Mafanikio ni kitu ambacho kila mtu anapenda kwenye maisha yake, lakini wachache sana ndiyo wanaishia kuyapata mafanikio. Japokuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kumzuia mwenzake kufanikiwa, bado wengi hawafikii mafanikio. Na hili halitokani na kukosa maarifa ya mafanikio, kwa sababu vitabu vilivyoandikwa kuhusu mafanikio pekee ni vingi. Hadithi za watu waliofanikiwa kwenye maeneo mbalimbali ni nyingi mno. Watu wanajua kila kitu kuhusu mafanikio lakini hawafanikiwi.

Hapa ndipo mwandishi Steve Chandler, alipofikiri kwa kina na kugundua kwamba tatizo siyo maarifa, bali tatizo ni dhamira ya kufanikiwa. Wale waliofanikiwa ni wale ambao wamejitoa kweli kufanikiwa, wamekuwa na dhamira isiyoyumbishwa juu ya mafanikio na hakuna kinachowazuia. 

Katika kitabu chake anatupa maeneo kumi ambayo tunahitaji kujiwekea dhamira ili kuweza kuwa na maisha ya mafanikio.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi ili uweze kuzijua dhamira hizi kumi na kuzifanyia kazi kwenye maisha yako na uweze kufanikiwa.

Dhamira ya kwanza; dhamira ya roho.

1. Mafanikio yanaanza na imani ambayo mtu unakuwa nayo juu ya mafanikio. Kama unaamini unaweza kufanikiwa, inakuwa rahisi kwako kuchukua hatua kuliko kutokuwa na imani hiyo.

2. Ili uweze kujenga vizuri imani yako ya mafanikio, lazima ujue kwamba wewe siyo mwili wako. Una mwili, lakini wewe siyo mwili, wewe ni roho ambayo inaishi kwenye mwili. Roho hii inaweza kufanya makubwa iwapo itaweza kuutumia mwili vizuri.

3. Furaha siyo kitu ambacho unapaswa kukitafuta, ni kitu ambacho tayari kipo ndani yako. Hivyo unapaswa kuwa na furaha wakati wote, na furaha ndiyo itakayokuletea mafanikio.

4. Uwezo mkubwa ambao binadamu tunao ni wa kuigiza, tunaweza kuigiza kitu chochote vizuri sana. Unaweza kuigiza maisha ya mafanikio mpaka pale utakapoyafikia mafanikio yako.

SOMA; Mambo Kumi(10) Muhimu Usiyojua Kuhusu Mafanikio, Na Jinsi Yanavyokurudisha Nyuma.

Dhamira ya pili; dhamira ya akili.

5. Akili yako ni zana muhimu kwa mafanikio yao. Mawazo unayotengeneza kwenye akili yako, yanaweza kukusukuma kufanikiwa au kukuzuia kufanikiwa.

6. Ili kufanikiwa, unahitaji kudhibiti mawazo yako, na usiruhusu mawazo yako yakudhibiti. Kudhibiti mawazo yako, jipe muda wa kutafakari na kuweza kuyaangalia mawazo yako jinsi yanavyopita kwenye akili yako. Chuja yale ambayo siyo mazuri na baki na yaliyo mazuri. 

Tahajudi inaweza kukusaidia sana kudhibiti mawazo yako.

7. Chochote unachofikiria, hakitoki nje na kuingia kwenye mawazo yako, bali mawazo yako ndiyo yanakitengeneza. Watu wengi wamekuwa wanajiambia hawawezi siyo kwa sababu wanajua hawawezi, ila kwa sababu mawazo yao yanawaambia hivyo.

8. Upweke unatokana na mawazo ya ubinafsi, unapojifikiria wewe mwenyewe kuliko wengine, unajikuta kwenye upweke, wa kuona labda kuna kitu unakosa. Kuondokana na upweke, acha kujifikiria wewe mwenyewe na fikiria namna unaweza kuboresha maisha ya wengine. Pia sikiliza wengine, hutajiona mpweke kamwe.

Dhamira ya tatu; dhamira ya matendo.

9. Hakuna mafanikio kama hakuna matendo, unachofanya ndiyo kinachokuletea mafanikio, na siyo kile unachosema au kufikiria.

10. Ili uweze kufanya, ili uweze kuchukua hatua, unahitaji ujasiri, kwa sababu mengi unayotaka kufanya ili kufanikiwa siyo rahisi, na pia kuna kushindwa.

11. Ujasiri siyo kutokuwepo kwa hofu, bali kujua ya kwamba unachotaka kufanya ni muhimu kuliko hofu, na hivyo kufanya licha ya kuwa na hofu. Usisubiri hofu iishe ndiyo ufanye, tafuta kilicho muhimu na fanya.

SOMA; PROSPERITY ON PURPOSE (Mwongozo wa kuishi maisha ya mafanikio makubwa).

12. Muda ndiyo kitu ambacho kinatengeneza maisha yetu, hivyo unapopoteza muda unapoteza maisha yako. Muda tulionao ni mchache, utumie kufanya yale ambayo ni muhimu kwako. Usikazane kufanya kila kitu, bali fanya yale ambayo ni muhimu.

Dhamira ya nne; dhamira ya utajiri.

13. Utajiri ni hali ya kuwa na kinachokutosheleza kuwa na yale maisha ambayo unataka kuwa nayo. Utajiri ni muhimu kwenye maisha yako kwa sababu unakuwezesha kupata yale ambayo ni muhimu.

14. Ili kufikia utajiri, lazima kwanza ujue wapi unapotaka kufika, ni kiasi gani unahitaji ili useme umefikia utajiri. Bila ya kujua unakokwenda, huwezi hata kujua safari unaianzaje.

15. Kitu pekee kitakachokuletea wewe fedha ni kutengeneza tofauti. Kama hakuna tofauti unayotengeneza kwa wengine, hakuna fedha unayoweza kupata. Wanaotengeneza tofauti, wanaoongeza thamani kwa wengine, ndiyo wanaotajirika.

16. Chochote unachorudia kufanya, ndiyo unachokuwa bora sana. Huhitaji kuanza na kitu cha tofauti sana, bali unahitaji kuanza na chochote na kisha kurudia kufanya mara nyingi, unakuwa bora kadiri unavyorudia kufanya.

Dhamira ya tano; dhamira kwa marafiki.

17. Marafiki ni watu muhimu sana kwenye maisha yako, hawa ni watu wanaojua mapungufu yako lakini bado wanakukubali ulivyo, bila hata ya kulazimishwa. Marafiki wanakuwezesha kupiga hatua kubwa kwenye mafanikio.

18. Ili kupata marafiki wazuri, anza wewe mwenyewe kwa kuwa rafiki mzuri. Marafiki hawatokei tu kama mvua, marafiki wanatengenezwa. Kadiri unavyojali kuhusu mambo ya wengine, ndivyo wanavyojali kuhusu mambo yako na ndivyo urafiki unavyokua baina yenu.

19. Ili urafiki uweze kudumu, lazima kuwe na maslahi ya pamoja baina ya marafiki. Uwepo wa maslahi haya unawafanya muweze kwenda pamoja.

20. Ukuaji wa urafiki pia unachochewa na hali ya kujisikia salama baina ya marafiki. Iwapo kutakuwa na ushindani baina ya marafiki, au mwingiliano wa maslahi, lazima urafiki huo utavunjika.

SOMA; Kama Unafikiri Mafanikio Yako Hivi Tu, Tayari Umeshapotea.

Dhamira ya sita; dhamira ya dhamira.

21. Unahitaji kuweka dhamira ya kuwa na dhamira, na dhamira ni maamuzi unayofanya, ambayo utayasimamia bila ya kujali nini kinatokea. Unajitoa kweli kwamba hakuna kitakachokuzuia katika maamuzi uliyofanya.

22. Jua wazi ni dhamira gani umejiwekea kwenye maisha yako, ni kitu gani ambacho lazima ufanye na lazima ufikie kwa juhudi zako zote hata kama utakutana na vikwazo. Hii itakusaidia kufika kule unakotaka kufika.

23. Kuweka dhamira haimaanishi kwamba mambo yatanyooka kama unavyofikiria, badala yake utakutana na vikwazo ambavyo vitakurudisha nyuma. Kuwa tayari kurudishwa nyuma, lakini usikubali kubaki hapo, weka juhudi kuhakikisha unafika pale ulipopanga kufika.

24. Acha kujidanganya kwamba mambo yatakwenda vizuri tu, kama ipo ipo tu. Mafanikio hayatokei kama ajali, mafanikio yanatengenezwa. Tengeneza mafanikio yako ili kuhakikisha unapata kile unachotaka.
Dhamira ya saba; dhamira kwa mwenda wako.

25. Usipoteze muda mwingi kutafuta mwenza aliyekamilika, badala yake jitengeneze wewe kuwa mwenza bora kwa mwenzako. Hakuna mtu aliyekamilika, bali watu wanaweza kuishi pamoja kama watachukuliana kwa mapungufu yao na kushirikiana kwa mazuri yao.

26. Njia ya kuepuka migogoro kwenye mahusiano ni kuepuka kuhukumu wengine. Unapohukumu, kabla hata hujawa na uhakika wa jambo, unajenga migogoro zaidi kwenye mahusiano hayo.

27. Kila mtu anapenda kukubaliwa kwa kile kizuri anachofanya, tumia tabia hii kwenye mahusiano yako ili kuyaboresha zaidi. Mkubali na kumsifia mwenzako kwa yale mazuri anayofanya, atafurahi na kufanya zaidi.

28. Siyo lazima uwe sahihi mara zote, wakati mwingine unahitaji kuacha kuwa sahihi ili tu muweze kuelewana na mwenzako. Furaha siyo kuwa sahihi wakati wote, bali kuweza kwenda vizuri na wengine wakati wote.
Dhamira ya nane; dhamira kwenye kazi.

29. Kazi yako ina mchango mkubwa kwenye mafanikio yako, hivyo unahitaji kuipa kipaumbele. Kama kwa sasa kazi yako haikupi kile unachotaka, unahitaji kutaka zaidi ya unavyotaka sasa, na kujitoa kufanya zaidi ya unavyofanya sasa.

30. Tatizo kubwa linalowakwamisha wengi, ni kutaka kujua JINSI YA KUFANYA kabla ya kujua KAMA KWELI WANATAKA KUFANYA. Vitabu vingi vimeandikwa jinsi ya kufanya kila unachotaka kufanya, lakini hakuna vilivyoandikwa JINSI YA KUTAKA KUFANYA UNACHOTAKA KUFANYA. Unahitaji kutaka kwanza kabla hujajua namna ya kufanya.

31. Siyo lazima uanze na kazi bora, unaweza kuanza na kazi za kawaida, na baadaye kadiri unavyokwenda ukaendelea kupiga hatua. Wengi unaowaona wamefanikiwa kwenye kazi na biashara zao, hawakuanzia hapo walipo sasa.

32. Kila mtu kuna kitu anauza, na unauza pale ambapo mtu anashawishika kuna thamani kwenye kile unachotaka anunue kutoka kwako. Hivyo chochote unachofanya, waoneshe wengine thamani kubwa watakayopata kwa kufanya kazi na wewe.
Dhamira ya tisa; dhamira ya mwili.

33. Mwili wako chombo kinachokupeleka popote unapotaka kwenda. Kama tulivyoona, wewe ni roho ambayo ipo ndani ya mwili. Hivyo ili roho hii iweze kufanya makubwa, inahitaji mwili ambao upo vizuri. Kama unavyotaka kusafiri unachagua gari zuri na imara, unahitaji mwili mzuri na imara.

34. Unahitaji kula vyakula bora kwa afya yako, na kwa kiasi cha kutosha. Kula kwa namna ya asili, na kamwe hutakuwa na uzito uliopitiliza.

35. Chakula unachokula pia kinahitaji kutumiwa, la sivyo uzito wa mwili utaongezeka. Unahitaji kufanya mazoezi ya mwili ili kutumia chakula na kutengeneza nguvu ambayo mwili itatumia kwa ajili ya kufanya yale muhimu kwa mafanikio yako.

36. Mwili wako unahitaji hewa ya kutosha kwa ajili ya kuunguza chakula na kupata nguvu. Hivyo unahitaji kuwa na upumuaji mzuri kuhakikisha mwili unapata nguvu za kutosha.
Dhamira ya kumi; dhamira ya muziki ulipo ndani yako.

37. Kila mtu ana muziki ambao upo ndani yake, kila mtu ana kipaji cha kipekee, ana uwezo mkubwa sana ambao anaweza kufanya makubwa na ya tofauti. Wengi wanakufa wakiwa hawajacheza mziki huu kwa sababu dunia inawahadaa wasipate muda wa kutoa muziki huu mzuri.

38. Hata kama kipaji chako ni tofauti na kazi au biashara unayofanya sasa, usikiache kife, bali kifanyie kazi. Tenga muda wa kufanyia kazi kipaji chako, na kifanye kwa hatua ndogo kila siku. Baadaye unaweza kuacha kazi yako au kustaafu na kufanya kipaji chako kuwa kazi yako ya kudumu. Na uzuri wa kufanya kipaji chako kuwa kazi yako, hutahitaji kustaafu kamwe, kwa sababu unafanya unachopenda na siyo kufanya kazi.

39. Usiogope kwamba hutakuwa vizuri kwenye kipaji ulichonacho. Unachohitaji ni kuanza kufanya na kurudia kufanya. Kadiri unavyofanya, ndivyo unavyokuwa bora.

40. Muziki uliopo ndani yako ni njia ya nafsi yako kujionesha. Unapoficha muziki huu unaificha nafsi yako na hivyo kuona kama kuna maisha ambayo hukupata nafasi ya kuyaishi. Anza kuyaishi sasa kwa kufanyia kazi vipaji vyako.

Dhamira hizi kumi za mafanikio siyo kitu cha kufanya kimoja halafu kwenda kingine, bali ni vitu ambavyo unahitaji kufanya kwa pamoja vyote. Unahitaji kutengeneza maisha ambayo mambo haya yote kumi ni sehemu ya maisha hayo, na unayafanya kila siku ya maisha yako. Hakuna namna mafanikio yakakukwepa kama kweli utajiwekea na kuishi dhamira hizi kumi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita