Waswahili wanasema, mipango siyo matumizi. Wakiwa na maana kwamba unaweza kupanga sana, lakini inapofika kwenye utekeleaji, mambo yanaweza kwenda tofauti na ulivyotegemea. Na kwa uzoefu wangu na wengine ambao nimekuwa nawaangalia, mara nyingi sana mambo huenda tofauti kabisa na mategemeo ambayo watu wanakuwa nayo.

IMG-20170322-WA0009

Inapofika hali kama hii, wengi hukata tamaa na kuona haiwezekani tena. Wengi huanza kujuta na kukumbuka nafasi walizoacha huko nyuma na kuchukua hii ambayo walitegemea iwe nzuri. Lakini mambo yanakuwa hayajaenda walivyotegemea.

Ni pale mtu anapoacha ajira na kwenda kujiajiri, akitegemea anakwenda kupata uhuru wa kipato na kujikuta kipato kinakuwa kigumu zaidi kuliko hata alivyokuwa kwenye ajira. Na kujiuliza kwa nini alifanya makosa makubwa hivyo, ili hali wakati akiamua alikuwa timamu kabisa. Ipo pia kwa wale wanaochagua aina fulani ya biashara na kuacha nyingine, au kuchagua aina fulani ya maisha na kukataa mengine ambayo walikuwa nayo. Kwa jambo lolote unalofanya maamuzi, matokeo yanaweza yasiwe kama unavyotaka, na hapo ndipo wengi wanapokubali kuanguka.

Hapa nakwenda kukushirikisha mambo matano muhimu ya kufanya pale unapokwama, ili uweze kujikwamua na usiwe mwisho wa safari yako. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia, kama bado unapumua, basi mapambano bado yanaendelea.

SOMA; Ni Matatizo Gani Unayotatua?

  1. Kuwa mkweli wa kile kinachoendelea.

Mara nyingi tunapokutana na vikwazo, huwa tunaingiwa na hisia na kushindwa kufikiri kwa usahihi. Wakati mwingine huwa tunatafuta nani kasababisha mpaka tumefika pale tulipofika. Na kwa namna jamii zetu zilivyo, nakuhakikishia hutakosa wa kumlaumu, hata kama hakuna kabisa, serikali lazima itakuwa imehusika kwa namna moja au nyingine. Wazazi pia nao huwa hawakosekani kwenye lawama, hata kwa jambo walilofanya wakati mtu yupo utotoni.

Sasa wewe usikubali kufikia hali hii, badala yake ona ukweli wa kinachoendelea. Kwamba umekwama kama watu wengine wengi wanavyokwama. Pia kukwama kwako siyo mwisho wa dunia, maisha bado yanaendelea na kesho ipo. Kuna mengi pia ambayo umejifunza kwa kukwama huko, yote hayo yachukue ili yakusaidie kusonga mbele.

  1. Dhibiti hisia zako.

Hasira, chuki, wivu na hata hofu ni hisia ambazo huambatana na vikwazo unavyokutana navyo.

Unakasirika kwa nini mambo yameenda kama yalivyoenda.

Unawachukia watu ambao unafikiri wamekufikisha pale, hata kama hawahusiki moja kwa moja.

Unakuwa na wivu kwa wale ambao wameanza kama wewe lakini wao wamefanikiwa na hawajakutana na vikwazo kama wewe.

Na unakuwa na hofu kwamba hutakuja kuweza tena, huo ndiyo mwisho wako na hakuna namna.

Ninachokuambia hizo zote ni hisia, ondokana nazo ili akili yako iweze kufikiri sawasawa. Akili ikisongwa na hisia, uwezo wa kufikiri unapungua.

  1. Chagua kuona uzuri kwenye kila jambo.

Siri, jambo lolote linalokutokea kwenye maisha yako, kuna uzuri umejificha ndani yake, hata kama ni jambo baya kiasi gani kwako. Wewe angalia tu, hata kama umepata ajali, jaribu kuangalia kwa undani, utaona kipo kitu cha manufaa kwenye ajali hiyo. Labda ni kujifunza kuhusu thamani ya maisha yako, labda ni kujifunza kuhusu kuwa makini zaidi. Wewe angalia na utaona uzuri, halafu utumie. Kama nilivyokueleza, kuuona uzuri lazima uweze kufikiri kwa usahihi na ili kufikiri kwa usahihi lazima hisia uweke pembeni.

Mtu mmoja aliambiwa ana kansa na amebakiza miezi tisa tu ya kuishi. Habari ile ilimfanya akumbuke kwamba hakuna cha maana alichofanya kwenye amisha yake. Ndani ya miezi hiyo tisa aliweza kuandika vitabu vingi, na kansa ile ikapotea kabisa.

Chagua kuona zuri kwenye kila hali unayopitia.

SOMA; Nani Atarithi Matatizo Na Changamoto Zako?

  1. Rudi kwenye wakati uliopo, kuwa hapa sasa.

Akili zetu zinashangaza sana, tunapokutana na vikwazo au matatizo, mawazo yetu yanahama kabisa, yatakwenda kwenye wakati uliopita na kujikumbusha kila ambacho tumefanya siku za nyuma. Tutapitia kila hali, lakini kama unavyojua, hakuna cha kubadili kwenye siku za nyuma.

Ikitoka hapo akili itakupeleka siku zijazo, ambazo bado hata hujazifikia, utajijaza hofu ambazo hata bado hujazifikia. Sehemu pekee ambapo akili yako haikupeleki ni wakati huu, wakati uliopo sasa. Ambao ndiyo wakati wenye nguvu sana kwenye maisha yako.

Ni sasa ndiyo unaweza kuamua kuchukua hatua ya kubadili kabisa maisha yako. Ni sasa ndiyo unaweza kufanya kitu, siyo jana wala siyo kesho. Hebu irudishe akili yako pale ulipo, weka mawazo yako kwenye kile ulichokwama, na angalia ni hatua ipi ya kuchukua, japo kwa sasa. Ukiweka mawazo yako pale, lazima utaona wazi kabisa hatua ipi uchukue.

  1. Kazana na kile unachoweza kudhibiti.

Katika kila hali unayopitia, zipo pande mbili;

Kuna mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako, mambo ambayo unaweza kuyadhibiti. Hizi ni zile hatua unazoweza kuchukua ili kubadili hali uliyonayo sasa.

Upande wa pili, kuna mambo ambayo yapo nje ya uwezo wako, mambo ambayo huwezi kuyadhibiti kwa namna yoyote ile. Yaani hata ufanye nini, hakuna unachoweza kubadili.

Sasa kwenye hali yako, angalia yapo unaweza kuyadhibiti, na kisha chukua hatua. Jua ni yapi huwezi kuyadhibiti na hakikisha hayapotezi muda na nguvu zako haya kidogo.

Kwa mfano wetu wa aliyegundulika na kansa, angeweza kulaumu sana, angeweza kulia sana, lakini hiyo isingemsaidia chochote. Ila yeye aliamua kuchukua hatua, angalau hata akifa, basi jina lake lisipotee. Na hatua hiyo ikazaa matunda makubwa zaidi.

Hebu angalia pale ulipokwama sasa, ni hatua ipi unaweza kuichukua, kisha ichukue sasa.

Hivi ndivyo unavyoweza kuona fursa kwenye matatizo au changamoto yoyote unayopitia. Hivi ndivyo unavyoweza kuwa kwenye matatizo makubwa lakini watu wanakuona huna wasiwasi, kwa sababu unaangalia upande wa ukweli na kuangalia hatua zipi za kuchukua. Hatua hizi unajifunza kadiri unavyokwenda, hivyo jifunze kila siku kwa kuchukua hatua, kwa kila changamoto unayokutana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog