Hongera rafiki kwa mapambano ya siku ya leo.
Nina hakika umeweka juhudi za kutosha kadiri ya uwezo wako.
Na pale ambapo mambo hayakwenda sawa, kuna kesho, hakikisha unafanya kwa ubora zaidi.

Jioni hii karibu kwenye #GHAHAWA ambapo tunashirikishana makosa tunayofanya kwenye kufikiri na namna ya kufikiri sawasawa.
Najua kila mmoja wetu amewahi kuona matangazo kwenye tv au mabango.
Unaona msichana mrembo anatangaza sabuni au mafuta fulani.
Au mwanaume mtanashati anatangaza kinywaji fulani.
Sasa wengi tusichojua ni kwamba, matangazo haya yametengenezwa makusudi kutufanya tusifikiri sawasawa na hivyo kuchukua hatua za hovyo.
Kwa mfano, kwa kuona sura ya msichana mrembo anatangaza mafuta au sabuni, kila mwanamke atavutiwa kununua sabuni au mafuta yale, kwa kuamini yatamfanya kuwa mrembo zaidi.
Au mwanaume mtanashati anapotangaza kinywaji fulani, kila mwanaume anavutiwa kutumia kinywaji kile, akiamini na yeye atakuwa mtanashati.
Lakini hapo tunasahau kwamba hawajawa warembo au watanashati kitokana na kile wanachotumia, bali walikuwa warembo na watanashati kabla ya hapo, walizaliwa hivyo. Na sifa hiyo ndiyo imewafanya waweze kutumiwa kwenye matangazo.
Ukweli ambao wengi huwa hatupati nafasi ya kuung’amua ni kwamba hakuna uhusiano wowote kati ya tangazo na anayetangaza, chochote kinachotengenezwa pale, yaani uhusiano, ni kukufanya wewe usifikiri sawasawa, ili uchukue hatua ambazo zitawanufaisha wengine.
Swali la kuungana na hili, ambalo utafikiri na kutafakari mwenyewe. Je u aposikia shule fulani ndiyo zinaongoza kila mwaka, unafikiri ndiyo zina kila kitu bora kuliko shule nyingine zote? Au ni kwa sababu pia zinachagua wale wanafunzi ambao ni bora zaidi? Je wakipelekewa wale wanafunzi wanaochaguliwa popote bila ya kujali maksi na uwezo wao darasani bado shule hizo zitaongoza? Fikiri kwa kina hapo.
Nikutakie mapumziko mema na maandalizi bora ya kesho.
Kumbuka; usilale kabla hujaipa akili yako kazi ya kufanya kwa ajili ya kesho. Hivyo ipange kesho yako kabla hujalala.
Rafiki yako,
#KochaMakirita