Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa, bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. Ni maneno mazito sana ambayo hunilazimu nijitafakari uwepo wangu kwenye sayari hii inayoitwa dunia. Naamini na wewe msomaji wa Makala hii ipo sababu ambayo imekulazimu kusoma safu hii, na sababu kuu ni kupata maarifa. Pamoja na mengine yote jitihada zetu ziwe katika mafanikio ya mwili na roho.

 

Makala hii ni maalumu kwa marafiki zangu ambao wamekuwa wakihoji waanzie wapi kwenye safari hii ya mafanikio katika uwekezaji wa ardhi na majengo. Kwa ufupi ni kutaka kufahamu hatua mbalimbali kwenye mfumo wa uwekezaji huu. Hawa ni marafiki zangu ambao wana lengo la kuanza safari ya mafanikio katika uwekezaji wa ardhi na majengo. 

Nimeona ni vema nikawashirikisha watanzania wengine ili niwape baadhi ya majibu ya maswali ambayo yamkini wanajiuliza kama ilivyo kwa marafiki zangu. Leo tutaangalia hatua mbalimbali za uwekezaji huu na fursa zinajitokeza pamoja na changamoto zake ili kwa umoja wetu tuweze kutembea salama na kwa uhakika ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea kujitokeza.

  1. KUMILIKI ENEO LA ARDHI ISIYOENDELEZWA


Watanzania wengi wapo kwenye hatua hii ya awali, hatua hii ni hali ya kumiliki ardhi ambayo haijaendelezwa na kuthaminishwa kwa namna yoyote. Haijalishi ni mjini au vijijini, ardhi iliyo kwenye kundi hili ni ile ambayo hadi leo bado unatafakari kuwa utaitumia kwa matumizi gani ambayo itakuletea tija au unaendelea kuitumia vyovyote unavyotaka kwa kuwa haipo kwenye urasimishwaji. Ni ardhi ambayo umeimiliki ukisubiri wakati muafaka uiendeleze au hata kuiuza kwa wenye uhitaji. Hapa Tanzania watu binafsi, kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali yanamiliki ardhi kwenye hatua hii wakiwa na matarajio chanya kwamba wataiendeleza pale watakapokuwa tayari endapo watalazimika kufanya hivyo au kuiuza kwa wengine endapo thamani ya ardhi itamshawishi kuwa atanufaika kwa kadri anavyotarajia.

SOMA; Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa”

  1. URASIMISHAJI WA ARDHI ISIYOENDELEZWA

Hatua hii inajumuisha ardhi ambayo imeshasanifiwa kwa matumizi mbalimbali yaliyohakikiwa vema na maafisa ardhi. Ni ardhi ambayo ina mgawanyo wa matumizi mbalimbali kama vile eneo la makazi, biashara, viwanda, kilimo, mifugo, huduma za jamii na maeneo ya wazi. Kazi hii ya urasimishaji wa ardhi hufanywa na wataalamu wa mipango miji na vijiji wakishirikiana kwa karibu na wataalamu wa mazingira. Hatua hii ni muhimu sana kwa maendeleo na matumizi ya ardhi. Rafiki yangu mpendwa kama upo kwenye hatua hii ya umiliki wa eneo la ardhi ambayo imesharasimishwa unapaswa ujiulize kuwa upo kwenye kundi gani la matumizi ya ardhi unayoimiliki. Ufahamu huu utakuwezesha kujitathmini na kufanya maamuzi sahihi yenye manufaa kwako binafsi na kuwa rafiki wa mazingira. Mfano upo kwenye eneo la mifugo na huna mpango wa kuwekeza kwenye mifugo, utapaswa uwape umiliki wenye matumizi halisi na wewe kutafuta eneo jingine linaloendana na matumizi ya malengo yako. Zama za leo zinahitaji sana “master plan” za miji na vijiji ili kuondoa mwingiliano wa matumizi ya ardhi ambao unahatarisha amani.

  1. KUMILIKI ARDHI ILIYOTHAMINISHWA NA KUPIMWA

Hatua hii inajumuisha eneo la ardhi ambayo imerasimishwa, kupimwa na kuthaminishwa rasmi na wataalamu wa ardhi. Hii ni hatua ambayo kila kipande cha ardhi iliyorasimishwa kugawanywa vipande kwa njia ya vipimo kwa kuzingatia matumizi rasmi ya kila kipande cha ardhi. Hapa ndipo tunapopata viwanja vya matumizi mbalimbali tunavyo vihitaji. Eneo lililorasimishwa makazi, tutapata viwanja kadhaa vya makazi, vivyo hivyo kwenye maeneo yalirasimishwa matumizi ya biashara, viwanda na huduma za jamii. Hatua hii tunapata mpangilio mzima wa miundombinu na huduma mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na jamii kwa ujumla. Kwa kiasi kikubwa tumeshindwa kufikia hatua hii hali ambayo imesababisha maisha ya kadhia kwa walio wengi. Ingawa kwa sasa wamejitokeza wataalamu na kampuni mbalimbali kutoa huduma hii ya upimaji lakini changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa watanzania wengi kuhusu umuhimu wa upimaji wa ardhi. Hii ni hatua muhimu sana ya umiliki wa ardhi kwa wale marafiki wanaotaka kuwekeza kwenye majengo kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Na endapo unamiliki ardhi isiyoendelezwa ni vema ukajitahidi kuifikisha hatua hii ambayo itakuhakikishia usalama wa umiliki wako.

SOMA; Usifanye Makosa Haya Kwenye Uwekezaji Wa Majengo.

  1. UENDELEZAJI WA MAJENGO NA MIUNDOMBINU

Hii ni hatua ambayo waendelezaji wa majengo na miundombinu huchukua nafasi zao ili kuonesha na kuainisha ubunifu na umaridadi wao. Hatua hii ndipo upembuzi yakinifu hufanyika, usanifu na ujenzi wa majengo na miundombinu huratibiwa kwa taratibu zote zinazopaswa kufuatwa katika kuiendeleza ardhi hiyo. Unapaswa kuwa makini kabla na baada ya ujenzi kuendana na taratibu zilizopo ili ujiweke sehemu salama nyakati zote. Tumia wataalam wa ujenzi watakao kusaidia na kuhakikisha kuwa unapata kilicho bora na kukidhi matarajio ya ndoto zako katika uwekezaji. Kwa uendelezaji wa majengo marefu na makubwa inakulazimu utumie kampuni za ujenzi zenye uwezo kulingana na aina ya majengo ili kufikia viwango vyenye ubora unaopaswa na kulinda usalama wa watumiaji.

  1. MATUMIZI YA MAJENGO NA MIUNDOMBINU ILIYOENDELEZWA

Hii ni hatua ambayo waendelezaji wa majengo na miundombinu wamemaliza ujenzi kulingana na usanifu uliofanywa kabla ya ujenzi na sasa wamekabidhi kwa watumiaji. Kwenye hatua hii unaweza ukajenga kwa matumizi yako, ukaamua kuuza au hata kupangisha, inategemea mipango na aina ya uwekezaji wako utakavyo uendesha. Hapa Tanzania watu binafsi, kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali wameshaanza kufikia hatua hii ya uwekezaji, changamoto kuu inayowakabili ni hali ya kupanda na kushuka kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Pia hali ya kukosa maarifa ya usimamizi na hali ya masoko ya nyumba imekuwa ikiwanyima raha wawekezaji wanaokua kwa sasa. Ni vema ukaweka mipango na usimamizi wa hali ya juu kuhakikisha unaulinda uwekezaji ulioufanya ili kuepuka hatari zisizojulikana na ambazo zinaweza kuzuilika.

  1. MAREKEBISHO YA MAJENGO NA MIUNDOMBINU

Kila chenye mwanzo kina mwisho, hata kwenye ujenzi hali ipo hivyo. Ujenzi wa majengo na miundombinu yake ina muda wenye ukomo wa matumizi kulingana na ubora wa malighafi za ujenzi zilizotumika. Baada ya muda kadhaa wa matumizi, sehemu mbalimbali huanza kuchakaa na kuharibika kutokana na sababu mbalimbali zinazoweza kujitokeza kutokana na mazingira halisi. Hali hii itakulazimu uiuze, ununue au kuirekebisha ili kuendana na hali ya usasa wa wakati huo. Zipo taratibu zinazoratibu aina mbalimbali za marekebisho ya majengo na miundombinu kwenye miji na vijiji, ingawa watu wengi hawajui hili. Kuna viwango fulani vimewekwa ili kukidhi mahitaji na mwonekano wa mji husika, endapo utashindwa kukidhi viwango hivyo utalazimika kuwakabidhi umiliki au kushirikiana na wenye uwezo wa kufikia 
viwango husika.

  1. UENDELEZAJI MPYA WA MAJENGO NA MIUNDOMBINU


Hii ni hatua ya uzee au ukongwe wa mji ulioendelezwa kwa muda mrefu na umefikia hatua ya kuonekana hali ya ukale na kutokidhi au kuendana na mahitaji na matumizi ya hali ya usasa kwa wakati huo. Hali hii imeshaanza kujitokeza hapa Tanzania, vijijini nyumba za tembe zinapotea na mijini majengo marefu yanachukua nafasi yake. Hali hii husababishwa na maendeleo ya miji na vijiji hali inayolazimu wataalamu wa mipango miji na vijiji kupandisha hadhi kwenye baadhi ya maeneo yaliyofikia viwango husika. Rafiki kama upo kwenye hatua hii ya ukongwe na huna uwezo wa kuendana na “master plan” mpya yenye hadhi ya usasa, utakuwa mgeni wa mji mpya unaoendelea pembezoni kwa wakati huo, tofauti na hapo unapaswa utunishe misuli ya “akili na fedha”.

Maendeleo ya ardhi na majengo ni kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine, hapo utakuwa umeongeza thamani, na ndiyo maana halisi ya uwekezaji. Hizo ni hatua muhimu za uendelezaji wa ardhi hata kufikia hatua ya mji au kijiji. Kuwa na miji au vijiji hatarishi kutokana na makazi holela ni kutokana na kuiruka hatua ya pili na hatua ya tatu. Tafakari…! 

Upo kwenye hatua gani ya mafanikio yako?

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com