Hongera rafiki kwa siku hii nzuri sana ya leo.

Ni nafasi nyingine kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

img-20161217-wa0002
Tunakwenda kufanya makubwa leo kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WASICHOFANYA WENGINE,
Kwa bahati mbaya sana, tumezungukwa na watu wengi wa kawaida, ambao wanafanya mambo yao kwa ukawaida na wanaishi maisha ya kawaida.
Na kazi yao kubwa ni kuhakikisha kila mtu naye anakuwa kawaida kama walivyo wao.
Lakini cha kuumiza zaidi ni kwamba kawaida haileti mafanikio, kawaida ni hovyo, kawaida inachosha na kawaida haihamasishi.
Hivyo kazi yetu kubwa ni kuondokana na kawaida, kuipinga kawaida na kuhakikisha tunakwenda mbali zaidi.

Hivyo basi, kwenye juhudi zetu za kuondokana na kawaida, tunahitaji kufanya yale ambayo wengi hawafanyi. Yale ambayo wengine hawawezi kufanya au hawana uvumilivu wa kutosha kuweza kuyafanya.
Na siyo mambo makubwa sana wala ya siri, ni mambo madogo madogo ya maisha ya kila siku.
Kama;
1. Unavyotumia muda wako.
2. Unavyofanya kazi zako.
3. Unavyoendesha biashara yako.
4. Unavyohusiana na wengine.
5. Unavyoendesha siku yako.

Hatari ni kwamba utakapokuwa unafanya kile ambacho wengine hawawezi kufanya, hawatakaa kimya. Watakusema sana, kwamba wewe siyo wa kawaida, kwamba unajisumbua, kwamba ridhika na kuwa kawaida.
Kitu muhimu ni kimoja, usimsikilize mtu wa kawaida anapokuambia ni namba gani uishi maisha yako.
Fanya kisicho cha kawaida ili upate matokeo yasiyo ya kawaida.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz