Moja ya sababu za biashara nyingi kudumaa, yaani biashara kuwa pale pale miaka nenda miaka rudi, ni wamiliki wa biashara hizo kuwa na malengo ambayo hayaendani na biashara zao.

Labda malengo yanakuwa madogo sana, kiasi kwamba wanayafikia bila ya kuhitaji juhudi za ziada. Kwa mfano kama unataka biashara ikupe hela ya kula, hutakesha ukifikiria kitu gani kikubwa cha kufanya. Kuwepo kwenye biashara muda mchache tu kunakutosha kupata hela ya kula. Unaweza kuamua kufungua muda wowote na kufunga muda wowote, hasa pale unapokuwa umeshapata hela ya kula.

Wakati mwingine malengo yanakuwa makubwa sana, kiasi kwamba mfanyabiashara anapoyaangalia malengo hayo, haoni ni kwa namna gani anaweza kuyafikia. Yanakuwa makubwa kiasi kwamba mtu anakata tamaa kabisa hata kujaribu. Malengo haya yanakosa hatua ndogo za kuanza kuchukua na hivyo mtu anashindwa kujua aanzie wapi.

Unapaswa kuweka malengo ya kibiashara, ambayo yatakuonesha hatua unazoweza kuchukua, lakini pia yatakusukuma sana. Malengo hayo yanakuwa wazi na kwa mpangilio mzuri kiasi kwamba unajua hatua ipi ya kupiga na wapi unaelekea.

SOMA; Ni Bora Kuweka Malengo Makubwa Na Kushindwa Kuliko Kuweka Malengo Madogo Na Kushinda.

Kwa mfano unapokuwa na lengo la kuongeza kipato kwenye biashara yako, usijiambie unataka tu kuongeza kipato, hilo litakuwa lengo dogo na halitakusukuma, kwani ukiongeza elfu moja umeongeza kipato. Pia usijiambie unataka kuongeza bilioni, hapo utapata wasiwasi wewe mwenyewe.

Njia nzuri ni kujiambia unataka kuongeza kipato chako mara mbili ya ulichonacho sasa. Hapo unajua wapi ulipo na hatua zipi za kuanza kufanyia kazi. Mfano kuongeza wateja mara mbili ya ulionao sasa, kuongeza bidhaa au huduma zaidi ya ulizonazo sasa, kuwauzia wateja zaidi ya unavyowauzia sasa na kadhalika. Kwa njia hiyo utaweza kupiga hatua kwenye biashara yako. Na ukifikia lengo hilo, unaweza kurudia tena, kwa kufikia mara mbili ya kile ulichofikia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog