Habari rafiki,

Karibu kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufanikiwa. Kupitia makala hizi nakushauri kwa zile changamoto unazopitia, hatua gani uchukue ili uweze kufanikiwa.

Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia jinsi ya kuchagua biashara ya kufanya pale unapokuwa na mawazo mengi ya kibiashara. Jambo la kushangaza ni kwamba wapo watu ambao kikwazo kwao ni wazo la biashara, yaani wapo tayari kufanya biashara, lakini hawana wazo zuri la biashara kwao. Kwa upande mwingine wapo watu ambao wanataka kuingia kwenye biashara, ila wana mawazo mengi na hawajui waanze na lipi. Leo tutashauriana na hawa wenye mawazo mengi ya kibiashara.

Kabla ya kuangalia jinsi gani uchague katika mawazo mengi, kwanza tusome maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Mimi ninataka kuanzisha biashara lakini nina mawazo ya aina tatu za biashara, mfano duka, mgahawa na ufugaji wa kuku, mpaka sasa sijui ni biashara gani nifanye kati ya hizo, naomba ushauri. Neema A. U.

Neema, na marafiki wengine ambao mna changamoto kama hii, ni hali ya kawaida kabisa kwa binadamu unapokuwa na machaguo mengi kujikuta unapoteza muda kwa sababu huna uhakika ni chaguo lipi la uhakika kwako. Na kwa kuwa wengi huwa tunapenda kuwa sahihi mara zote, basi inaweza kutuchelewesha sana kama hatuna uhakika njia ipi ni sahihi kwetu.

Yapo mambo muhimu sana ya kuzingatia unapokuwa na wazo zaidi ya moja ya biashara. Na hapo chini nitayajadili kwa kina na kisha kukuambia hatua gani uchukue.

1. Kizuizi kwako ni nini?

Wazungu wanasema limiting factor. Kama tusingekuwa na kizuizi, basi kila mtu angeweza kufanya kila kitu ambacho anafikiria kufanya. Lakini hilo haliwezekani kwa sababu kuna vizuizi kwenye maisha yetu, kulingana na kile ambacho tunafanya. Vizuizi vinaweza kuwa vingi, na kwenye biashara vizuizi muhimu ni kama ifuatavyo;

Moja ni mtaji. Tunapenda kufanya biashara kubwa na nzuri, lakini mara nyingi huwa hatuna mtaji mkubwa wa kuanzia. Hivyo inatubidi kuangalia ni biashara ipi tunayoweza kuanza kwa mtaji kidogo. Hichi ni kizuizi ambacho lazima ukiangalie unapokuwa na mawazo mengi ya kibiashara.
 

Mbili ni usimamizi. Kila mtu angependa kuwa na biashara nyingi awezavyo, lakini usimamizi unapokosekana kinachofuata ni hasara. Haijalishi una mtaji mkubwa kiasi gani, kama huwezi kusimamia biashara zako kwa karibu, utaishia kupata hasara. Na kama huwezi kusimamia biashara zako kwa karibu, usianzishe biashara zaidi ya moja kwa wakati mmoja.


Tatu ni rasilimali. Rasilimali pia zinaweza kuwa kizuizi kwako kuanzisha biashara nyingi. Rasilimali zinaweza kuwa nguvukazi ya watu ya kukusaidia kuendesha biashara hizo na hata rasilimali nyingine ikiwepo maeneo mazuri ya kuweza kufanyia biashara husika.

2. Uwezekano wa biashara tofauti kufanyika pamoja.

Kitu kingine muhimu sana unachopaswa kuangalia pale unapokuwa na wazo zaidi ya moja la biashara ni uwezekano wa biashara hizo kufanyika kwa pamoja. Kuna baadhi ya biashara unaweza kuzifanya kwa pamoja na zikaendana vizuri, lakini zipo ambazo zinatofautiana sana hivyo haziwezi kwenda kwa pamoja. Kwa kuyachambua vizuri mawazo yako ya kibiashara uliyonayo, kunakuwezesha kuona kama mawazo hayo yanaendana au hayaendani.

3. Ukubwa wa ndoto zako kibiashara.

Kitu muhimu pia kuangalia pale unapokuwa na wazo zaidi ya moja la biashara ni ndoto zako binafsi. Pale unapojiona siku zijazo, kunakusukuma kuchukua hatua sasa. Ndoto zinaweza kuwa kizuizi katika kuanzisha na kuendeleza biashara zako. Biashara zako haziwezi kukua zaidi ya ndoto zako. Hivyo ndoto zako zinapokuwa ndogo, unaishia na biashara ndogo, hata kama ungefanya kazi masaa 24 kwa siku na siku 7 za wiki.

Hatua za kuchukua unapokuwa na wazo zaidi ya moja la biashara.

1. Anza na biashara moja kwanza.

Kipaumbele cha kwanza unapokuwa na mawazo mengi ya kibiashara ni kuanza na wazo moja kati ya yale ambayo unayo. Katika mawazo hayo, chagua lolote unaloweza kuanza nalo. Na kigezo cha kuchagua kiwe uwezo wako wa mtaji, namna unavyopenda kufanya wazo hilo na soko ambalo kwa sasa unalilenga. Kwenye mawazo ambayo unayo, angalia lipi ukianza nalo, unaweza kupiga hatua.

Faida ya kuanza biashara moja kwa wakati ni kukupa wewe muda wa kuijua biashara vizuri na kuweza kupambana na changamoto za kibiashara unazokutana nazo, ambazo lazima ukutane nazo. Unapokuwa na biashara zaidi ya moja na zote zikawa na changamoto, itakuwa mzigo kwako zaidi.

Japokuwa utaanza na wazo moja, yale mengine usiyazike kabisa, yahifadhi na utayarudia baadaye ukishaweza kusimamia biashara nyingi kwa pamoja.


2. Kama upo uwezekano, anza biashara mbili kwa pamoja.

Hii inaonekana kupingana na hiyo hapo juu, lakini nitakueleza vizuri kwa kutumia mfano wa rafiki yetu Neema. Yeye ana mawazo matatu ya biashara; mgahawa, duka na ufugaji wa kuku. Ukiangalia kwenye hayo mawazo matatu, ufugaji wa kuku unaweza kwenda na moja ya hayo mawili; mgahawa na duka. Ufugaji wa kuku haumhitaji mtu kukaa na wale kuku muda wote wa siku, bali unamhitaji kuwahudumia asubuhi na jioni na nyakati za chanjo au magonjwa yanapotokea.

Hivyo Neema, kama mtaji na rasilimali zinaruhusu, anaweza kuanza biashara ya mgahawa, iwapo yupo eneo lenye uhitaji na wakati huo pia akawa anafuga kuku. Atahitaji kutumia muda wake vizuri ili aweze kuyaendesha hayo mawili vizuri.

Hivi ndivyo unavyoweza kufanya pale ambapo unakuwa na mawazo mengi ya kibiashara na hujui wazo lipi ambalo uanze nalo. Kipaumbele chako cha kwanza ni kuanza na biashara yoyote utakayoweza kwa mwanzoni na baadaye kukua zaidi. Lakini kama itawezekana, unaweza kuanza biashara ambazo zinaendana. Unahitaji umakini mkubwa kwenye hilo ili usiingie kwenye matatizo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,



TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.