Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu dunia kutokuacha kirahisi.
Kamwe dunia haitakuacha kirahisi, upate kila ambacho unataka kupata.
Dunia itakutesa, dunia itakuzungusha ili tu ukate tamaa.
Na ukikata tamaa ndiyo kamwe hutapata kile unachotaka.
Ila kama utaendelea kuwa mbishi na kuendelea kupambana, dunia itafika mahali na kukupa kile ambacho unataka.
Haitaweza tena kuendelea kupambana na wewe, na hapo utapata kile unachotaka.
Vitu vyote vizuri, dunia imevificha,
Hebu angalia madini ya thamani, yapo chini sana ardhini, lazima uchimbe sana ndiyo upate madini hayo.
Dunia haikupi tu madini kirahisi, ni mpaka upambane sana ndiyo uyapate.
Angalia hata mazao ya kilimo, hayaoti tu yenyewe na wewe ukavuna,
Badala yake inabidi ulime vizuri, upande, uweke mbolea, uyahudumie ndiyo uweze kuvuna.
Chochote unachokifanya kwenye hii dunia, jua wazi ya kwamba, hakitakuwa rahisi, upinzani wako wa kwanza utatoka kwenye dunia yenyewe, kwenye ugumu wa jambo lenyewe.
Halafu sasa bado kuna wale wanaokuzunguka, nao pia hawatakuacha kirahisi.
Hivyo rafiki, chochote unachotaka, jiandae kupambana, na siyo kidogo.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.