. Watu waliofanikiwa wanatumia kalenda katika kupangilia muda na siku zao. Kama kuna jambo ambalo wanataka kufanya, wanalipangia siku ya kulifanya na muda wa kulifanya. Muda unapofika wanafanya jambo hilo. Watu wengine wanahangaika na kutengeneza orodha ya mambo wanayotaka kufanya kwa siku. Tatizo la orodha ni kwamba vitu vinakuwa vimepangwa bila ya muda na havina kipaumbele. Anza kutumia kalenda badala ya orodha.

6. Unapotumia kalenda, pangilia wiki yako nzima kwa yale ambayo ni muhimu. Unapoianza siku unajua kabisa lipi muhimu la kufanya.

SIRI YA 4; unaweza kuishinda tabia ya kuahirisha mambo kwa kuishinda nafsi yako ya baadaye.

7. Kinachowafanya watu waahirishe mambo, kufikiria nafsi zao za baadaye zaidi ya nafsi za sasa. Watu wanaona baadaye mambo yatakuwa mazuri zaidi au baadaye mambo yatakuwa mabaya zaidi kwa kufanya au kutokufanya kitu husika. Ili kuishinda tabia ya kuahirisha mambo, usisikilize chochote unachojiambia kuhusu kesho, badala yake panga kitu sasa na kifanye sasa.

8. Chochote unachofanya au kutokufanya sasa, angalia madhara yake kwa baadaye. Kwa mfano kama unaahirisha kukamilisha kazi yako, angalia jinsi itakavyokunyima fursa nzuri za baadaye. Kama unaahirisha kufanya mazoezi sasa, angalia jinsi afya yako itakuwa hovyo baadaye.

SIRI YA 5; Kubali ukweli kwamba kila mara kuna vitu zaidi vya kufanya.

9. Kwenye kila eneo la maisha yetu, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kifamilia, kuna jambo zaidi tunalohitaji kufanya. Kuna ripoti ya kumalizia, kuna simu ya kupiga, kuna mahesabu ya kufanya, kuna usafi wa kufanya, kuna vitu vya kupanga. Ukipeleka siku yako kwa kufanya kila unachoona kinafaa kufanya, utashindwa kutumia muda wako vizuri.

10. Maliza kazi yako kwa muda uliopanga kumaliza, na siyo kwa kufikiria utamaliza kila unachotaka kufanya. Panga muda wa kuanza na kumaliza kazi fulani na muda huo unapofika acha, usiendelee kufanya kwa sababu tu unaona yapo mambo ya kufanya. Kwa kujiwekea ukomo wa muda kama hivyo unathamini muda wako na kuupa kipaumbele.

SIRI YA 6; Mara zote beba kijitabu cha kuandika (NOTEBOOK).

11. Akili yako haiwezi kukumbuka kila kitu unachotaka kukumbuka. Na kuibebesha akili yako vitu vingi ni kuichosha na kushindwa kufikiria yale ambayo ni muhimu. Ndiyo maana watu wenye mafanikio wanajua siri ya kuwa na kumbukumbu na kutumia vizuri muda wao ni kuwa na kijitabu cha kuandika mambo muhimu kwao.

12. Kuwa na kijitabu cha kuandika mambo muhimu popote unapokuwa. Unapopata wazo lolote zuri, liandike, unapojifunza kitu kipya kiandike. Kwa njia huu hutasahau mambo na pia hutaichosha akili yako.

SIRI YA 7; Barua pepe ni njia ya wengine kukudhibiti wewe.

13. Dunia tunayoishi sasa, barua pepe ni moja ya mifumo muhimu ya mawasiliano. Kazi nyingi zinafanyika kwa njia ya barua pepe. Pamoja na uzuri huu wa barua pepe, pia zimekuwa changamoto kwenye matumizi ya muda. Watu wamekuwa wakijikuta wanatumia muda mwingi kusoma na kujibu barua pepe wakati hata siyo muhimu sana. Na hili pia limekuwa tatizo kwenye mitandao ya kijamii na hata simu.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Matumizi Mabaya Ya Mtandao Wa Intaneti Na Kutumia Vizuri Muda Wako Kujiongezea Kipato.

14. Usikubali muda wako utawaliwe na wengine kupitia barua pepe, simu na hata mitandao ya kijamii. Hivyo mara zote panga muda maalumu unaoingia kwenye barua pepe, mitandao ya kijamii au kujibu jumbe za kwenye simu. Muda mwingine uweke kwenye kazi ambazo ni muhimu zaidi.

SIRI YA 8; Hudhuria ile mikutano ambayo ni muhimu tu kwako, mingine angalia njia rahisi ya kunufaika nayo.

15. Katika ulimwengu wa kazi na biashara, hakuna kitu kinapoteza muda kama mikutano. Kumekuwa na mikutano mingi ambayo hata haina umuhimu, watu wanakaa na kubishana mambo ambayo hata hawaji kuyatumia. Watu wenye mafanikio wanaepuka sana mikutano ambayo siyo muhimu kwao.

16. Punguza idadi ya mikutano unayohudhuria, hudhuria ile ambayo ni muhimu tu, ambayo kwa kuhudhuria unaongeza thamani zaidi kwako na kwa wengine. Usihudhurie mkutano kama hakuna anayekulipa, usihudhurie mkutano kama hujui ajenda na pendelea zaidi mikutano ya kusimama.

SIRI YA 9; Sema HAPANA kwa kila kitu ambacho hakina msaada kwenye mipango yako.

17. Watu waliofanikiwa wanatumia neno moja muhimu sana kulinda muda wao, neno hilo ni HAPANA. Kwa kuwa muda ni mdogo na mambo ya kufanya ni mengi, njia pekee ya kupata muda wa kufanya yale muhimu ni kukataa kufanya yale ambayo siyo muhimu. Watu wengi watataka kutumia muda wako kwa manufaa yao, sema hapana.

18. Moja ya changamoto inayowakumba watu mpaka wanashindwa kusema hapana ni kuogopa watu watawachukuliaje. Watu wanajali sana kuhusu namna wanavyoonekana kwa wengine kuliko wanavyofanyia kazi ndoto zao. Kuanzia sasa, mtu anapokutaka ufanye kitu, fikiria kwanza kitu hicho kina mchango gani kwako na kwa wengine, na kama kinaendana na ndoto ya maisha yako. Kama hakiendani sema HAPANA na wala usijali watu wanakuchukuliaje.

SIRI YA 10; Asilimia 80 ya matokeo yako yanatokana na asilimia 20 ya juhudi zako.

19. Watu waliofanikiwa wanajua kwamba juhudi chache muhimu wanazofanya, zina mchango mkubwa kwenye matokeo yao. Yaani asilimia 80 ya matokeo mazuri wanayopata, yanatokana na asilimia 20 ya juhudi wanazoweka. Asilimia 80 ya faida unayopata, inatokana na asilimia 20 ya kazi unazofanya, au wateja wako. Hii ina maana kuna juhudi chache ambazo zina matokeo makubwa, na zipo juhudi nyingi ambazo zina matokeo madogo. Jua zile chache muhimu na komaa nazo.

SOMA; Kama Unafikiri Huwezi Kuwa Bilionea Soma Hapa Na Uanze Kuelekea Kwenye Ubilionea.

20. Usiyape mambo yote uzito sawa, chagua yale muhimu ambayo ukiyafanya, utapata matokeo makubwa, na kazana kuyafanya hayo. Mengine achana nayo.

SIRI YA 11; Tumia muda wako kwenye vile vitu ambavyo wewe pekee ndiyo unaweza kuvifanya.

21. Tofauti nyingine ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni kwenye mambo wanayofanya. Waliofanikiwa wanajua yale mambo muhimu ambayo wanaweza kuyafanya wao tu na wanayafanya, mengine wanawaachia wengine wafanye. Lakini wasiofanikiwa wanakazana kufanya kila kitu, wakiamini ni wao tu wanaweza kufanya kwa ubora.

22. Kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako na kwenye kila siku yako, jiulize maswali haya matatu;

Moja; je naweza kuacha kukifanya kitu hiki bila madhara yoyote kwenye matokeo yangu? Kama ndiyo acha, kama siyo nenda swali la pili.

Mbili; je kuna mtu mwingine anaweza kufanya kitu hiki kwa urahisi na vizuri zaidi. Kama ndiyo tafuta mtu huyo na mpe akifanye. Kama hapana nenda swali la tatu.

Tatu; je nawezaje kukifanya kwa ubora zaidi. Hapa ni kile kitu ambacho unaweza kufanya wewe tu, na unahitaji kukifanya kwa ubora na ufanisi zaidi, ili uweze kupata matokeo bora.

SIRI YA 12; Zipangilie kazi zako kwenye makundi yanayojirudia rudia.

23. Watu wenye mafanikio wanajua siri hii muhimu, hakuna kitu kinapoteza muda kama kufanya kitu, ukaishia katikati halafu ukaenda kufanya kitu kingine. Unaporudi kufanya kile cha kwanza inakuchukua muda mpaka ufike ulikotaka kufika. Pangilia majukumu yako kwa makundi, na tenga muda au siku maalumu ya kufanya kundi la majukumu fulani.

24. Unaweza kutenga siku fulani za wiki zikawa kwa ajili ya majukumu fulani. Mfano siku za jumatatu zikawa siku za kufanya majukumu ya usimamizi, vikao na kufuatilia mengine muhimu. Siku za jumanne zikawa siku za kuboresha zaidi bidhaa au huduma mnazotoa. Siku nyingine ikawa kwa ajili ya masoko na kadhalika. Hii ni kama unaendesha biashara yako mwenyewe.

SIRI YA 13; Kama kitu unaweza kukifanya ndani ya dakika tano, kifanye mara moja.

25. Kitu kikubwa kinachopoteza muda ni kugusa vitu mara mbili. Kwa mfano unafungua email, unasoma na kuona huwezi kujibu sasa hivyo unaifunga na kusema utakuja kuijibu baadaye. Watu wenye mafanikio wamejipa tabia ya kugusa kitu mara moja. Kama kitu wanaweza kukifanya ndani ya dakika tano, wanakifanya mara moja na kuachana nacho.

26. Jijengee tabia hii ya kugusa kitu mara moja tu na kuachana nacho. Unapokutana na jukumu dogo unaloweza kufanya chini ya dakika tano, lifanye mara moja, usiliweke kwenye mlolongo wa vitu vya kufanya, unajikuta una vitu vingi ambavyo havina maana kubwa.

SIRI YA 14; Wekeza dakika 60 kila siku kwa ajili yako wewe binafsi.

27. Watu wenye mafanikio wanajua hakuna uwekezaji muhimu kama uwekezaji kwao wao binafsi. Na hivyo wengi wanaamka mapema na wanatenga angalau dakika 60 kwa ajili yao wao binafsi. Muda huu ni muhimu kwao kuanza siku zao vizuri, kupangilia mambo yao na kupitia ndoto za maisha yao.

28. Kwenye kila siku ya masaa 24, jipendelee saa moja tu na iwe yako. Kwenye saa hii usikubali usumbufu wa aina yoyote, hii ni saa yako wewe binafsi. Na ili uifaidi saa hii, hakikisha unaianza mapema kabisa wakati dunia nzima imelala. Hivyo amka mapema kabisa, saa 10 asubuhi ukiweza au saa 11 asubuhi. Katika muda huu fanya mazoezi, fanya meditation, Sali, pangilia siku yako na jifunze mambo mazuri.

SIRI YA 15; Uzalishaji wenye tija ni namna unavyodhibiti nguvu zako na siyo muda.

29. Watu wenye mafanikio wanajua muda hawawezi kuubadili kwa namna yoyote ile, ila wanaweza kujibadili wao na kutumia muda walionao vizuri. Na njia rahisi ya kujibadili wao, ni kudhibiti na kutumia vizuri nguvu zao. Wanajua wanapoamka asubuhi wanakuwa na nguvu kubwa, hivyo wanafanya majukumu muhimu asubuhi hiyo. Na wanajua ili wapate nguvu zaidi wanahitaji kufanya mazoezi.

30. Masaa mawili ya kwanza kwenye siku yako yalinde na kuyatumia vizuri sana, huu ni muda ambayo unakuwa na nguvu kubwa, hivyo kuweza kufanya makubwa. Muda huu fanya yale majukumu muhimu na magumu, ambayo yana matokeo makubwa kwako. Na ili kupata nguvu zaidi za kufanya makubwa kwenye siku yako, kula vizuri, lala vizuri na fanya mazoezi, kila siku.

Hizo ndizo siri 15 ambazo watu waliofanikiwa wanazitumia kila siku kwenye maisha yao na wanaweza kufanya makubwa, kwa muda huu huu ambao wengine wanaona hauwatoshi.

Kama unavyojua, ukitaka kufanikiwa basi angalia waliofanikiwa wanafanya nini na wewe uanze kufanya. Sasa umeshajua siri 15 za waliofanikiwa kwenye matumizi yao ya muda, zitumie na wewe ili uweze kudhibiti muda wako na kufanya makubwa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita