Kwenye maisha, wapo watu ambao wanafanya mambo makubwa na ya kushangaza bila ya kujali wameanzia wapi, na wapo watu ambao wanafanya mambo ya kawaida kabisa kama ambavyo kila mtu anafanya. Wale ambao wanafanya makubwa, ni wachache sana na wanapata mafanikio makubwa. Wale ambao wanafanya mambo ya kawaida ni wengi na maisha yao ni ya kawaida sana.

 

Grant Cardone, kupitia maisha yake, amejifunza kwamba kama unataka kufanikiwa kwenye maisha lazima upende sana kile ambacho unakifanya. Lazima uwe tayari kukifanya kwa hamasa kubwa hata kama wengine hawafanyi hivyo. Na lazima uwe tayari kufanya hata kama wengine wanakukatisha tamaa, kukubeza au kukucheka.

Grant anatushirikisha namna kupenda kile anachofanya kumeweza kuokoa maisha yake kutoka kwenye umasikini na matumizi ya madawa ya kulevya mpaka kufikia kuwa milionea. Hakuna na chochote cha kuanzia, bali alianza kama wakala wa uuzaji wa magari na kupenda sana kile alichokuwa anafanya. Alianza kuweka maono na malengo makubwa sana ambapo kila mtu alikuwa akimcheka. Kwa kila lengo alilokuwa nalo, alilizidisha mara kumi na kuanza kulifanyia kazi. Kwa njia hii aliweza kufanya makubwa kuliko ambavyo alikuwa akitegemewa.

SOMA; Vitu Muhimu Unavyotakiwa Kuwa Navyo Ili kufanikiwa Kwa Kile Unachofanya.

Kama kuna kitabu kimoja ambacho nakushauri wewe rafiki yangu ukisome, basi ni kitabu hichi BE OBSESSED OR BE AVERAGE, ni hazina ya mafanikio. Mambo mengi utakayojifunza kupitia kitabu hichi unaweza kuwa na wasiwasi nayo, na kuona labda wengine watakushangaa na kukuona umechanganyikiwa. Lakini ukweli ni kwamba kama hakuna anayekushangaa na kukuona umechanganyikiwa, haupo kwenye njia ya mafanikio, badilika haraka.

Hapa nakwenda kukushirikisha machache sana kati ya mengi niliyojifunza kwenye kitabu hichi. 

Naomba nisisitize, ninachokushirikisha hapa ni sehemu ndogo sana, kama punje tu ya hazina kubwa iliyopo kwenye kitabu hichi, muhimu sana wewe pia ukae chini na kukisoma.
Karibu upitie haya machache;

1. Jamii ina tafsiri mbaya pale unapoonekana unapenda sana kile unachofanya. Pale unapofanya kazi muda wa ziada, pale unapozungumzia fedha kila mara, pale unapoweka mipango ya mabilioni na pale unapofanya kazi au biashara zaidi ya moja. Jamii itakuambia usijisumbue sana, pumzika kidogo, acha kujidanganya na maneno mengine kama hayo. Usisikilize maneno ya aina hii, kama kuna kitu unakipenda sana, kipende vile utakavyo na kifanyie kazi usiku na mchana.

2. Kila mtu ana nguvu ya kupenda kitu ndani yake. Changamoto ni kwamba nguvu hiyo unaipeleka wapi. Wapo ambao wanapeleka nguvu hiyo kwenye kufanya kazi, wapo wanaoipeleka kwenye kusaka fedha na wapo wanaopeleka nguvu hiyo kwenye ulevi na uteja. Wapo pia wanaopoteza nguvu hiyo kwa kupenda vitu ambavyo havina faida kwao, mfano kufuatilia maisha ya wengine, udaku na hata habari.
Unachohitaji wewe ni kuchagua eneo la maisha yako unalotaka kufanikiwa na peleka nguvu yako ya kupenda kwenye eneo hilo, usisikilize maneno ya watu wanaokukatisha tamaa.

3. Huhitaji kufanya kile ambacho unakipenda ndiyo ufanikiwe, bali unahitaji kupenda kile unachofanya sasa. Watu wengi wamekuwa wakijidanganya kwamba pale walipo sasa hawapapendi na hivyo kutoweka juhudi kubwa, mwishowe wanajikuta wamenasa pale pale, iwe ni kazi au biashara.

Siri ni hii rafiki, anza kupenda hapo ulipo sasa, anza kuweka juhudi zako zote kwenye kile unachofanya sasa, hata kama ni kazi ambayo inadharaulika na kila mtu. Wewe ipende sana, ifaye kwa juhudi kubwa, ijue zaidi ya watu wengine wowote wanaoijua. Kwa kufanya hivi utapata matokeo mazuri sana na baadaye utaweza kutoka hapo na kwenda kwenye kazi au biashara nyingine unayoipenda zaidi.

4. Wale wanaopenda kila wanachokifanya, na kujitoa kukifanya kwa moyo wao wote ndio wanaoitawala dunia, ndiyo wanaoiendesha dunia, ndiyo wanaokuja na njia mpya na bora zaidi za kufanya mambo. Hawa ndiyo watu ambao kila mtu anatamani kuwa kama wao, kwa kufikiri wana siri fulani kubwa, kumbe hakuna siri.

Siri tayari unayo hapo ulipo, weka juhudi kubwa sana, penda sana unachofanya na kifanye kwa moyo mmoja.

SOMA; Sababu 7 Zinazokufanya Upoteze Hamasa Kwa Kile Unachokifanya.

5. Chochote unachopenda kufanya sasa, hapo ulipo, unaweza kukigeuza kuwa sehemu yako ya mafanikio. Unaweza kukigeuza kuwa sehemu ya dunia kukujua wewe, kuwa sehemu ya kutoa thamani kwa wengine na kufanya makubwa sana.

Kipaji chochote ulichonacho sasa, kitumie vizuri, chochote unachopendelea kukifuatilia, angalia ni namna gani unaweza kuongeza thamani kwa wengine na wao wakakulipa wewe. Watu wanalipwa kwa mambo ambayo hatukuwahi kufikiri yanafaa kulipiwa. Tuoneshe kile unachokipenda sana, kifanye kwa viwango vya hali ya juu na dunia nzima itakuwa tayari kukupa fedha ili kupata thamani hiyo.

6. Unahitaji kuwa na ndoto kubwa sana ambazo zinakutisha wewe mwenyewe. Ndoto ambazo wewe mwenyewe huna uhakika wa kuzifikia. Ndoto ambazo wengine wakizisikia wanasema huyu mtu amechanganyikiwa. Halafu kila siku ziandike ndoto hizo na kila siku piga hatua kuelekea kwenye ndoto hizo.

Njia ya kuanza kutengeneza ndoto hizo ni kuchukua ndoto au malengo uliyonayo sasa na kuzidisha mara kumi. Kama lengo lako ni kujenga nyumba moja, fikiria kujenga nyumba kumi, kama lengo lako ni kuwa na bilioni moja, anza kufikiria bilioni kumi.

Huenda usifikie ndoto hizo kubwa, lakini hutabaki hapo ulipo. Kwa mfano anayefikiria nyumba moja, anaweza akaipata au asiipate. Ila wewe unayefikiria nyumba kumi, unaweza kupata hata nyumba tatu, maana namna yako ya kufikiri ni tofauti. Nyumba tatu kwa vyovyote vile ni bora kuliko nyumba moja.

7. Jiandae kupingwa, kudharauliwa, kusemwa vibaya na kuchekwa na wale wanaokuzunguka, pale utakapoanza kufanyia kazi ndoto zako. Utakapoanza kusema ndoto zako hadharani, na ni muhimu uziseme, watu watasema umechanganyikiwa. Ndugu zako wanaweza kujaribu hata kukutafutia daktari. Hivi ndivyo watu wote waliofanikiwa sana walivyopitia.
Wengi hawatakuelewa kwa sababu hawajawahi kuona kile unachosema utafanya kikiwa kinafanyika. Na hivyo wataona wewe huwezi kufanya. Usiwasikilize, wewe fanya.

8. Usivumilie kitu chochote ambacho hukipendi kwenye maisha yako, hata kama kila mtu anavumilia, hata kama kila mtu anachukulia kawaida. Kama kitu hukipendi, au kama unaona siyo viwango vyako, usikubaliane nacho, wewe fanya kazi kupata kile unachotaka, kile ambacho ni viwango vyako.

Waliozoea shida watakushawishi na wewe uzoee shida, walioshindwa kufanikiwa kwenye kazi zao watakushawishi na wewe uwe kama wao. Walioshindwa kukuza biashara zao watakuwa wa kwanza kukushawishi wewe usiingie kwenye biashara wanazofanya, kwa sababu siyo nzuri, hazilipi. Nani alitunga hiyo sheria? Usikubaliane nao, kama kitu unakipenda, au kama kitu huridhishwi nacho, chukua hatua.

9. Epuka kuwa kawaida, ogopa sana kuzungukwa na kushauriwa na watu wa kawaida. Kuwa kawaida ni kuchagua kuwa hovyo, hakuna mtu anapenda kitu cha kawaida, kila mtu anapenda kitu cha tofauti, kitu cha kipekee.

Watu wa kawaida wanapenda kuzungukwa na watu wa kawaida. Utakapokataa kuwa kawaida, wale wa kawaida wanaokuzunguka hawatafurahia hilo, hivyo watafanya kila juhudi kuhakikisha unarudi kuwa wa kawaida. Ndiyo maana unahitaji kuwa makini sana na wale wanaokuzunguka.

10. Chochote ambacho unafanya, chochote ambacho unaruhusu mikono yako kushika, chochote ambacho unaruhusu kibebe jina lako, basi kimiliki kwa asilimia 100. Usikubali kabisa kufanya kitu juu juu au kwa kawaida kwa sababu tu hakikuhusu wewe moja kwa moja. Miliki kile unachofanya, miliki maisha yako, miliki muda wako na miliki fedha zako. Simamia kila unachofanya kwa karibu, fuatilia na ujue kila kinachoendelea. Usiamini mtu mwingine ndiyo awe msimamizi wa maisha yako au kile unachofanya. Hata kama umeajiriwa, ile kazi unayofanya kwa mikono yako ifanye kuwa bora sana na ya kipekee.

11. Fedha ni muhimu, kwa vyovyote vile usiibeze fedha, wala kuidharau, wala kujifanya hutaki fedha. Fedha ni muhimu kwenye maisha yetu ya kila siku, na unahitaji kuipenda fedha, kama unataka ije kwako na iwe rafiki yako.

Jamii itajaribu kukufanya uipuuze fedha, utakapozungumzia fedha waziwazi watu watakuona ni mbaya, una tamaa na una dhambi. Ukiwaangalia watu hao wanaokuchukulia hivyo, wote ni masikini, na unaweza kupata jibu kwa nini ni masikini, na kama utataka kuendelea kubali kama wao basi wasikilize.

12. Wapo watu ambao watakuchukia kwa sababu ya mafanikio yako, huna namna ya kuwabadili. Wenye chuki wataendelea kukuchukia, hata kama ungefanya nini. Wataona mafanikio yako na kusema una bahati, au unatumia nguvu za kishirikina kupata mafanikio. Hivyo ndivyo masikini wanavyofikiri mara zote, wala usijisumbue kuwaelewesha, utapoteza muda wako bure na kujikuta unaanza kufikiri kama wewe. Wewe endelea kutimua vumbi, wewe endelea kufanya makubwa, wenye chuki wataendelea kuchukia.

Njia bora kabisa ya kuwaadhibu wale wenye chuki na wewe ni kufanikiwa zaidi. Hakikisha unafanikiwa mpaka watamani kujiua, kwa sababu kila wanapoendeleza chuki zao wewe unafanikiwa zaidi.

13. Muda ni kitu muhimu sana kwenye mafanikio yako makubwa. Usiruhusu watu wachezee muda wako wanavyotaka wao wenyewe. Kuruhusu uwe na muda ambao huna cha kufanya ni kifo cha mafanikio yako. Kujikuta upo mpweke na huna cha kufanya ndiyo mwanzo wa kukaribisha mawazo ya kawaida na kujikuta unaanza kuwasikiliza wale waliokata tamaa na wanaotaka kukukatisha tamaa pia.

Hakikisha kila muda wa siku yako kuna kitu muhimu umepanga cha kufanya, kuanzia kwenye kazi au biashara yako, afya yako, mahusiano yako na kadhalika.
Kuwa bize mpaka wale wanaotaka kukuletea habari za kukukatisha tamaa waone aibu, maana kila wakija kwako na habari zao hasi wanakukuta uko bize na mambo yako.

SOMA; Ni Wakati Gani Unatakiwa Kuacha Kile Unachokifanya, Kama Hakikuletei Matokeo Unayotaka Kabisa?

14. Mafanikio siyo kupata hiki na kukosa kile, siyo kutumia muda mwingi kwenye kazi na kukosa muda na familia, siyo kuwa bize na kazi na kusahau afya yako. Mafanikio ni kuwa na kila kitu, kuwa na fedha nyingi, kuwa na afya bora, kuna na mahusiano mazuri na wengine, kuwa vizuri kiimani na kuweza kushirikiana na wengine.

Unahitaji kulipenda kila eneo la maisha yako, kazi, fedha, afya, imani, mahusiano na kufanyia kazi kila siku ili kuwa bora zaidi.

Usikae chini na kufikiria inabidi ukose hichi ili upate kile, kaa chini na ufikirie unawezaje kupata kila kitu. Wapo waliopata kila kitu, jifunze kutoka kwao.

15. Tumia teknolojia mpya kukuza zaidi kile unachofanya sasa. Kama unafanya biashara hakikisha unatumia mitandao ya kijamii kuwafikia wengi zaidi kupitia biashara yako. Kwa utaalamu wowote ulionao, ujuzi au uzoefu wowote ulionao, tumia mitandao ya kijamii kuhakikisha kila mtu anafikiwa na ujumbe wako.
Mitandao ya kijamii ni njia rahisi ya kuifikia dunia nzima. Usiitumie tu kufuatilia wengine, itumie kuhakikisha watu wanakufuatilia na wewe pia.

Hatua ya kwanza kabisa kwako ni kuwa na blog, unahitaji kuwa na blog ambapo unaandika yale unayopenda na kuishirikisha dunia. Kisha tumia mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe unaotoa kupitia blog yako.

Kama mpaka sasa huna blog, karibu nikutengenezee blog nzuri kwa gharama rahisi kabisa. Tuwasiliane 0717 396 253 (wasap tu).

16. Kuwa na ndoto kubwa, kuandika ndoto zako kila siku haimaanishi zitakuja kirahisi. Unahitaji kutokwa jasho, machozi na hata damu. Utahitaji kufanya kazi sana, siyo kidogo. Kuna wakati utaumizwa na kuona huwezi kuendelea tena. Kuna wakati utakutana na vikwazo vya kukukatisha tamaa. Lazima ujiandae na haya yote kama kweli unataka kufikia ndoto yako.

17. Ili kuweza kuweka kazi kuba unayohitajika kuweka ili kufikia ndoto zako, lazima afya yako iwe vizuri. Bila afya imara, huwezi kufanya makubwa, huwezi kufika popote.
Afya yako ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako. Kula vizuri, pata muda wa kupumzika na fanya mazoezi. Mazoezi yanaupa mwili wako nguvu zaidi ya kuweza kufanya makubwa zaidi.

18. Mtu yeyote ambaye anafanya kazi yako, hakikisha ana ule mtizamo ambao wewe unao kwenye kazi yako. Kama umeajiri au una wasaidizi, hakikisha wana mtizamo ule ambao unao wewe. Hakikisha wana hamasa uliyonayo wewe, na hakikisha kila wakati wana fikra sahihi za kufanikiwa kupitia kile wanachofanya.

Unahitaji kufanya hivi kwa kuhakikisha upo nao karibu, kwa kuhakikisha una mikutano ya kila siku na wale wanaokusaidia. Kila wakati jua mtu anafanyia kazi nini na changamoto zipi anakutana nazo.

Unapokuwa karibu na wale wanaokusaidia, unawapa uhakika wa kile wanachofanya na kuacha kubashiri wao wenyewe.

19. Usisubiri mpaka uwe umekamilika ndiyo uanze kitu. Kusubiri kukamilika kumeua ndoto za wengi, kumezuia wengi kuanza na hata kufanikiwa.
Kama unataka kufanya biashara fulani, anza kuifanya leo, anzia hapo ulipo sasa, usisubiri mpaka ukamilike, hutakuja kufikia mahali na ujione umekamilika.
Kama kuna kitabu unataka kuandika, anza kukiandika leo, kiandike kwa maarifa uliyonayo sasa, na kama hakitakuwa bora baadaye unaweza kukiboresha zaidi.
Usijidanganye hujawa tayari, upo tayari kuanza chochote unachotaka kuanza, anza sasa.

20. Kitabu hichi ni ufunguo wa maisha yanayowezekana kwako, ni ufunguo wa uwezo mkubwa ambao upo ndani yako na ni ufunguo wa uhuru wa maisha yako. Tumia maarifa haya kuweka juhudi kubwa kwenye chochote ambacho umechagua kufanya. Tumia maarifa haya kuepuka kurudishwa nyuma na wengine na tumia maarifa haya kuepuka kukata tamaa na kuacha pale unapokutana na magumu.

Kitu kimoja muhimu sana kukumbuka ni kwamba juhudi zinahitajika, uvumilivu unahitajika na kukata tamaa ni mwiko.

Nakusihi sana wewe rafiki yangu soma kitabu hichi, kisome na fanyia kazi yale ambayo unajifunza, mengi niliyoyasoma nimejikuta nilikuwa nayafanyia kazi tangu zamani na yamekuwa yananisaidia sana. Nina uhakika na wewe yatakusaidia pia.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita