Leo nakuletea makala hii ambayo nitahitaji uwe mtulivu sana, na uisome kwa kina ili tuweze kuelewana. Ni makala yenye hoja kinzani, hivyo ukienda nayo haraka, unaweza usinielewe, au ukaona inakwenda kinyume na kile ambacho nimekuwa nakushirikisha kila siku.
Ninachotaka kukuambia ni kwamba, watu wengi waliofanikiwa ni waongo, na hii inapelekea wale ambao wanajifunza kutoka kwao kushindwa kufanikiwa. Na nitakueleza kwa kina kwa nini hilo lipo hivyo. Na kama ilivyo kawaida yangu, nitakupa hatua ya kuchukua wewe ili uweze kufanikiwa.
Maana ya mafanikio.
Siyo vibaya tukakumbushana tena maana ya mafanikio, kwa sababu wengi wanaposikia neno hilo, mawazo yao moja kwa moja huenda kwenye fedha na mali. Hayo ni mafanikio, lakini ya eneo moja tu. Mafanikio ni dhana pana inayogusa kila eneo la maisha yetu wanadamu. Mafanikio kwenye maisha ni kuwaza kufikia kile ambacho mtu anapenda kufikia, kuweza kufikia ndoto za maisha yake. Kwa dhana hii, mafanikio ni tofauti kwa kila mtu. Kwa mwingine kitu kinaweza kuwa cha kawaida, lakini kwa mwingine yakawa mafanikio makubwa.
Lakini pia kuna mafanikio kwenye maeneo madogo madogo ya maisha yetu. Mafanikio kwenye maeneo kama biashara, kazi, fedha na kadhalika, yanaweza kupimwa kwa usawa kwa wote. Kwa mfano watu wanaweza kusema fulani amefanikiwa kwenye biashara yake, kwa sababu alianza na mtaji wa laki moja, na sasa ana mtaji wa mabilioni. Au mwingine amefanikiwa kwenye kazi yake kwa sababu alianza kama mtu wa chini, na sasa ni bosi au mkurugenzi. Haya ni mafanikio ya maeneo madogo madogo ambayo kila mtu anaweza kuyaona.
Eneo hili la mafanikio ya maeneo madogo madogo ya maisha, ndipo kuna uongo mwingi sana. Uongo huu umepoteza watu wengi na kuwakuta wanaona huenda wao hawakupangiwa kufanikiwa.
SOMA; Uongo Huu Unaojiambia Kila Siku, Ni Adui Mkubwa Wa Mafanikio Yako.
Umewahi kusikia hadithi hizi?
Zipo hadithi nyingi kwenye maisha yetu ya kila siku ya watu waliofanikiwa.
Utasikia huyu alianza na genge, lakini sasa hivi anamiliki viwanda.
Au alianza kuuza karanga na sasa anamiliki biashara kubwa.
Au alianza kama mfanya usafi ofisini na sasa ni bosi mkubwa.
Aliacha shule na kwenda kufanya biashara na sasa anamiliki biashara kubwa.
Umewahi kuzisikia? Kama ndiyo, niambie watu hao wanasemaje?
Watu hawa wanapoulizwa siri zao za mafanikio, na tunakuwa na shauku kubwa ya kuzisikiliza, huwa wanatuambia hadithi nzuri sana za mafanikio yao. Watatuambia ni kuweka juhudi kwenye kazi, kufanya unachopenda na kutokukata tamaa. Mambo haya kwanza siyo siri, yapo wazi kabisa. Lakini tunapoambiwa na waliofanikiwa, ghafla yanabadilika na kuwa siri, na tunayabeba kwa moyo mkuu.
Sasa shida kubwa inakuja pale tunapojaribu kuyafanyia kazi yale tunayoambiwa na wale waliofanikiwa. Na kabla hatujafika mbali, changamoto zinabisha hodi. Na hapo ndipo hatujui tufanyeje tena, maana mstari tuliopewa, ni fanya kazi, penda unachofanya, usikate tamaa. Lakini changamoto uliyokutana nayo ni kubwa mno, hujui hata ufanyeje, unapojipa moyo usikate tamaa, mbele unaona giza. Na hapa ndipo unaweza kuona na hata kuamini kwamba, mafanikio ni kwa ajili ya wengine, na siyo kwa ajili yako.
Mafanikio yanayosimuliwa na yanayofundishwa.
Kitabu cha kwanza kabisa kuandika kuhusu maisha ya watu wenye mafanikio, ni THINK AND GROW RICH. Mwandishi wa kitabu hichi, Napoleon Hill, alitumia miaka 25, kuwafuatilia watu wenye mafanikio makubwa. Hebu fikiria hapo miaka ISHIRINI NA TANO, anawafuatilia kwa karibu. Anaongea nao, anafuatilia biashara zao, anaona mambo wanayoyafanya na matokeo wanayoyapata. Na hapo ndipo akaja na sheria 17 za mafanikio.
Kitabu hichi kimekuwa na mafanikio makubwa, kimeweza kuwasaidia wengi kutoka kwenye nyakati ngumu na kufanya makubwa. Na hii yote ni kwa sababu kitabu hichi hakikusimulia mafanikio, bali kilifundisha mafanikio.
Hakikuwa ni kitabu cha hadithi za fanya kazi, penda unachofanya, usikate tamaa. Bali ni kitabu ambacho kimeyachimba mafanikio kwa undani wake. Ndani ya kitabu hichi tumejifunza mambo ambayo hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa anaweza kukuambia anafanya. Kwa sababu ambazo nitakueleza hapo baadaye kidogo.
Kitabu hichi kimeeleza nguvu kubwa sana iliyopo kwenye akili zetu. Kimeeleza namna ya kuitumia nguvu hii vizuri. Kimeeleza mambo mengi ambayo watu wamekuwa wanayafanya bila ya kujua lakini ni msingi muhimu wa mafanikio yao.
Kwa nini watu waliofanikiwa ni waongo?
Watu waliofanikiwa ni waongo, kwenye kukueleza kuhusu mafanikio yao, kwa sababu hawakuelezi kila kilichopelekea wao kufanikiwa. Naomba unielewe vizuri hilo, na nitalitetea vizuri sana.
Yale wanayokueleza, ni mambo ya juu juu, ambayo tayari unayajua. Lakini yapo mambo ya ndani, ambayo huwa hawayasemi, haya ni mambo ambayo yana mchango mkubwa sana kwenye maisha yao na mafanikio yao. Mambo hayo yamewaweka kwenye eneo sahihi kwa wakati sahihi.
SOMA; Watu Wanaokuzuia Kufanikiwa Lakini Huwajui Ni Hawa….
Watu waliofanikiwa hawasemi yale ya ndani kuhusu mafanikio yao kwa sababu mbili;
Moja; jamii inayowazunguka haipendi kusikia ukweli mchungu kuhusu mafanikio. Wanapenda kusikia vile wanavyotaka kusikia, ambavyo vitawafanya wajisikie vizuri. Fanya kazi, penda unachofanya, usikate tamaa. Maneno hayo yanatia faraja, na yanaeleweka kwa urahisi.
Lakini siku moja mtu aliyefanikiwa aitwe kwenye tv kuhojiwa na aanze kusema haya;
Tangu naanza mpaka leo huwa naamka mapema na kuchelewa kulala, watu hawatasikiliza, sana sana watasema mtu huyo hana maisha, hana balance na maneno mengine kama hayo.
Au mtu akasema nimefanikiwa kwenye kazi kwa sababu kila wakati nilikuwa nafanya kazi kubwa kuliko niliyopangiwa. Nilifanya zaidi ya nilivyolipwa na sikuwa mtu wa kulalamika bali kuchukua hatua. Na wanaomwangalia watasema hamna kitu kama hicho, siwezi kufanya zaidi ya ninavyolipwa, kwanza wananilipa kidogo.
Hiyo ni mifano michache na rahisi, ila yapo makubwa zaidi ya ndani ambayo wakiyasema, watu watanza kuwaangalia vibaya. Na wala siyo mambo ambayo yapo kinyume na sheria, bali ni mambo ambayo hayajazoeleka kwenye jamii zetu.
Sasa kuepuka hilo la kusemwa vibaya na kuonekana watu wa ajabu, waliofanikiwa wamekuwa wakiishia kuongea maneno yale yale, ambayo ni rahisi na siyo kweli.
Sababu ya pili ni wao wenyewe kutokujua kipi hasa kimewafanya wafanikiwe. Yaani watu waliofanikiwa, kuna vitu wanavifanya, kwao ni kama mazoea, lakini kumbe ni msingi muhimu sana kwa mafanikio yao. Wao wanafanya kwa sababu wamechagua kufanya hivyo, lakini ndipo mafanikio yao yalipo.
Hivyo wanapoulizwa, hawawezi kusema kwa sababu hata wao wenyewe hawajui. Na hivyo kuishia kusema mambo ambayo siyo ya kweli. Hapa ndipo vitabu kama THINK AND GROW RICH, viliwafungulia watu mlango na kuona yale ambayo hakuna ambaye ameweza kuyaona.
Sasa unawezaje kuvuka haya ili kufanikiwa?
Unapaswa kufanikiwa, ni haki yako kufanikiwa, na hakuna wa kukuzuia, bali wewe mwenyewe. Na moja ya njia unazoweza kutumia kujizuia ni kupokea na kuamini hadithi ambazo siyo za kweli kuhusu mafanikio. Na hii ndiyo maana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, mara zote nakushauri utengeneze mfumo wako mwenyewe wa mafanikio. Tumia hadithi za wengine kama hamasa, lakini tengeneza mfumo wako mwenyewe. Mfumo huu ukuwezeshe wewe kuweka juhudi kwenye kile unataka kufanya, na pia ukuwezeshe kupambana na changamoto mbalimbali utakazokutana nazo kwenye lolote utakalochagua kufanya.
Mfumo ni muhimu sana rafiki, muhimu mno. Na ukishakuwa na mfumo, unachofanya ni kuufuata. Usiwe mtu wa kuruka ruka na kila unachosikia, badala yake angalia mfumo wako unauboreshaje kwa kile unachojifunza kila siku.
Sehemu muhimu ya mfumo wako wa mafanikio ni kile unachofanya na namna unavyoweza kukabiliana na kuzishinda changamoto utakazokutana nazo kwenye kila unachofanya. Mfumo lazima ukuwezeshe wewe kutumia mazingira yoyote unayopitia kama fursa kwako na siyo kikwazo kwako. Mfumo lazima ukuwezeshe wewe kutumia kila nafasi unayoipata kuwa bora zaidi. Na mfumo huo utakuwezesha kufikia mafanikio.
Ukipata nafasi ya kukaa karibu na waliofanikiwa, usiishie tu kusikia wanasema nini, badala yake angalia wanafanya nini. Angalia namna maisha yao walivyoyapangilia. Angalia namna wanavyofanya maamuzi yao, angalia namna wanatatua changamoto zao, na angalia namna wanajihusisha na wengine. Utajifunza mengi sana na kuona mifumo wanayoitumia wao kufanya makubwa, hata kama hawawezi au hawapo tayari kuieleza kwa wengine.
Nihitimishe kwa kusema, watu waliofanikiwa ni waongo kwenye hadithi zao za mafanikio, kwa sababu ambazo siyo mbaya. Kama wewe utachukua hadithi hizo kama zilivyo, unaweza kukwama. Lakini kama utaenda mbali zaidi na kuchimba ndani zaidi, utaona yale ambayo wengine hawayaoni, na hayo yatakuwezesha kufanikiwa sana kwenye kile unachofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Shukrani sana kocha kwa makala hii nzuri.
Umeongelea kuhusu mtu kujitengenezea mfumo na kwenda nao kwa kila kitu kinachotokea kuangali kuwa kinaendana na mfumo uliojiwekea ndipo ukifanye. Ningependa ugusie namna ya kuutengeneza huo mfumo na ikiwezekana uelezee kwa mfano yaan mfano wa mfumo wa maisha unaogusa nyanja zote za Maisha.
LikeLike
Asante Peter,
Kama ulishiriki semina ya kuanza mwaka huu 2017 niliyoiendesha kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tulifanya kazi hiyo ya kutengeneza mfumo na mwisho nilitoa kitabu cha mwongozo wa maisha ya mafanikio.
Rejea kitabu kile, kimegusa maeneo yote muhimu ya maisha na unaweza kukitumia kama mfumo mzuri wa maisha ya mafanikio.
LikeLike
Ahsante kocha kwa makala hii iliyo nifungua zaidi ya nilivyo kuwa naziamini hadithi hizi.
Kocha ninawezaje kutengeneza mfumo wangu utakao niongoza/kuutumia kwenye hatua za mafanikio yangu.
Ernest Lwilla
LikeLike
Unatengeneza mfumo wa maisha yako kwa kuzingatia yafuatayo;
1. Kuwa na ndoto kubwa ya maisha yako, haya ni maono ya maisha yako, unataka kuwa wapi.
2. Weka mipango ya namna gani unafika kwenye ndoto hiyo kubwa ya maisha yako.
3. Panga hatua za kuchukua kila siku ili kuweza kufikia maisha hayo ya ndoto yako.
4. Fanyia kazi kila siku bila ya kuacha.
5. Kila siku jifunze mambo mapya kwenye yale unayofanya, pia jitathmini kwa namna unavyoenda.
Huu ni mchakato wa kila siku, kupambana na changamoto unazokutana nazo, kuwa bora zaidi kadiri unavyokwenda.
LikeLike