Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao utatuwezesha kupata chochote tunachotaka.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DEAD-END.
💥Wapo watu ambao wapo kwenye kazi ambayo hawaoni kesho bora kwao. Wanachoona ni kazi ambayo leo ni kama jana na kila siku mambo yanazidi kuwa hovyo zaidi. Hakuna kitu ambacho mtu anajifunza kwenye kazi hiyo na haimpi hamasa yoyote ile.
💥Wapo watu ambao wako kwenye biashara ambazo hakuna popote zinapoenda, biashara zipo vile vile kila siku, hakuna kipya kinachotokea, kila siku biashara inazidi kudhoofika.
💥Wapo watu ambao wanaishi leo kwa sababu waliishi jana, hawana chochote kinachowahamasisha, maisha yamekuwa mazoea kwao na hawaoni maisha yakiwa bora zaidi kwa siku zijazo. Wanachoona ni hali kuzidi kuwa mbaya zaidi kadiri siku zinavyokwenda.
Hizi hali ndiyo zinaitwa DEAD-END,
Ni sawa na kufuata njia halafu ukafika mahali na njia ikawa imeishia pale, haiendelei tena.
Hii ni hali ya kukatisha tamaa na wengi wakishafika hapo wanaona hakuna jipya tena kwenye maisha yao.
Hakikisha hufiki kwenye hali hiyo kwa kuwa na ndoto kubwa za maisha yako ambazo unazifanyia kazi kila siku. Kila siku unapoamka ziandike ndoto zako na kila siku piga hatua kuelekea kwenye ndoto hizo.
Kama umeshafika kwenye hali hii, maana yake huna ndoto kubwa au umesahau ndoto zako. Hivyo kaa chini na tengeneza ndoto yako kubwa na hakikisha unaiishi kila siku.
Usikubali kuwa kwenye maisha ambayo hayana jipya, yanachosha na kukatisha tamaa.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako, Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT