Zipo changamoto nyingi za biashara, na kwenye kupata wateja zipo changamoto pia. Lakini ipo changamoto moja kubwa ambayo wafanyabiashara wengi, huwa hawaielewi. Hasa kwa wale wafanyabiashara wanaoanza, huwa hawaelewi changamoto hii kwa sababu bado wanakuwa hawajawaua wateja wa biashara zao.

Changamoto tunayokwenda kuigusia leo ni kuchagua wateja wa biashara yako. Kila mfanyabiashara, anapaswa kuchagua ni wateja wa aina gani ambao atawahudumia kwenye biashara yake, ili aweze kuwahudumia vizuri.

Hapa wengi hawaelewi, kwa sababu wamekuwa wakifikiri kwamba kila mtu ni mteja wa biashara yao. Hivyo hukazana kukimbizana na kila mtu, mwishowe wanachoka, wanaishia kuwa na wateja wasio wazuri huku wateja wazuri wakipotea.

Kwenye biashara, ukichagua wateja wazuri umeshinda, ukichagua wateja wasio wazuri, yaani wasiojali biashara yako, umeisha.

Kwenye biashara yako, unapaswa kuwahudumia wateja wazuri, watu wanaojali kuhusu biashara yako, watu wenye mahitaji ya kweli, na ambao wanategemea kuendelea kupata mahitaji hayo kwako. Hawa ni watu wanaiheshimu biashara na hata kuleta wateja zaidi.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Biashara Kubwa Ya Wateja Wanaolipa Fedha Taslimu Na Siyo Mikopo.

Lakini inapokutana na wateja ambao hawajali kuhusu biashara, ambao wanataka wao pekee ndiyo wapate kile wanachotaka, bila ya kujali biashara inaendaje, hapo unaiweka biashara kwenye matatizo.

Mwisho kabisa, kumbuka biashara ni yako, hivyo una uhuru wa kuijenga na kuwa bora kadiri ya uwezo wako, kazana kuwasaidia watu bora, na biashara yako itawavutia watu bora zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog