Rafiki yangu mpendwa,

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba maisha ni magumu kwa kila mtu, lakini maisha ni magumu zaidi ukiwa mpumbavu.

Na ukiyaangalia maisha, kauli hiyo ina ukweli usiopingika. Pamoja na ugumu wa maisha, wapo watu ambao wanachagua kuyafanya maisha yawe magumu zaidi ya yalivyo. Na ukiangalia kwa undani kwa nini watu wachague kuyafanya maisha yawe magumu zaidi ya yalivyo, ndipo ukweli wa hiyo kauli unakuja wazi zaidi.

Kwa mfano, hebu chukulia mtu ambaye kipato chake ni kidogo na hawezi kumudu mahitaji yake ya msingi kwenye maisha. Mtu huyu anapaswa kuchukua hatua gani ili kuondokana na hali hiyo? Mtu yeyote ambaye akili zake zipo sawa, anajua hatua ya kuchukua ni kuongeza kipato. Kwa sababu kama kipato hakitoshelezi, unahitaji kuongeza kipato. Hilo halihitaji hata uwe na cheti cha darasa la saba kujua.

Lakini sasa nenda kwenye uhalisia, nenda kaangalie watu wanafanya nini hasa pale ambapo kipato chao kinakuwa kidogo na hakimudu mahitaji yao ya msingi. Wanakopa. Na wanakopa siyo kwa sababu ni suluhisho la muda mfupi, kwamba labda wanahitaji kiasi fulani cha fedha kama dharura na huku wakiendelea kuongeza kipato chao. Bali ukopaji unakuwa tabia. Mtu anapokea kipato chake kidogo anakitumia kinaisha, anaenda kukopa, akipata kipato kingine anarudisha mkopo halafu anakopa tena na maisha yanaenda hivyo.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Kama hivi ndivyo umekuwa unaendesha maisha yako kwa upande wa fedha na hata maeneo mengine, nafikiri ujumbe umeshaupata, umeshaelewa nini nilikuwa nakuambia hapo juu.

Sasa rafiki yangu, leo nakwenda kukushirikisha mtazamo ambao utayafanya maisha yako yasiwe magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa. Ukiiangalia dunia na maisha yako kwa namna ninayokwenda kukushirikisha leo, utaona utofauti mkubwa sana na kwa kila tatizo linalokukabili, utaona suluhisho lake likiwa mbele yako.

Mtazamo muhimu wa kuendesha nao maisha yako ni huu; KILA KITU UNACHOFANYA KWENYE MAISHA NI MAUZO, NA KILA UNACHOTAKA NI KAMISHENI.

Hii ina maana kwamba, kila mtu kwenye haya maisha ni muuzaji, kila mtu kuna kitu ambacho anauza. Na ili upate chochote kile unachotaka, lazima uuze.

Ukishajua kwamba wewe ni muuzaji na ukishajua unauza nini, halafu ukajua njia bora za kuuza kile unachouza, hutakosa kamisheni ambayo unataka kupata.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Ten Commitments To Your Success (Dhamira Kumi Kwa Mafanikio Yako.)

Hata kama umeajiriwa na unajiambia wewe siyo mtu wa mauzo, unauza kila siku. Kwanza ili kupata ajira hiyo umeuza elimu yako, taaluma yako na hata uzoefu wako. Ili uendelee kuwa kwenye ajira yako kila siku unamuuzia mwajiri wako muda wako na utaalamu wako. Na ili kazi yako iwe na maana, lazima utatua matatizo ambayo watu wanayo.

Kila mtu anauza, na kila kitu kwenye maisha kinapatikana kama kamisheni, baada ya kukamilisha mauzo.

Unapokuwa umekwama kwenye maisha yako kumbuka kitu kimoja muhimu sana, hujauza. Kama ukiuza, kamwe huwezi kukwama kwenye maisha. Unakwama pale ambapo huuzi, pale ambapo huuzi vya kutosha au huna wateja sahihi wa kuwauzia.

Kwa mfano kama upo kwenye kazi ambayo haikulipi kama unavyotaka kulipwa, shida siyo yule aliyekuajiri kukulipa kidogo, shida ni wewe muuzaji, hujamuuzia mwajiri wako thamani ambayo atalazimika kukulipa kama unavyotaka. Kama utaongeza sana thamani ya kile unachofanya, kwa namna ambayo hakuna mwingine anaweza kufanya, na mwajiri wako akajua hilo, unaweza kumfuata na kumwambia nataka kulipwa zaidi na hatosita kukulipa. Kama hataweza, basi unaweza kupeleka thamani hiyo kubwa kwa mwajiri mwingine na akakulipa vizuri utakavyo.

Kadhalika kwa wale waliojiajiri na wanaofanya biashara, kile unacholipwa ni matokeo ya thamani unayotoa kwa wengine. Ukitoa thamani zaidi utalipwa zaidi.

Kumbuka, maisha ni mauzo na tunachotaka ni kamisheni. Kupata kamisheni zaidi lazima uuze zaidi. Hakuna mtu mwenye wajibu wa kuuza kwa ajili yako, ni wewe mwenyewe unayepaswa kuuza, ni wewe mwenyewe unayepaswa kutoa thamani kubwa ili kuweza kupata kamisheni kubwa.

Endesha maisha yako kwa mtazamo huu na mara zote utaweza kuvuka changamoto unazokutana nazo. Kwa sababu suluhisho la changamoto yoyote kwenye maisha ni kuuza. Hata kama umekosana na mtu, mmekosana kwa sababu mmeshindwa kuuziana hoja fulani mlizokuwa nazo. Kama kila mtu akiweza kumuuzia mwenzake hoja zake vizuri, basi mtaelewana sana.

Kila kitu tunachofanya kwenye maisha ni mauzo na kila tunachotaka ni kamisheni. Uza kila wakati na maisha hayatakuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji