Biashara ni ngumu, hilo halina ubishi, lakini ugumu mwingine tumekuwa tunautengeneza sisi wenyewe. Hasa pale ambapo tunakuwa tunatafuta njia rahisi ya kufanikiwa kwenye biashara.
Kwa kuwa kufikiri ni kazi ngumu, na kwa kuwa njia bora za kuifanikisha biashara yako kutakuhitaji ufikiri, watu wanakwepa hilo. Na badala yake wanaangalia kipi rahisi kufanya, na mara nyingi kinakuwa kuiga kile ambacho wafanyabiashara wengine wanafanya.
Ndiyo maana eneo linaweza lisiwe na biashara ya aina fulani, mtu mmoja akaja kuanzisha, na baada ya muda kila mtu akakimbilia kuanzisha biashara ya aina ile kwenye eneo lile. Hakuna ubaya wowote kwenye hili, lakini kama biashara zote zinafanana kwa kila kitu, basi kuna tatizo kubwa.
Hiyo ni kwenye kuanzisha biashara, ambapo watu hawataki kuumiza kichwa.
Sasa kuna kuendeleza na kukuza biashara, wengi pia hawapendi kuumiza kichwa hapo. Hivyo wanachofanya ni kuangalia njia rahisi ni ipi.
Na wote hufikiria sehemu moja, kupunguza bei. Hakuna ubunifu wowote kwenye kupunguza bei kwenye biashara, na mbaya zaidi inapelekea biashara kufanyika kwa mazingira magumu zaidi.
Kwa sababu ni rahisi kufanya, na kwa sababu matokeo yanaweza yakaonekana haraka, japo siyo matokeo mazuri, wengi hukimbilia kufanya.
SOMA; Vitu Viwili Vinavyojenga Biashara Yenye Mafanikio.
Kudanganya wateja, kwa kutoa ahadi ambazo huwezi kutekeleza, au kuwapa watu kitu ambacho hakijakamilika, ni njia nyingine ya kutafuta urahisi kwenye biashara. Wengi wanafanya hivyo na wateja wanakuja mara moja na hawarudi tena.
Hivyo nataka nikukumbushe hapa rafiki, maamuzi yoyote unayotaka kufanya kwenye biashara yako, yasiwe rahisi. Isiwe tu umejiambia kwenye akili yako nikifanya hivi nitaongeza faida, au kuongeza wateja.
Badala yake kaa chini na yapime maamuzi unayofanya, iangalie biashara, jua kila eneo la biashara yako vizuri na jua maamuzi unayofanya yataathiri eneo gani la biashara yako. Angalia athari zake, chanya na hasi kwenye biashara, na ona kama kutakuwa na manufaa makubwa, hasa ya muda mrefu kwenye biashara yako.
Maamuzi mengi ambayo yanaleta matokeo ya haraka, mara nyingi huwa yanakuwa siyo bora, na kwa muda mrefu yanakuwa na madhara. Na maamuzi bora ambayo yana manufaa ya muda mrefu, mara nyingi matokeo yake huwa hayaonekani haraka.
Kama ni rahisi usifanye kwenye biashara yako, haina thamani na itakuletea madhara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
