Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi zaidi kwenye kile tunachofanya ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.
Tutumie nafasi ya leo vizuri rafiki, kwa sababu muda huu ukipita, hatutauona tena.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu OWNERSHIP, yaani UMILIKI WA KILA TUNACHOFANYA.
Chochote ambacho unaruhusu kichukue muda wako, chochote ambacho unaruhusu mikono yako ikishike, basi kimiliki moja kwa moja, kwa asilimia 100.
Usifanye kitu chochote kwa kugusa gusa tu, bali miliki kila unachofanya, miliki maisha yako. Yachukue majukumu yako kama sehemu ya maisha yako, na weka kila unachoweza ili kuhakikisha unayafanya vizuri.
Kwenye biashara miliki biashara yako, miliki wateja wako. Mteja anapokuja kwako hakikisha unamchukulia ni jukumu lako wewe kumpa kile ambacho amekifuata.
Kwenye kazi miliki majukumu yako, miliki wale ambao wanakutegemea katika utekelezaji wa majukumu fulani.
Usijaribu kukwepa au kukimbia majukumu yako.
Na muhimu zaidi, miliki maisha yako, kila eneo la maisha yako lifanye kuwa jukumu lako. Usiwape wengine jukumu lolote, na kwa maana hiyo basi usimlalamikie yeyote kwa kinachoendelea kwenye maisha yako.
Kama maisha ni magumu jua hilo ni jukumu lako na kama kuna unakotaka kufika na maisha yako ni jukumu lako.
Hakuna kitu kinacholeta uhuru kama umiliki, hivyo hakikisha unamiliki chochote unachofanya na maisha yako pia.
Wanamafanikio wote ni WAMILIKI, lazima na wewe uwe mmiliki.
Nakutakia siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info