Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili tuweze kupata matokeo bora sana.


Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya mambo makubwa kwenye leo na kila siku kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo titafakari kuhusu EFFORTLESS SUCCESS, yaani MAFANIKIO BILA YA KUWEKA JUHUDI KUBWA.
Sijui hii dhana imeanzia wapi, lakini naona inatafuna hichi kizazi kuliko ugonjwa mwingine wowote ule.
Pamekuwa na wimbi kubwa la watu wanaokimbizana na aina mpya za biashara ambazo unaweza kupata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi na bila kufanya kazi.
Watu, wakiwa na akili zao timamu, wanaacha shughuli zao na kuanza kukimbizana na mambo hayo, ambayo hayana msingi wowote.
Hapo ndipo unajiuliza hawa watu wanafanya hayo kwa misingi ipi?

Rafiki, kila kitu hapa duniani kinaendeshwa kwa misingi.
Ipo misingi ya utajiri,
Ipo misingi ya mafanikio,
Ipo misingi ya biashara,
Ipo misingi ya kazi,
Ipo misingi ya mahusiano.

Sasa kama unajaribu kufanya kitu chochote, kabla hujaijua misingi, unataka kujipoteza. Kwa sababu usipojua misingi, utapotezwa, utalaghaiwa, utatapeliwa na hutadumu kwa muda mrefu.

Kwa wale watafuta biashara za mafanikio ya haraka bila kazi, niwakumbushe tum msingi mkuu wa biashara ni huu; kubadilishana thamani kwa fedha. Yaani mtu mmoja lazima awe na thamani, ambayo huenda ni bidhaa au huduma inayotatua matatizo ya wengine, au kutimiza mahitaji yake, na mwenye uhitaji lazima awe na fedha ya kulipia bidhaa au huduma ile. Nje na msingi huu, hakuna biashara. Kama unakaa tu kwa kufanya kitu kisicho na mchango kwa wengine na fedha zinaingia, usijione una bahati, jua tu poromoko liko mbele hako.

Mwisho kabisa, kila mtu kufanya kitu haimaanishi kitu hicho ni kweli. Na watu kupata pesa haimaanishi wanachofanya ni sahihi. Maana hili limekuwa linatumiwa na watu kujihalalishia, kwamba mbona mtu fulani anafanya, au mbona wengi wanafanya, wengi huwa wabakosea, mara zote. Kadhalika kwenye kupata fedha, hata kama unaona kila mtu anapata fedha, haimaanishi wanachofanya ni sahihi. Anza na misingi, kama ipo sahihi, hapo ni pazuri. Ila kama misingi siyo sahihi, usipogeze muda wako.

Nikutakie siku njema sana ya leo, tumia muda wako kufanya mambo ya msingi, usikubali kupotoshwa.

Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info