Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine ya kipekee, ambapo tunakwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora.

Siku ya leo tunakwenda KUTHUBUTU, KUSHINDA NA KUSHUKURU.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UVUMILIVU NA KASI.
Hakuna mtu ambaye hapendi kuwa na maisha bora na ya mafanikio,
Lakini changamoto kubwa inaanzia kwenye uvumilivu na kasi.
Ili ufanikiwe, ili ufikie ndoto zako, unahitaji kuwa na uvumilivu, kwa sababu hutapata unachotaka ndani ya siku moja. Haipo njia ya mkato ya kukupa chochote unachotaka. Unahitaji muda ili kuweza kufika pale unapotaka.
Lakini kwenye kufanya mambo yako ya kila siku, unahitaji kasi,
Unahitaji kuwa na kasi katika kutekeleza yale uliyopanga kutekeleza kila siku, kwa sababu muda ndiyo kikwazo kikuu kwetu.
Cha kushangaza, watu wanageuza hilo la uvumilivu na kasi,
Wanataka mafanikio na wanayataka sasa, tena kwa haraka, hawana muda wa kusubiri. Lakini kwenye yale mambo wanayofanya kila siku, hawana kasi yoyote, hawana hata vipaumbele, wanafanya tu kama wanavyojisikia.
Kwa hali hii wanajikuta wameingia kwenye njia ambazo zinawapoteza zaidi ya kuwafikisha kwenye mafanikio.
Kwa kuwa hawans uvumilivu, wanatafuta njia za mkato, ambazo siyo za kweli hivyo wanapoteza muda, nguvu na hata fedha.
Rafiki, kuwa na uvumilivu katika kufikia ndoto zako, lakini kuwa na kasi katika kutekeleza majukumu yako ya kila siku.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.