Kama ambavyo tumejifunza mpaka sasa, ustoa ni moja ya falsafa nzuri sana za maisha kwa sababu inatupa utulivu ndani ya nafsi zetu na kutuwezesha kuwa na maisha bora bila ya kujali tunapitia nini.
Lakini kuishi falsafa hii ya ustoa kwa mgeni inaweza kuwa changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu wengi wanaweza kukushangaa kwa namna unavyoendesha maisha yako. Ili kuondokana na changamoto hii, yafuatayo ni mambo muhimu sana kuyazingatia.
1. Ishi falsafa ya ustoa kwa ukimya.
Usimtangazie kila mtu kwamba sasa wewe ni mstoa na maisha yako yamebadilika. Badala yake ishi misingi ya ustoa. Utakapoishi misingi hii, wengine wanaweza kuona tofauti kwako na kuuliza, na hapo unaweza kuchagua kuwaambia kama nao watanufaika au usiwaambie.
2. Unapoanza kuishi falsafa hii, usianze kila kitu kwa wakati mmoja. Badala yake anza zoezi moja ukishaliweza vizuri nenda kwenye zoezi jingine.
Kwa kuanza, anza na zoezi la kujenga taswira hasi, kwa kuchukulia kile ulichozoea au unachothamini kimeondoka kwenye maisha yako.
Fanya hivi kila siku, tenge muda mchache wa kujijengeabtaswira hii. Zoezi hili litakuwezesha kuthamini vitu ulivyonavyo.
Baada ya zoezi hilo unaweza kuingia kwenye zoezi la utatu wa udhibiti. Hapa kila linalotokea kwenye maisha yako, unalipanga kutokana na udhibiti ulionao.
Kama lipo kabisa nje ya uwezo wako unaachana nalo, kwa sababu hakuna namna unaweza kuliathiri.
Kama lipo ndani ya uwezo wako kabisa unachukua hatua.
Kama lipo ndani ya uwezo wako kwa kiasim unachukua hatua kwa kile kiasi chako.
Kwenye udhibiti pia utajifunza kuyaelekeza malengo yako ndani na kuchukulia kwamba mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi.
Baada ya mazoezi haya makuu mawili, unaweza kuishi maisha bora kwa falsafa hii ya ustoa.