Habari za leo rafiki yangu?

Leo ni tarehe 01/04/2017 hii ina maana kwamba mwezi wa kwanza umeisha, wa pili umeisha na wa tatu tumeumaliza hapo jana. Kwa kuwa mwaka una miezi 12, ukigawa kwa nne, unapata miezi mitatu. Mpaka sasa, kwenye mwaka huu 2017 tumeshamaliza robo ya kwanza. Na leo tumeanza robo ya pili rasmi.

 

Sasa kabla hatujaendelea na robo hii ya pili, ni vyema tukafanya tathmini ya robo ya kwanza ya mwaka huu 2017. Imekwendaje, tumefanya nini, yapi ambayo hatujafanya na hatua zipi za kuchukua.

Kabla sijakupa maswali ya kutafakari robo ya kwanza ya mwaka, naomba nikuambie haya muhimu sana kwa maisha yako, kwa mwaka huu 2017 na miaka mingi ijayo.

Kuna kauli moja ambayo ninapenda sana kuitumia, kauli hii ni kwamba UNAPATA KILE UNACHOTAFUTA. Hivyo ni muhimu sana ujue kwa hakika ni nini unatafuta.

Ambacho nimekuwa najifunza kwa wengi ni kwamba, unaweza kuwa unatafuta matokeo, au unatafuta sababu. Chochote kati ya hivyo viwili, ukikitafuta kisawasawa utakipata, bila ya ubishi wowote.

Cha kushangaza na kusikitisha sana, watu wamekuwa wanatumia muda mwingi kutafuta sababu zaidi ya kutafuta matokeo. Kwa sababu kupata matokeo ni kugumu, na kwa sababu wengi hawapendi ugumu, basi wanakimbilia kilicho rahisi, ambacho ni kuja na sababu kwa nini kile walichopanga hawawezi kukitimiza.

SOMA; SOMA; Chanzo Kikubwa Cha Mabadiliko Ya Maisha Yako, Kinaanzia Hapa.

Mwezi wa kwanza kila mtu alikuwa na kilio kimoja, ‘january ngumu’. kila mtu unayekutana naye utasikia akisema, lakini si unajua ni january hii, mambo magumu bwana. Yaani january ikiisha tu, basi mambo yanakwenda poa. Wengine wakatengeneza mpaka utani kwamba mwezi january ni mwezi mrefu sana, kwamba umegoma kuisha.

Mimi huwa sikubaliana na vitu kama hivi hata siku moja, hivyo sikutaka kubishana na watu, bali nilikuwa nawaambia kitu kimoja, kama january ni ngumu, basi tusubiri february tuone jinsi ambavyo fedha zitakuwa zinamiminika zenyewe kwenye mifuko ya watu.

January ikaisha, ikaingia february, tatizo likaendelea kuwa lile lile, lakini sasa sababu ikabadilishwa. Ikawa tena siyo mwezi ni mgumu, bali Magu kabana. Kila mtu utamsikia kwamba Magu kabana kila kona, mambo hayaendi na sababu nyingine kama hizo. Wapo wanaotabiri kabisa ya kwamba uchumi utaanguka na mambo yatakuwa mabaya zaidi. Lakini mimi huwa siendi na hayo, huwa sitafuti sababu za kujipooza, ninachojua ni kimoja, kama kipo kitu unataka, unaweza kuweka juhudi zako kukipata, au unaweza kutafuta sababu. Huwezi kufanya vyote kwa pamoja, ndiyo maana hutanisikia nikikupa sababu zozote, badala yake nitatumia muda huo kufanya, na siyo kwamba nitapata kila mara, bali nitajaribu mara nyingi iwezekanavyo, nikijua ya kwamba kama nitaendelea kukomaa, basi dunia itanichoka tu na kunipa kile ninachotaka.

Hivyo rafiki yangu, nakusihi sana, achana na sababu, achana nazo kabisa, zifute kabisa kwenye maisha yako. Weka akili na mawazo yako yote kwenye kutengeneza matokeo. Wanaokuzunguka watakujia na habari za hofu kwamba kila kitu kinaharibika, lakini wewe achana nao, ambana, na ninakuhakikishia, utapata kile unachotaka. Sikuhakikishii kwamba utapata mara ya kwanza, lakini ninachokuhakikishia ni kwamba, kama hutokata tamaa, lazima utapata kile unataka. Hivyo weka sababu pembeni na weka kazi.

Soma; Wacha Maneno Weka Muziki…

Baada ya kukupa msingi huo muhimu rafiki, sasa turudi kwenye mada yetu ya leo ambayo ni tathmini muhimu kwa robo hii ya mwaka ambayo tumeshaitafuta. Unakumbuka nilivyokuambia kwamba muda haurudi tena nyuma. Hivyo robo hii uliyotafuna hutaiona tena.

Nakusihi rafiki yangu, kaa chini kwa japo nusu saa (najua wengi litakuwa zoezi gumu, lakini fanya), jiulize na kupata majibu ya maswali haya muhimu. Andika majibu yake na nitumie majibu hayo.

Zoezi hili litakusaidia sana kujua kwa hakika uko wapi na kama utaweza kufanya makubwa kweli kwa mwenendo unaoenda nao sasa. Pia yatakufanya ujue kama unahitaji mabadiliko kwenye safari yako ya maisha.

Maswali muhimu ya kutafakari na kujipa majibu ni haya.

1. Unayakumbuka mambo matatu muhimu uliyopanga kuyafanyia kazi mwaka huu 2017?

2. Je umefikia wapi kwenye kila jambo mpaka leo hii?

3. Je umeshaanza biashara au kukuza biashara yako kwa mwaka huu? Kipi cha tofauti ambacho umefanya kwenye biashara yako?

4. Je kwa miezi mitatu iliyopita, umekuwa unajilipa wewe mwenyewe kwanza kwa kutenga sehemu ya kumi ya kila kipato chako? Kama hapana kwa nini?

5. Je umefanya uwekezaji wowote katika kipindi hichi? Ni uwekezaji gani?

6. Je umesoma vitabu vingapi katika miezi hii mitatu? Nitajie vitabu ulivyosoma na kitu kimoja kikuu ulichojifunza kwenye kila kitabu. Kama hujasoma kitabu chochote mpaka sasa ni kwa nini?

7. Kwa jinsi ambavyo unaenda mpaka sasa, unajiona ukifanya makubwa mwaka huu 2017? 
Kama hapana, wapi unahitaji kubadili?
Rafiki yangu, naomba utenge nusu saa, jiulize maswali hayo na andika majibu kwa ajili yako, pia nitumie majibu hayo, nitafurahi kujua unaendeleaje. Hata kama hujachukua hatua yoyote niandikie, sitakucheka, bali nitajitahidi sana kukushauri uanze na nini.

Zoezi hili litakuchukua nusu saa, lakini majibu yake yatakuwa na manufaa makubwa sana kwako. 

Lifanye leo hii na kisha nishirikishe majibu yako. Kama umepokea kwa email jibu email hii kwa majibu yako. Kama umesomea kwenye blog niandikie majibu kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Nasubiri kwa hamu kubwa kusikia kutoka kwako rafiki yangu. Bado mwaka 2017 tunao, usikate tamaa kwa namna yoyote ile, endelea kuweka juhudi na utaweza kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.