Biashara ni sawa na kiumbe hai, na kama viumbe hai vyote vilivyo, huzaliwa na kufa, na ili kukua, basi kiumbe hai lazima kipate matunzo yote muhimu. Biashara inahitaji matunzo muhimu sana ili iweze kukua, na kama itapata matunzo yote muhimu kwa wakati, basi inaweza kuvunja sheria moja ya viumbe hai, haitakufa, bali itadumu kwa muda mrefu.

IMG-20170228-WA0006

Moja ya mahitaji muhimu sana ya viumbe hai, ni mzunguko wa damu ndani ya miili yao. Hii ni kwa sababu damu inabeba virutubisho kulisha mwili, na pia inabeba uchafu na kuutoa nje ya mwili. Iwapo mwili utakosa damu, utakufa, kwa sababu utakosa virutubisho, kinga na hata uchafu utakuwa mwingi.

Je unaijua damu ya biashara yako ni nini? Ambayo inaleta virutubisho kwenye biashara? Hili ni eneo muhimu mno ambalo lazima ulipe kipaumbele cha kipekee ili uweze kufanikiwa kwenye biashara.

Damu ya biashara ni mzunguko wa fedha, fedha inapozunguka kwenye biashara, inalisha biashara virutubisho muhimu, kama mahitaji ya msingi, gharama za msingi na hatimaye ukuaji wa biashara. Lakini mzunguko wa fedha unaposuasua kuzunguka, basi biashara nayo huanza kufa.

SOMA; Kama Unataka Fedha….

Ili kuhakikisha mzunguko wa fedha kwenye biashara unakuwa imara, hii hapa ni misingi mitatu muhimu sana ya kuzingatia kwenye biashara yako linapokuja swala la fedha.

Msingi wa kwanza; jua fedha inapotoka, na weka juhudi zako pale.

Sehemu ya kwanza muhimu ya kuangalia na kufanyia kazi, ni wapi fedha inayokuja kwenye biashara yako inatoka. Lazima tujue chanzo, ili tuweze kukilinda, kiendelee kuwepo zaidi na kuzalisha zaidi. Chanzo cha fedha kwenye biashara yoyote ni hiki; MAUZO. Mauzo ndiyo yanaleta fedha kwenye biashara, kama biashara haiuzi, hakuna namna inaweza kudumu kwa muda mrefu.

Hivyo basi kwenye biashara yako, jua mauzo ni yapi, unauza nini na kwenye kila unachouza, ni kiasi gani cha fedha kinachoingia kwenye biashara yako. Kununua tu na kuuza hakukufanyi wewe kuwa mfanyabiashara, unahitaji kwenda ndani zaidi, kujua unauza nini, kwenye kila unachouza unapata nini na pia unamuuzia nani. Hii ni muhimu sana, kwa sababu mauzo yanaposhuka, jua biashara inashuka.

Ili kwenda sawa, piga hesabu zako za kibiashara vizuri, na ujue ili biashara iweze kwenda vizuri, unahitaji kuuza kiasi gani kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka. Usifanye biashara tu kwa mazoea kwamba nikifungua nauza, bidhaa zikiisha nitaongeza nyingine. Ukifanya hivyo ndiyo unashangaa biashara haina bidhaa na fedha pia huzioni. Mwishowe utafikiri kuna watu wamekuibia au kukudhulumu.

Jua namba za biashara yako, jua unahitaji kuuza kiasi gani na wanaonunua ni watu gani. Hii itakuwezesha kujua unawezaje kuongeza mauzo zaidi.

Msingi wa pili; jua fedha inapotoa kwenye biashara yako inaenda wapi.

Yupo rafiki yangu ambaye ana duka nyumbani kwake, karibu kila mwaka huwa analifungua kwa kulijaza vitu, lakini baada ya muda analifunga. Ameshafanya hivyo mara kadhaa, tulishashauriana njia bora zaidi ya kuondokana na hali hiyo lakini naona amekuwa hafuati njia hiyo. Sasa hii ni kwa biashara ndogo, japo kubwa pia zina tatizo hili moja; hawajui fedha zinaenda wapi. Hapa ndipo shida kubwa kwenye kila aina ya biashara inapoanzia, unauza kweli, lakini fedha zinaenda wapi? Zinapotelea wapi?

SOMA; Haijalishi Hali Ya Uchumi Ikoje, Fursa Za Kutengeneza Fedha Bado Ni Nyingi…

Kwa utafiti mkubwa ambao naufanya kupitia hawa wanaosema fedha hawazioni, siyo kwamba wameibiwa au wamedhulumiwa, ila tu wanazitumia bila ya mipangilio, na hili linaleta shida kubwa kwenye biashara. Matumizi ya biashara na matumizi binafsi yanachanganywa kwenye biashara moja, inakuwa changamoto kujua fedha halisi ya biashara inaenda wapi.

Jambo la kwanza kabisa, jua biashara siyo wewe, yaani wewe na biashara yako ni watu wawili tofauti kabisa, mna uhusiano tu wa karibu, wewe ni wewe na biashara ni biashara. Hivyo mzunguko wowote wa fedha baina yako na biashara yako, lazima uwe kwenye utaratibu mzuri wa kumbukumbu.

Hivyo basi fanya yafuatayo;

  1. Jua matumizi ya msingi kabisa ya biashara yako, na hayo yape kipaumbele. Yale mengine ambayo siyo muhimu sana, yanaweza kusubiri kama biashara bado ni changa au haitengenezi faida nzuri.
  2. Jua matumizi yako binafsi na jua kipato gani kinahudumia matumizi hayo. Kama unaitegemea biashara yako moja kwa moja kwenye matumizi yako, unahitaji kuwa makini zaidi, usitoe tu fedha au bidhaa pale unapojisikia, badala yake weka utaratibu wa kujilipa, ikiwa ni kwa siku, wiki au mwezi, na chukua kiasi kile tu ulichopanga, usizidishe. Unahitaji nidhamu sana kwenye hili, la sivyo utarudi nyuma.
  3. Matumizi yote ambayo yanategemea fedha kwenye biashara yako, NI LAZIMA yawe madogo kuliko faida unayopata kwenye biashara yako. Kama matumizi ni makubwa kuliko faida, ongeza faidia kwa kuuza zaidi na pia punguza matumizi yasiyo ya msingi.

Msingi wa tatu; unawekeza nini kwenye biashara yako?

Biashara yako ina miaka mingapi kwa namna ilivyo? Au kama biashara yako ni mpya, angalia wale waliokutangulia kwenye biashara kwa muda mrefu, wamepiga hatua gani? Utakachoona kinaweza kukukatisha tamaa, watu wapo pale pale, miaka nenda rudi. Hii inasababishwa na biashara kuendeshwa bila mpango wowote wa ukuaji, kinachopatikana kinatumika na mzunguko unaendelea. Ni nunua, uza, pata faida, tumia yote, nunua tena.

Unahitaji kuwa na mpango wa ukuaji wa biashara yako, na mpango huu lazima upate nguvu ya fedha katika kukua. Mpango huu unaweza kuwa na bidhaa au huduma zaidi, pia kuwa na matawi zaidi ya biashara yako. Hivyo sehemu ya faida unayopata kwenye biashara yako, lazima irudi kujenga na kukuza zaidi biashara yako. Lazima uwekeze kwenye biashara yako mwenyewe, ili faida iendelee kuwa kubwa zaidi na mafanikio yawe makubwa zaidi.

Kwa mwanzoni mwa biashara, yafaa sana faida isitumike kabisa, badala yake irudi kwenye biashara, lakini kama hilo haliwezekani, basi weka juhudi zaidi na nusu ya faida irudi kwenye biashara.

Hiyo ndiyo misingi mitatu muhimu ya fedha kwenye biashara, ambayo unahitaji kuifuata iwapo unataka kuwa na biashara yenye mafanikio. Kama ambavyo umeona, unahitaji umakini mkubwa katika kujenga misingi hii na muhimu zaidi, unahitaji nidhamu ya hali ya juu. Misingi hii ipo wazi lakini wengi hawawezi kuitumia, kwa kukosa nidhamu. Wewe mwanamafanikio nina imani unajijengea nidhamu kila siku na hivyo utaweza kuifuata misingi hii vizuri.

Kama una swali au maoni kuhusiana na hili, karibu tujadiliane hapo chini kwenye maoni.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog