Kijana mmoja ambaye alikuwa ndiyo ameajiriwa kama miaka miwili hivi, tukiwa kwenye maongezi aliniambia tangu ameajiriwa hajawahi kuchukua mkopo benki kwa kutumia mshahara wake. Nikamwambia hizo ni dalili nzuri, ni vyema akaendelea hivyo. Lakini yeye alikuwa akichukulia hilo kama siyo sawa, kwa sababu wenzake wote anaofanya nao kazi, wana mikopo kwenye mabenki. Na pia walikuwa wanamwambia yeye asipochukua mkopo, lolote linaweza kutokea na akawa hajanufaika na kazi yake.

IMG-20170314-WA0002

Hapo nilishangaa namna ambavyo watu wanaweza kutumia sababu za hovyo kabisa kuingia kwenye madeni ya kifedha. Na kikubwa zaidi ninachojifunza kila siku, watu wengi wanaingia kwenye madeni kwa sababu ambazo hata wao wenyewe hawazijui.

Madeni ya kifedha, hasa ambayo hayakuzalishii wewe, ni madeni mabaya kwenye maisha yako, ni sawa na kuchagua wewe mwenyewe kupoteza fedha zako kupitia riba unayolipa unapolipa madeni. Kwa mfano kama umekopa shilingi milioni moja, na unapaswa urudishe milioni moja na laki moja, wewe ukaenda kutumia hiyo milioni moja kununua vyakula, unafikiri wakati unalipa hilo deni ile laki moja ya ziada inatoka wapi? Ni kwenye fedha zako, kwa sababu deni ulilochukua, halikukuzalishia chochote.

Changamoto nyingine kubwa ya madeni ni kuwa kama tabia. Yaani huwa inaanza kidogo kidogo, baadaye mtu anajikuta ameshatumbukia kwenye madeni kabisa, hawezi tena kutoka. Inakuwa ni tabia kwake, akili yake yote ni kwenye kukopa. Hata anapokutana na tatizo dogo, hafikirii kitu kingine bali atakopa wapi.

SOMA; Weka Macho Yako Fedha Zako Zilipo…

Mafanikio na madeni mabaya haviwezi kwenda pamoja. Hivyo ni jukumu lako kama mwanamafanikio kuhakikisha huingii kwenye madeni mabaya, na kama ulishaingia basi uweze kuondoka mara moja.

Leo tutakwenda kujifunza kuhusu tabia moja inayopelekea wengi kuingia kwenye madeni, na tukishaijua tabia hii, itatuwezesha kuiepuka na kuepuka madeni moja kwa moja.

Kabla ya kuangalia tabia hii, hebu kwanza tuangalie madeni kwa undani. Kwa nini mtu anakopa? Na kumbuka leo tunajadili kuhusu madeni mabaya, yaani madeni ambayo hayazalishi. Hatuongelei mikopo ya kibiashara, huo utakuwa mjadala wa siku nyingine.

Mtu anakopa, pale anapotaka kupata kitu ambacho hawezi kukimudu. Yaani mtu anataka kununua kitu, lakini uwezo wa kukinunua hana, na anajua kabisa hana uwezo huo kwa wakati huo, lakini anataka akipate, NI LAZIMA NIKIPATE SASA. Kwa msisitizo huo, anakaribishwa kwenye dunia ya madeni, ambapo unaweza kupata chochote unachotaka, kwa muda wowote hata kama huna fedha, ila baadaye utakuja kulipa na kuadhibiwa kwa kitendo chako hicho.

Unaanza kupata picha sasa ya tabia inayopelekea kwenye madeni?

Tabia kubwa inayowapelekea watu kuingia kwenye madeni ni kukosa subira, kutaka kitu na kukitaka muda huo. Kama ambavyo watoto wadogo walivyo na tabia ya kutaka kitu kwa wakati wanataka wao. Akikosa atalia mpaka akipate. Hivyo ndivyo watu wazima wanavyokuwa kwenye madeni. Ipo nguo nzuri ameiona, na anaitaka sasa, ila hana fedha, anakopa ili akipata fedha alipe. Sasa hebu niambie hapo, kwa nini usisubiri mpaka upate hiyo fedha ndiyo ununue hicho ulichotaka? Je ni kwamba ukiacha kununua sasa utakufa?

Hapana, ni vitu vichache sana ambavyo ukivikosa utakufa, na hivyo wala huhitaji kukopa ili kuvipata. Ukifanya tathmini ya watu wengi wenye madeni, sehemu kubwa ya madeni yanayowatesa siyo ya chakula, bali ya vitu ambavyo wangeweza kusubiri na kununua kwa fedha taslimu. Iwe ni nyumba ya kuishi, gari ya kutembelea, mavazi na vitu vingine ambavyo haviingizi fedha, watu wangeweza kabisa kusubiri mpaka pale wanapopata fedha na kununua bila ya shida.

SOMA; Zipo Fedha Za Kutosha Kila Mtu Kuwa Bilionea…

Lakini utaniambia ukisubiri mpaka upate fedha, matumizi yanakuwa makubwa zaidi. Au huwezi kukusanya fedha mpaka ifike kununua gari au kujenga nyumba ya kuishi. Na hivyo bora kukopa ambayo unalipa kidogo kidogo. Na kujiaminisha kwamba hilo siyo deni baya, kwa sababu usingeweza kukusanya mwenyewe na kufanya maendeleo yako. Mimi hapo nitakuambia sasa una matatizo mawili, tatizo la kwanza ni la kukosa subira, na tatizo la pili ni kukosa nidhamu binafsi na nidhamu ya fedha.

Kwa sababu kama unakopa kwa sababu huwezi kukusanya mwenyewe, kumbuka unalipa kwa kipato kile kile ambacho wewe mwenyewe ungeweza kukipangilia vizuri ungeepuka riba ambazo unakatwa kwenye mikopo hiyo. Hivyo unakubali tatizo lako la kukosa nidhamu binafsi, likuletee adhabu ya makato kwenye riba ya mikopo ambayo umechukua.

Mwingine atasema kinachopelekea mtu kuingia kwenye madeni ni pale inapotokea dharura mtu akiwa hana fedha. Kwamba huna fedha na umepata tatizo, kama la ugonjwa, au ajali, au kupoteza kitu muhimu kwako. Hapo huna namna ni lazima ukope. Na hapo nitakubaliana naye kwamba matatizo hakuna anayejua yatatokea wakati gani, lakini tunajua matatizo huwa yanatokea. Hivyo ni wajibu wetu kujiandaa kwenye matatizo kama hayo. Unahitaji kuwa na fungu la dharura ambalo utalitumia kwenye nyakati kama hizo. Huhitaji kuwa huna fungu lolote la dharura, hata kama hujapata dharura kwa muda mrefu. Ndiyo maana inaitwa dharura, kwa sababu hakuna anayejua inatokea wakati gani, hivyo maandalizi ni muhimu.

Mwisho kabisa, nikuambie rafiki, weka juhudi kwenye kuongeza kipato chako kama unaona kila wakati matumizi yako yanakuwa makubwa kuliko kipato chako. Ukishajiona upo kwenye huo mstari, pambana zaidi, fanya kazi zaidi, jitoe zaidi kuhakikisha kipato chako kinaongezeka. Nakuambia hivyo kwa sababu, kukopa ili kufidia upungufu wa kipato chako siyo suluhisho la matatizo yako ya kifedha, bali ni kupooza kwa muda mdogo tu, na baadaye unatengeneza matatizo makubwa.

Hivyo kama kipo kitu ambacho unakihitaji kweli, na fedha huna, kitumie kama msukumo wa wewe kuhakikisha unapata fedha ya kukipata. Mfano unataka kununua gari, fedha huna, badala ya kujiuliza utakopa wapi fedha za kununua gari, jiulize unawezaje kuongeza kipato chako ili uweze kununua gari. Angalia ni kiasi gani unahitaji kwa gari hiyo, na weka mipango ya njia mpya za kipato utakazotumia kuhakikisha unapata fedha hiyo. Jipe muda na pambana kuhakikisha unapata hiyo fedha na kununua kwa fedha zako.

Nihitimishe kwa kuweka vizuri yote tuliyojadili hapa.

  1. Kukopa kunatokana na tabia ya kukosa subira, unataka kitu na unakitaka sasa, bila ya kujali una fedha au la.
  2. Pamoja na kukosa subira, kukosa nidhamu binafsi na nidhamu ya fedha kunachangia wengi kuingia kwenye madeni. Wangeweza kukusanya fedha zao wenyewe, wasingeingia kwenye madeni.
  3. Unahitaji kuwa na mfuko wa dharura ambapo unaweza fedha ambazo utazitumia wakati wa dharura. Hakuna ajuaye dharura inakuja wakati gani na itauja kiasi gani, hivyo ni vyema mfuko wako ukawa vizuri wakati wote. Hii itakuzuia kuingia kwenye madeni.
  4. Unaweza kutumia kila unachotaka kuongeza kipato chako zaidi, badala ya kukimbilia kukopa. Kama kuna kitu unataka, badala ya kufikiria kukopa, fikiria kuongeza kipato chako ili kukipata.
  5. Njia pekee ya kumaliza changamoto zako za kifedha, hasa pale matumizi yanapozidi mapato na hivyo kulazimika kukopa, ni kuongeza kipato chako. Juhudi zako ziwe kuongeza kipato chako kila wakati, hii itakuondoa kwenye mzigo wa madeni.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog