Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Nafasi hii tuliyopata leo ni ya kipekee sana, twende tukaitumie vizuri ili tuweze kufanya makubwa kuelekea kwenye ndoto zetu.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MAISHA HAYATAKUWA RAHISI…
Watu huwa wanajidanganya na kujipa matumaini hewa kwamba wakishafika hatua fulani tu, basi ugumu wa maisha utaondoka na yatakuwa rahisi sana.
Labda ni wakati mtu anasoma, na kujiambia akishamaliza kusoma, na kuanza kufanya kazi, maisha yatakuwa rahisi sana,
Au mtu anatafuta kazi hapati, matumaini yake yote yanakuwa kwamba akipata kazi basi maisha yatanyooka sana.
Au ni biashara mtu anafikiria, kwamba akishaweza kuingia kwenye biashara ya ndoto zake, mambo yatakuwa rahisi sana.
Watu huwa na matumaini haya, mpaka pale wanapoingia kwenye kile wanachosubiri kwa hamu, na ndipo wanapokutana na ukweli kama ulivyo, kwamba mambo siyo rahisi.
Wanapoingia kwenye kazi wanakutana na changamoto za kazi, kuanzia kazi yenyewe, mwajiri na hata wanaomzunguka, hapo bado matarajio ya jamii ambayo inafikiri kwa kuwa mtu ana kazi basi ameshatoka kimaisha.
Au anapoingia kwenye biashara, ndipo anapokutana na changamoto za kibiashara, ambazo hakuwahi kuzifikiria hapo mwanzo.
Hivyo, rafiki, chochote unachofikiria sasa kwamba ukianza kukifanya basi maisha yako yatakiwa rahisi, UNAJIDANGANYA, kila kitu kinakuja na changamoto zake. Hata kama unasubiri kwa haku kiasi gani, utakutana na magumu mengi tu.
Na hata kama kuna changamoto unayopitia sasa, usijidanganye kwamba ukishaimaliza hii basi maisha yamenyooka, hiyo ni hatua tu, ukimaliza changamoto hiyo ndogo, unafungua milango kwa changamoto kubwa zaidi ya unayopitia sasa.
Kwa kifupi ni kwamba, hakuna wakati maisha yatakuwa rahisi tu, hakuna chsngamoto wala matatizo. Hivyo jukumu letu siyo kuangalia tunakimbia vipi matatizo na changamoto, bali tunazitatuaje ili tuwe bora zaidi na tusishindwe na changamoto zaidi zinazokuja.
Muhimu zaidi, tuache kujidanganya kwamba tukivuka tulipo sasa, basi maisha ni mteremko, vuka ulipo sasa na utakutana na mlima au bonde jingine la kuvuka. Hayo ndiyo maisha, lazima tuende nayo hivyo.
Nikutakie kila la kheri rafiki, na hii ni tafakari ya mwisho mimi kukuandikia kwa kipindi hichi, kwa vyovyote vile, USIACHE KUTAFAKARI KILA SIKU KABLA YA KUIANZA SIKU YAKO.
Na hakuna sheria yoyote, wewe tafakari chochote unachojisikia kwa siku hiyo, muhimu uondoke tu na hatua za kuchukua.
Tutaendelea kuwa pamoja kwenye mambo mengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.