Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi nzuri sana ya siku hii ya leo katika maisha yako kwani leo ni siku bora na ya kipekee sana katika maisha yako. Hivyo basi, unaalikwa kutumia vizuri muda wako ili uweze kuvuna matunda mazuri unayotarajia kwenda kuyapanda asubuhi ya leo. Pia, hongera kwa zawadi ya mwezi wa sita lakini pia nakutakia kila la heri katika kupambana na maisha mpaka upate kile unachokipata.

 

Mpendwa msomaji, nipende kutumia nafasi hii kuweza kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja mambo mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Hivyo basi, nakusihi sana tuweze kusafiri kimawazo wote kwa pamoja hadi pale nukta ya mwisho ya somo letu la leo. Katika somo letu la leo ninakwenda kukushirikisha somo lenye kichwa cha habari kinachosema hawa ndiyo watu wenye sifa za kufanikiwa hapa duniani, je ungependa kujua ni watu gani hao? Karibu sana ndugu msomaji tuweze kujifunza wote kwa pamoja.

Kila mtu anaweza kufanya chochote kama akiamua kufanya bila kusingizia sababu yoyote ile. Tumeshazoea katika jamii yetu kusikiliza wimbo unaoimbwa na kila mtu ambao ni sina muda wa kufanya au nitafanya baadaye na hatimaye baadaye inakuwa baadaye kweli. Ni wazi kabisa kila siku tunazika ndoto zetu nyingi ambazo tungeweza kuzifanya basi leo hii dunia ingekuwa sehemu bora sana ya kuishi mimi na wewe. Kizazi cha watu wa sababu kimekuwa kimeamua kujichagulia kulalamika na kutafuta sababu nyingi za kwa nini hawawezi kuliko kutafuta matokeo kwa nini wanaweza.

SOMA; Do More Great Work (Acha Kuwa Bize Na Anza Kufanya Kazi Yenye Maana)

Kila mtu anaweza kufanikiwa katika kitu fulani kwa sababu uwezo anao mkubwa aliopewa na Mungu ukilinganisha na viumbe vyote hapa duniani. Na habari njema ni kwamba kila mtu amekuja na zawadi yake hapa duniani lakini wengi wamekuwa ni wachoyo na zawadi zao hivyo wanaona ni bora kufa nazo kuliko kuisaidia dunia. Na wachache wanaotambua kusudi lao ndiyo wanaoamua kugusa maisha ya watu wengine kupitia zawadi kubwa waliyopewa na Mungu na ubaya au uzuri wa zawadi hii ni kwamba hakuna zawadi ambayo inafanana na mtu kwa hiyo, kila mtu ana zawadi yake ya kipekee ambayo haifanani na mtu mwingine.

Ndugu msomaji, licha kuwa kila mtu amepewa sifa za kufanikiwa lakini kama kila binadamu atakuwa amekosa sifa hii basi hawezi kushinda kwenye kitu chochote kile. Sifa yenyewe ni kukaa chini na kufanya, hapo awali nilikueleza kuwa leo nitakushirikisha somo lenye kichwa cha habari kinachosema hawa ndiyo watu wenye sifa za kufanikiwa hapa duniani na watu hao ni wale ambao wanaweza kukaa chini na kufanya. Kama mtu hana sifa ya kukaa chini na kufanya basi amepoteza sifa ya mtu anayepaswa kufanikiwa hapa duniani. Hata usijisifie wewe ni mtu wa bora kiasi gani lakini bila kukaa chini na kufanya huwezi kupata matokeo yoyote chanya katika maisha yako. Kama ni kuongea kila mtu anaongea lakini wanaokaa chini na kufanya ni wachache sana.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria. ( 2)

Mpenzi msomaji, unataka kufanya nini katika maisha yako? Je tatizo lako ni kupata muda? 

Unafikiri kuna siku muda utaongezeka? Au unafikiri kuna siku majukumu yatapungua katika maisha yako? Kama unafikiria hivyo unajidanganya mwenyewe kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo majukumu nayo yanaongezeka zaidi. Je ufanye nini sasa? Jawabu ni moja jirisishe falsafa hii ya kukaa chini na kufanya na utapata chochote kile unachotafuta juu ya kitu fulani.

Rafiki, je unataka kuimba, kuandika, kuchora, kucheza mpira na mengine mengi basi njia rahisi au falsafa rahisi ni kununua mbinu ya kukaa chini na kufanya utafanikiwa. Watu wengi wanaweza kufanya ila wamekosa nidhamu ya kukaa chini na kufanya. Unataka kusoma kitabu kaa chini na soma acha kutafuta sababu za muda, una muda mwingi wa kufanya chochote katika maisha yako. Tumia saa moja ya dhahabu (Golden Hour) kila siku katika maisha yako kufanya kitu unachokipenda na hakika utakuwa bora.

Hatua ya kuchukua leo, kama una kitu chochote unataka kufanya usisubiri kupewa ruhusa bali kaa chini na fanya, ruhusa yako iwe ni kukaa chini na kufanya. Epuka kutafuta sababu kwani ukitafuta sababu huwezi kukosa na utapoteza sifa ya kuwa mwana mafanikio.

Mwisho, tunaalikwa kutumia falsafa ya kukaa chini na kufanya ili tuweze kufanikiwa katika maisha yetu. Tuna mambo mengi a mbayo tunaweza kuyafanya lakini tunakosa nidhamu moja tu nayo ni kukaa chini na kufanya. Utamaduni wa uvivu unazaa walalamikaji wengi katika jamii yetu na epuka kuwa katika utamaduni huo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.