Habari ya leo Mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri katika maisha yako. Maisha ni mapambano na usichoke kupambana kwani bila kupambana huwezi kupata kile unachokitaka. Hongera sana rafiki kwa zawadi nzuri ya siku hii ya leo kwani leo ni siku nyingine bora na ya kipekee sana katika maisha yetu. Kumbuka kutumia vizuri muda wako na iendee siku hii ya leo kwa utii, kujituma na kubuni kwenye kile unachofanya.

 

Mpendwa msomaji, napenda kutumia nafasi hii kuweza kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa hiyo, nakusihi sana tuweze kusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo.

Ndugu msomaji, ni wazi kwamba kila mmoja wetu amezaliwa katika familia na ni mpango wa Mungu kila mmoja wetu kuzaliwa katika familia. Familia ndiyo mzalishaji wa miito yote tunayoiona leo hii duniani, kwa mfano miito ya ndoa, utawa, upadre, uchunguaji na viongozi bora tunaowaona wote wanatokea katika familia. Familia ndiyo imekuwa mama wa jamii hii yetu ya leo ndiyo maana tusipokuwa na familia bora basi hatuwezi kujenga jamii bora. 

Zinahitajika juhudi za makusudi kuweza kutoa elimu elekezi kwa watu wote kujenga misingi imara katika familia zetu.

SOMA; Huyu Ndiye Mshauri Wa Kwanza Katika Maisha Ya Ndoa.

Ndugu mpendwa, licha ya kutambua familia ndiyo msingi wa jamii lakini pia je tunapaswa kujiuliza je chimbuko la familia ni nini? Kumbe basi, ndoa ndiyo chimbuko la miito yote hapa duniani au tunaweza kusema ndoa ndiyo chemchem ya miito yote tunayoiona hapa duniani kama tusipokuwa na ndoa nzuri na imara hatuwezi kuwa na familia bora hapa tutaendelea kutuanga maji katika kinu bila kuwa makini na ndoa zetu ambazo ndiyo wazalishaji wa familia na hatimaye jamii kwa ujumla.

Rafiki, tunahitaji wanandoa makini watakao weza kuzalisha familia bora na siyo bora familia. Ndoa zimekosa ubora wa kuzalisha familia imekuwa ni kama fasheni kufunga ndoa kwa gharama kubwa lakini baada ya siku chache wale waliooana wanaachana. Tunapaswa kutambua ya kuwa Mungu mwenyewe ndiye mwasisi wa ndoa , na inabidi ifikie wakati kila mtu asikilize sauti yake ya ndani ameitwa katika wito gani siyo kila mtu kukimbilia katika ndoa siyo fasheni ndiyo maana kuna miito ya aina mbalimbali.

Wazazi ambao ndiyo wanandoa wanapaswa kuwauliza watoto wanataka kuwa nani au kuwa katika wito gani na siyo kumchagulia hii ndiyo maana tunapelekea kuwa na ndoa nyingi za fasheni. Wazazi wanawachagulia watoto wao waende katika wito Fulani bila ridhaa ya mtoto hapa ndiyo maana hatupati watu wengi makini na wanaojitambua kama wana ndoa na kusudi lao nini hapa duniani.

Ndugu msomaji, wanandoa au wazazi ndiyo makuhani wakuu au wachungaji wakuu waliokabidhiwa jukumu la kuwachunga kondoo wao ambao ndiyo watoto wao. Wengi wamekuwa ni wazazi lakini hawana au hawajui sifa ya kuwa kuhani wa familia ni ipi. Kama tunavyojua sifa ya mchungaji mwema ni kuwaongoza kondoo wake kwa haki kuhakikisha anawapeleka katika malisho, na kuwaongoza katika sehemu za kunywa maji na hatimaye sehemu za mapumziko. Wazazi wamepewa watoto ili wawafundishe na kuwaongoza vizuri hilo ndiyo jukumu kuu waliopewa na Mungu. Tunapaswa kutambua kuwa kama wanandoa wasipokuwa makini hatuwezi kuwa na familia makini, na usilazimishe kuingia katika wito wa ndoa kama huna sifa hizo angalia au sikiliza umeitwa wapi ndoa siyo fasheni ambayo kila mtu anapaswa kuingia.

SOMA; Ndoa Inayokuzuia Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa, Na Jinsi Ya Kuivunja.

Tusipokuwa na ndoa nzuri hatuwezi kupata watumishi wazuri wa Mungu, hatuwezi kuwa na viongozi wazuri, hatuwezi kuwa na jamii chanya itakayoweza kuleta maendeleo na kuifanya dunia kuwa sehemu salama kuishi kwa kila mmoja wetu. Leo hii kama wazazi wasipokuwa makini katika malezi ya watoto tutaishia kuwa kama nchi za magharibi na kugeuza mbwa kuwa kama watoto wao. Leo hii inafikia mahali watu wanataka ndoa za jinsia moja yaani mwanaume kwa mwanaume, na mwanamke kwa mwanamke sasa kama ndiyo hivi dunia itaongezekaje?

Ndugu mpendwa, tunapaswa kuwa makini katika maisha haya, tusipojenga ndoa imara basi ni sawa na kuandika sifuri katika maji. Kama wazazi wa siku hizi wamekuwa na maadili ya hovyo watawezaje kuwafundisha watoto wao maadili mazuri? Nani atamfunga paka kengele au je kipofu anaweza kumuongoza kipofu mwenzake? Hapa ni pagumu tunahitaji kuamka na kubadilika kujenga kwanza ndoa imara, hatimaye ndoa inazalisha familia, hatimaye jamii.

Rafiki, jamii ni mali ya familia ambao watu wote wanatokea huko, hivi kama leo hii wazazi waliotuzaa sisi wangekuwa wako katika ndoa za jinsia moja tungewezaje kupatikana mimi na wewe leo hapa duniani? Kumbe basi ndoa ya kati ya mwanaume na mwanamke ndiyo chimbuko la miito yote hapa duniani. Kila mmoja anapaswa kusikiliza sauti yake ya ndani ameitwa wapi badala yake tuache mazoea ya kila mtu kuingia katika ndoa za kimazoea hatimaye tunakuja kuzalisha familia mbovu na hasara kwa jamii yote.

Hatua ya kuchukua leo, ndoa ndiyo chemchem ya miito yote duniani, hivyo basi wewe kama mwanandoa ndiyo kuhani mkuu wa watoto wako kuhakikisha unawaongoza katika njia sahihi. Je kama ndoa siyo ya watu sahihi itawezaje kuwa na familia sahihi? Tunatakiwa kwanza tuwe na wanandoa sahihi ndiyo mambo yataenda vema. Tusitegemee kupanda ndimu na kuvuna limao au chungwa.

Kwa kuhitimisha, malezi yamekuwa ni changamoto kubwa kwa wazazi wengi, kwa hiyo, wazazi kama makuhani wakuu wanapaswa kuwajibika katika hilo. Watu wanapaswa wajifunze mambo ya ndoa kabla ya kuingia vitabu viko vingi, watu wako walioishi katika ndoa muda mrefu ni vema kujifunza kuliko kuingia na kuwa kero kwa watu wengine tunawapa kazi kubwa viongozi wetu wa dini kusuluhisha migogoro ya ndoa kila siku, tunapaswa kujitambua kwani kujitambua ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.