Barua Ya Wazi Kwa Wazazi Wa Kizazi Kipya (Kama Una Miaka Chini Ya 40 Soma Hapa).

Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye makala yetu ya ambapo tunakwenda kushirikishana yale muhimu kwa maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Leo nimewaandikia barua wazazi wote wa kizazi kipya. Na kabla hatujaingia kwenye barua yenyewe, lazima kwanza tujue wazazi wa kizazi kipya ndiyo wapi.

 

Wazazi wa kizazi kipya ni wale wote ambao wamepata watoto wao kwenye karne hii ya 21. 

Yaani kama umeanza kupata watoto kuanzia mwaka 2000 na kuendelea, basi wewe ni mzazi wa kizazi kipya. Ukiangalia kwa hesabu za haraka haraka za miaka, walioanza kupata watoto miaka hii ya 2000, wengi watakuwa na miaka chini ya 40. Japo wapo wachache ambao watakuwa na miaka zaidi ya hiyo.

Hii ndiyo maana hapo juu nimeeleza kama una miaka chini ya 40, iwe una mtoto au la, ni muhimu kusoma, maana itakusaidia. Pia kama una miaka zaidi ya 40 unaweza kusoma kwa sababu pia inaweza kukusaidia, kama bado hujachelewa sana, au unaweza kuwashauri watoto na ndugu zako wengine ambao ni wazazi wa kizazi kipya.

SOMA; Huyu Ndiye Adui Namba Moja Kwenye Malezi Ya Watoto.

Hivyo basi karibuni sana wote kwenye barua hii ya wazi;

Barua ya wazi kwako mzazi wa kizazi kipya,

Kutoka kwa kocha na rafiki yako, Makirita Amani.

Nikupongeze kwa uzazi na malezi bora kwa sababu hakuja jukumu muhimu na gumu kama la uzazi na ulezi. Hii ni kwa sababu watoto wanakuja duniani bila ya kitabu cha maelekezo, hivyo ni kujaribu na kukosea katika malezi. Kila mtoto anakuja na changamoto zake na hakuna aliye na uzoefu wa kutosha katika eneo la malezi. Kila mtu anajifunza kadiri mambo yanavyokwenda.

Barua yangu hii nataka kukushirikisha mambo muhimu matatu kuhusu uzazi na malezi kwenye karne hii ya 21. Hii ni kwa sababu tunaishi kwenye mabadiliko makubwa sana ukilinganisha na enzi walizoishi wazazi wetu. Enzi zao wakati wanatuzaa na kutulea, hapakuwepo na mabadiliko haya makubwa yaliyopo sasa. Na hata maadili yalikuwa yakichukuliwa tofauti na inavyochukuliwa sasa. Mabadiliko yanaendelea kutokea na kila mzazi na mlezi lazima aendelee kubadilika.

SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.

Jambo la kwanza ninalotaka kukushirikisha ni kuhusu kuwekeza kwa watoto. Wazazi wa kizazi kilichopita, walijitahidi sana kupata watoto wengi, wakiamini kwamba kadiri unavyokuwa na watoto wengi, ndivyo unavyopata msaada zaidi unapokuwa mzee. Hivyo walifanya watoto kama uwekezaji wao wa baadaye, kwamba wakishachoka basi watoto watawasaidia. Siyo jambo baya, ni jambo zuri kwa sababu watoto wamezaliwa na kutunzwa na ni moja ya wajibu wao kuwatunza wazazi wao wanapozeeka.

Lakini kwa kizazi cha sasa, sikushauri kabisa utegemee hilo. Kwanza kabisa maisha yanakuwa magumu na hivyo kila mtu anapambana kwanza kupata msimamo wake kwenye maisha. Kingine watu wengi wanachelewa kupata watoto sasa, hivyo unaweza kufika wakati unastaafu kazi, au huwezi tena kupambana na shughuli zako, na kukuta wakati huo hata watoto wenyewe hawajaweza kusimamisha maisha yao vizuri.

Hivyo kwa mzazi wa kizazi kipya, pata watoto, lakini usiwahesabu kama uwekezaji wa baadaye. 

Badala yake wewe fanya uwekezaji wako wa baadaye. Kwa kile fedha unayoipata sasa, tenga sehemu ya kumi na iwekeze. Unaweza kuwekeza maeneo mbalimbali kama ambavyo nimeeleza kwenye makala hii; Njia Nne Za Uhakika Za Kufikia Utajiri, Angalizo; Ajira Sio Mojawapo.

Chukulia kazi yako ya kuzaa na kulea kama wajibu wa kuhakikisha maisha yanaendelea hapa duniani, na usichukulie kama uwekezaji ambao lazima baadaye ukulipe. Utakuja kujikuta unawalaumu bure watoto ambao hata wao hawajapata uhakika wa maisha yao, na hapo ukute nao wana watoto wao.

Jambo la pili ni kuhusu majukumu yako kama mzazi na mlezi.

Katika dhana ile ya zamani ya kupata watoto wengi, siyo wote walikuwa wakipata matunzo mazuri. Wengi hata mlo kamili hawakuwa wanapata, na elimu ndiyo kabisa ilikuwa changamoto. 

Wazazi walikuwa na watoto wengi ambao wanashindwa kuwahudumia vizuri, lakini katika hao wengi kuna wachache ambao wanaweza kupambana wenyewe na kuweza kuwa na maisha mazuri, baadaye wazazi hao wakanufaika nao.

Sasa wewe mzazi wa kizazi kipya usifanye hili. Usikwepe majukumu yako kwa watoto wako. Na hivyo unahitaji kuwa na watoto ambao unaweza kuwalea na kuwahudumia mahitaji yao yote. 

Unaweza kuhakikisha wanapata chakula vizuri, na pia wanapata elimu bora kabisa itakayowawezesha kuwa na maisha ya uhuru.

Usijipe sababu kwamba umeshindwa kuhudumia watoto kwa sababu yoyote ile. Badala yake pambana mno, hata kama hutalala, hakikisha watoto wanapata mahitaji yao ya msingi. 

Hukutumwa uwatafute hao watoto, na hivyo usitake kumbebesha mwingine majukumu yao.

Watoto wako ni jukumu lako, hivyo lipe kipaumbele cha hali ya juu.

SOMA; Ufanyeje Pale Familia Yako Inapopinga Ndoto Zako?

Jambo la tatu ni kuhusu urithi na maisha ya baadaye ya watoto.

Wazazi wengi wa zamani, ambao walifanikiwa kupambana na kuwa na maisha mazuri, hawakutaka watoto wao wateseke kama wao. Hivyo waliwaandalia maisha mazuri kabisa, wakawaandalia kila walichotaka. Hivyo watoto wao hawakuwa na uhitaji wa kupambana, kila wanachotaka kipo, tayari wana nyumba, wana magari na wana kazi ambazo wamewezeshwa na wazazi wao kupata.

Lakini wengi wa watoto hawa, maisha yao hayakuenda vizuri, hasa baada ya wazazi wao kufariki. Wengi walijikuta wakiuza mali walizoachiwa, au kuendelea kuishi maisha tegemezi.

Usiwajengee watoto wako utegemezi wa moja kwa moja, hata kama una mafanikio makubwa kiasi gani kifedha, usiwafanye watoto waone maishani rahisi kwao kwa sababu wewe ulipambana. Unahitaji uwajengee uwezo wa kupambana pia, kwa sababu dunia siyo rahisi. 

Wanaweza wasikutane na misuko suko wewe ukiwa hai, kwa sababu utakuwa unawasaidia. 

Lakini utakapoondoka utakuwa umewaacha kwenye hatari ya kukumbwa na misukosuko ambayo itawaangusha vibaya.

Kazana sana kuwajengea watoto wako uwezo, uwezo ambao utawawezesha kupambana na changamoto za maisha ya kila siku. Hata kama utawaandalia mali za kurithi, hakikisha kuna kazi kubwa wanazoendelea kufanya ili kweli wastahili kurithi mali hizo. Hakikisha wanajua uchungu wa kupata mali hizo, ili zinapokuwa chini ya mikono yao wazithamini, wakumbuke maumivu ambayo waliwahi kuyapata wakipambana kukuza au kulinda mali hizo.

Hayo ndiyo mambo matatu muhimu ambayo nimechagua kukushirikisha wewe rafiki na mzazi mwenzangu wa kizazi kipya kwenye barua hii ya leo. Kama kipo kitu umejifunza, inafaa sana uanze kukifanyia kazi mapema, ili uweze kulea watoto wenye uwezo mkubwa wa kupambana na maisha na kuweza kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

One thought on “Barua Ya Wazi Kwa Wazazi Wa Kizazi Kipya (Kama Una Miaka Chini Ya 40 Soma Hapa).

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: