Mwanasayansi Albert Einstein amewahi kunukuliwa akisema kwamba; riba mkusanyiko ni ajabu la nane la dunia, anayeielewa ananufaika, asiyeielewa analipa gharama. Kauli hii pekee inatosheleza kukushawishi kwa nini ni muhimu sana kujua na kutumia nguvu ya RIBA MKUSANYIKO au kama inavyofahamika kwa kiingereza COMPOUND INTEREST.
Leo tutakwenda kujifunza kwa kina kuhusu riba mkusanyiko na namna tunavyoweza kutumia kwenye maisha yetu ili kuweza kufanya makubwa na kutajirika sana.
Lakini kabla hatujaingia kwenye kujifunza kuhusu riba mkusanyiko, kwanza nikupe mfano halisi kupitia hadithi hii muhimu.
Hapo zamani alikuwepo mfalme wa India ambaye alipenda sana michezo ya kutumia akili. Siku moja mtu akaja na mchezo mpya mzuri unaofahamika kama chess (unachezwa kwenye kibao kama mchezo wa draft, una madirisha 64). Mfalme yule alifurahia sana mchezo ule na kumwambia aliyeugundua aseme chochote anachotaka na yeye atampatia kama zawadi kwa ugunduzi huo mkubwa. Mtu yule alimwambia mfalme, hitaji langu mimi ni dogo sana. Naomba unipe punje moja ya mchele kwenye dirisha la kwanza la ubao wa huo mchezo, na kila dirisha linalofuata, uzidishe mara mbili ya dirisha lililopita. Mfalme alikubali zawadi hiyo rahisi na kuwaagiza wasaidize wake kukokotoa punje hizo za mchele na kumpa yule bwana aende zake. Hapo ndipo alipopokea habari za kushangaza, kwamba mchele anaopaswa kupewa yule mtu, ni mwingi kuliko unaopatikana dunia nzima. Mfalme alishangaa mpaka alipooneshwa kwa mfano. Kwamba ubao una madirisha 64, dirisha la kwanza unaweka punje 1, dirisha la pili punje 2 dirisha la tatu punje 4, dirisha la nne punje 8 dirisha la tano punje 16 na kuendelea, mpaka wanafika dirisha la 64 zilikuwa jumla ni punje zaidi ya 18 milioni trilioni. Yaani trilioni milioni 18. Ni kiasi kikubwa sana cha mchele ambacho ni zaidi ya unaopatikana duniani. Mfalme alikubali ombi lile haraka kwa sababu hakujua nguvu iliyopo kwenye riba mkusanyiko ambayo tutakwenda kujifunza leo.
Mfano wa pili, na ambao nitakwenda kuutoa kama swali kwako. Kuna mtu yupo tayari kukupa fedha, na anakuambia uchague akupe shilingi milioni 100 leo, au akupe shilingi moja leo na kila siku akupe mara mbili ya aliyokupa jana yake kwa siku 30. Utachagua akupe ipi kati ya hizo mbili? Kwa hesabu za haraka utasema akupe milioni zako 100 na uondoke. Lakini hayo siyo maamuzi mazuri, wacha nikuoneshe hesabu za shilingi moja. Siku ya kwanza anakupa shilingi 1, siku ya pili shilingi 2 siku ya tatu shilingi 4 siku ya nne shilingi 8, siku ya tano shilingi 16, siku ya sita shilingi 32, siku ya saba shilingi 64 anaendelea kuzidisha mara mbili kia siku inayofuata. Kufika siku ya 30 atakupa shilingi 536,870,912!!! Hizo ni zaidi ya milioni mia tano. Unaona namna mkusanyiko ulivyo na nguvu? Sasa leo utakwenda kujifunza nguvu hii na namna ya kuitumia.
SOMA; Uwekezaji Unaolipa Riba Kubwa Sana
Riba mkusanyiko maana yake nini?
Riba mkusanyiko maana yake ni kupata riba kutoka kwenye riba yako. Iko hivi, ukiwekeza fedha mahali, tuseme umeweka milioni moja na riba ni asilimia kumi kwa mwaka. Mwisho wa mwaka utapewa milioni moja yako na riba ambayo itakuwa ni laki moja. Sasa kama hutaki kuchukua fedha hiyo wala riba yako, unaweza kuwekeza tena vyote kwa pamoja, kwa hiyo mwaka huu wa pili, utakuwa umewekeza milioni moja na laki moja, na mwisho wa mwaka huo wa pili, kwa riba ile ile ya asilimia kumi, utapata laki moja na elfu kumi. Umeanza kuona tofauti? Wewe uliweka milioni moja tu, mwaka wa kwanza umepata riba ya laki moja, mwaka wa pili riba ni laki moja na elfu kumi, huku msingi wako ukiwa siyo milioni moja tena, bali milioni moja na laki moja.
Maajabu zaidi yapo kwenye mwaka wa tatu, ambapo msingi unaoanza nao ni huu; milioni moja ya mwaka wa kwanza + laki moja ya riba ya mwaka wa kwanza + laki moja na elfu 10 ziba ya mwaka wa pili ambapo mwaka wa tatu msingi utakuwa = 1,110,000/=. Sasa ukiwekeza hii kwa mwaka wa tatu, riba itakuja 111,000/= na unapoanza mwaka wa nne, msingi unazidi kuongezeka. Ukiendelea na hesabu hizo, miaka kumi utakuwa umepata 2,707,041.49, na kama ukiwa mvumilivu zaidi, miaka 20 itafika shilingi 7,328,073.63.
Unaiona hiyo nguvu ya riba mkusanyiko, yaani kwa kuweka milioni moja mahali, ambapo kila mwaka unapewa asilimia kumi ya msingi wako, na usiguse fedha hiyo, ndani ya miaka kumi inakaribia milioni tatu, ndani ya miaka 20 inazidi milioni saba! Hii ndiyo nguvu ambayo matajiri wote duniani wanaitumia kwenye uwekezaji.
Hata wewe unaweza kuitumia nguvu hii, kwa kuwekeza maeneo ambayo yanakupa riba, hata kama ni kidogo ila ikarundikwa kwa muda mrefu, utapata faida kubwa sana baadaye.
Mambo mawili muhimu ya kuzingatia ili nguvu hii ifanye kazi kwako.
Jambo la kwanza; unahitaji kuanza mapema.
Umeona hiyo tofauti hapo juu, kwa kuweka kiwango kile kile, miaka kumi unapata karibu milioni tatu, lakini miaka 20 unapata zaidi ya milioni saba. Hii inaonesha kwamba kadiri msingi wako unavyokaa muda mrefu, ndivyo unavyozidi kunufaika. Hivyo kama unafanya uwekezaji kwa ajili ya kufika uhuru wa kifedha baadaye, mtu atakayeanza akiwa na miaka 30 na mwingine akaanza akiwa na miaka 40 pale wanapofika miaka 60 wote, aliyeanza na miaka 30 atakuwa amepata faida kubwa kuliko aliyeanza na miaka 40. Hata kama yule aliyeanza na miaka 40 atawekeza kiasi kikubwa kuliko wa aliyeanza na miaka 30.
SOMA; Mshahara Au Faida Pekee Haitakufikisha Kwenye Utajiri.
Kadiri uwekezaji unapoanza mapema, ndivyo unavyokusanya riba kubwa na kupata riba zaidi kwenye riba unayopata.
Jambo la pili; usiondoe hata senti kwenye uwekezaji wako.
Kama ulivyoona kwenye hiyo hesabu, matokeo hayo yanapatikana kama hakuna hata senti moja inayotolewa kwenye fedha uliyowekeza. Hivyo ili kuifaidi vizuri nguvu hii ya riba mkusanyiko, usitoe fedha yoyote kwenye uwekezaji wako. Acha riba ijiongeze na kukuzalishia zaidi.
Nyongeza; ukiendelea kuongeza msingi, unaendelea kunufaika zaidi.
Watu wengi hufikiri kwamba ili waweze kunufaika na nguvu hii ya riba mkusanyiko, ni mpaka wasubiri wapate kiasi kikubwa na kuwekeza. Lakini unaweza kuanza kwa kuwekeza kiasi kidogo na kila muda ukawa unaongeza uwekezaji wako. Unaweza kuwekeza kiasi kidogo na kila mwezi au kila mwaka ukaongeza uwekezaji wako. Kadiri unavyoendelea kuwekeza, kwa muda mrefu, huku hupunguzi msingi wako, unazidi kutengeneza faida kubwa zaidi.
Huu ni utangulizi tu wa dhana hii ya riba mkusanyiko, yapo mengi zaidi ya kujifunza kuhusiana na hili, hivyo nakukaribisha kwenye maoni hapo chini tulijadili hili kwa kina. Karibu sana, weka maoni yako kwa swali au nyongeza zaidi ili tuweze kujifunza zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Asante sana coach, ni taasisi gani uwekezaji wa riba mkusanyiko inafanya vizuri zaidi hapa Tanzania?
LikeLike
Asante Mbise,
Sijaona taasisi ambayo inafanya vizuri riba mkusanyiko kwa hapa Tanzania.
Ila vipande vya UTT ni kama vinakua kwa dhana hii ya riba mkusanyiko kwa sababu kila mwaka vinaongezeka thamani kwa kiasi fulani, mara nyingi kati ya asilimia 7 mpaka kumi. Hivyo kama hukuuza vipande vyako, mwaka unaofuata vinaendelea kukua zaidi kwa thamani ambayo vinayo kwa mwaka huo.
LikeLike
ahsante sana kwa uchambuzi huu kocha.
mimi binafsi nimeona ni njia nzuri kuwekeza kwa staili hii nadhani watu wengi wanapenda uwekezaji huu upo kwenye kununua hisa au kuwekeza kwenye vipande kwa kutumia pesa ndogo.
lakini pesa inapanda na kushuka thanani yaani mfano miaka 20 iliyopita 10000 thamani yake ilikua kama 100000 leo au hata hiyo milioni ilivoleo taani mtu akiwa na 10000 angeweza kupata hekali za kutosha kwa kununua shamba.hivyo miaka 20 ya baadaye hiyo milioni saba haiwezi kua na nguvu wakati huo.
kimsingi hapa tusiangalie sana thamani ya jana ilivo leo ila tuangalie leo kwa upande wa kesho itakuwaje dunia yetu iko kasi katiko mabaliko yetu
kwa maoni yangu hii tuitumie kujiongeza sisi kama leo nimefanya kazi nimepata 1000 basi kesho niongeze 2000 keshokutwa 4000 nadhani tutaenda kasi na dunia inavoenda
LikeLike
Ni kweli kabisa Emanuel ya kwamba thamani ya fedha hupungua kadiri muda unavyokwenda.
Na ndiyo maana kuweka akiba benki kwa muda mrefu unaishia kupoteza kwa sababu benki hawalipi riba nzuri.
Lakini kuwekeza kwenye vitu vinavyoongezeka thamani kadiri muda unaenda, ndiyo kuzuri zaidi.
Hisa na vipande pia vinabadilika thamani kadiri thamani ya fedha inavyobadilika. Ndiyo maana bei zake hupanda na kushuka lakini ukichukua muda mrefu, kwa ujumla bei inakuwa imepanda. Hivyo hupotezi sana kwenye mabadiliko ya thamani ya fedha.
LikeLike
Ahsante sana kaka Makrita. Nmekuwa nawekeza kwenye mfumo wa UTT kwa mwaka mmoja sasa, Ila nmekuwa nataka nianze kuwekeza kwenye Hisa. Mpango wangu ni kuchukua Uwekezaji wangu wa UTT na kuuweka kwenye Hisa. Naomba ushauri wako hapo kaka, ni bora niziache pesa za UTT au itakuwa sawa kuzitumia kununua Hisa?
LikeLike
Vizuri Daniel,
Nachokushauri hapo ni zile za UTT ziache na pia endelea kuwekeza huko kidogo kidogo.
Na kwenye hisa anza na kiasi kingine cha fedha. Wekeza kote kadiri ya unavyoweza, fanya hivyo kwa malengo ya muda mrefu.
LikeLike
Kuna uhusiano gani kati ya compound interest na fixed diposit?
LikeLike
Fixed deposit inaweza kutumia kanuni ya kompaund interest, lakini unapoweka fedha hizo ni kwa kipindi fulani ambapo huwezi kuzipata kabla ya hapo, labda kwa gharama kwako, kwa upande wa riba.
Hivyo inakuwa fixed kwa kipindi hicho ambacho umechagua. Na kadiri muda unavyokuwa mrefu, ndivyo riba inavyozidi kuwa kubwa.
Hivyo kwa kujumuisha naweza kusema compound interest ni dhana au kanuni wakati fixed deposit ni kitendo cha kuweka fedha ambapo utapata faida kwa compound interest.
LikeLike