Mambo Kumi (10) Usiyojua Kuhusu Tajiri Mpya Namba Moja Duniani (Jeff Bezos).

Jana ulimwengu wa biashara na fedha ulikuwa na habari kuu moja ya ujio wa tajiri namba moja duniani. Jeff Bezos alifanikiwa kumpiku tajiri namba moja wa muda mrefu Bill Gates baada ya thamani ya utajiri wake kufikia dola bilioni 90.08. Hizi zimekuwa habari mpya na za kushangaza kwa wengi kwa kuwa ni jambo ambalo wengi hawakulitegemea.

Rafiki yangu mmoja aliniandikia jana akitaka kujua huyu Bezos hasa ni nani na amewezaje kumpiku mtu tajiri duniani Bill Gates. Hapa ndipo niligundua wapo wengi huenda hawajawahi kumsikia au kumjua kwa undani Jeff Bezos. Nimekuandalia makala hii yenye mambo kumi muhimu ambayo huenda huyajui kuhusu tajiri huyu mpya namba moja duniani. Yapo mengi ya kujifunza kupitia maisha yake.

1. Utoto wake ulikuwa na changamoto.

Mama yake mzazi alipata mimba akiwa shuleni, baadaye aliolewa na aliyempa mimba lakini waliachana kutokana na maisha kuwa magumu na mwanaume kuwa mlevi. Baadaye aliolewa na mwanaume mwingine ambaye alimchukulia Jeff kama mtoto wake wa kumzaa. Mpaka anafikisha miaka 10, hakuwa anajua anayemlea siyo baba yake mzazi.

SOMO; Haijalishi umepitia maisha magumu kiasi gani, bado una uwezo wa kufanya makubwa kwenye maisha yako. Usiangalie sana ulikotoka, bali angalia unakotaka kufika.

2. Biashara yako kuu ni Amazon.

Bezos ni mwanzilishi wa mtandao mkubwa wa kuuza vitu wa Amazon. Ni mtandao ambao ulianza kwa kuuza vitabu, ila kwa sasa unauza kila kitu. Mtandao huu ulianza tangu mwaka 1994 na umekuwa unakua kwa kasi kubwa kila mwaka. Kampuni hii aliianzia nyumbani kwake alipokuwa anaishi.

SOMO; Kuanza kidogo haimaanishi utaendelea kuwa hapo, kuwa na ndoto kubwa lakini anzia chini na endelea kukua.

3. Amewahi kuwa mhudumu wa mgahawa.

Wakiwa kijana mdogo, Bezos amewahi kuwa mhudumu wa mgahawa wa McDonald’s, akiwa kama mhudumu na msafishaji wa meza. Anasema kazi hii ilimpa msingi muhimu sana wa kubeba majukumu yake.

SOMO; Kama huna pa kuanzia, anzia chini kabisa, jifunze kwa kila unachofanya na kuwa na ndoto kubwa zaidi ya ulipo sasa.

4. Aliacha kazi inayolipa kwenda kujiajiri.

Kabla ya kuanzisha Amazon, Bezos alikuwa ameshaajiriwa sehemu tatu, Fitel, Bankers Trust Company na D.E. Shaw, zote zikiwa kampuni zinazohusika na fedha na uwekezaji. Katika kampuni ya tatu, aliweza kupanda vyeo mpaka kufikia nafasi ya makamu wa raisi wa kampuni hiyo, tena katika umri mdogo sana. Wakati anaacha kazi yake na kwenda kujiajiri, kila mtu alimwambia anafanya kosa kubwa ambalo atajutia maisha yake yote.

SOMO; Unapokuwa na ndoto kubwa, ifanyie kazi, hata kama kila mtu yupo kinyume na wewe.

5. Wakati anaanzisha Amazon hakuwa na uhakika wa anafanya nini.

Kabla ya kampuni yake kuitwa Amazon, aliita cadabra, baadaye akaona jina siyo zuri, akaiita Relentless, nalo akaona halifai. Baadaye ndiyo aliamua kuchagua Amazo, jina la mto mrefu zaidi, akiwa na maono ya kampuni kuwa kubwa zaidi.

SOMO; watu wengi wamekuwa wanashindwa kuingia kwenye biashara kwa sababu wanajiona hawajawa na wazo kamili. Ni bora kuanza, utaendelea kurekebisha wazo lako kadiri unavyokwenda.

6. Amewekeza kwenye makampuni mengine zaidi ya 40.

Bezos amekuw amwekezaji mkubwa kwenye makampuni mengine kama google, twitter, uber, Airbnb n.k. alikuwa mwekezaji wa kwanza kabisa kuwekeza kwenye kampuni ya google kabla hata haijajulikana, aliwekeza dola 250,000 mwaka 1998. Wakati huo hisa moja ya google ilikuwa dola 0.04. Sasa hivi hisa moja ya google ina thamani ya dola 966. Hii ina maana kama hakuuza hisa zake, dola laki mbili na nusu aliyowekeza mwaka 1998, sasa hivi imefikia dola bilioni sita.

SOMO; Uwekezaji unakuwezesha kutengeneza utajiri mkubwa bila ya kufanya kazi moja kwa moja, hasa pale unapochagua vizuri na kuwekeza mapema.

7. Ana mpango wa kuwaondoa binadamu duniani.

Lakini siyo kwa kuwaangamiza, bali kwa kuwawezesha kuishi kwenye sayari nyingine. Kupitia kampuni yake ya Blue Origin aliyoianzisha mwaka 2000, anataka watu kwenda sayari nyingine iwe rahisi na nafuu kama watu wanavyosafiri kwenda nchi nyingine.

SOMO; Upo uwezekano wa kufanya makubwa kuliko wengi walivyozoea, fikiria makubwa, hata kama hakuna mwingine anayeona hivyo.

8. Anaogopa kupanda helikopta.

Katika maisha yake, Bezos ameponea kifo mara mbili, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2001 ambapo tetemeko la ardhi lilitokea na kunusurika kuangukwa na chuma ambacho kingemuua. Mara ya pili ilikuwa mwaka 2003 ambapo helikopta aliyokuwa amepanda ilipata ajali mbaya. Tangu wakati huo amekuwa akiogopa kupanda helikopta

9. Ameshindwa mara nyingi.

Ni kawaida kusikia hadithi za mafanikio, lakini huwa hatupendi kusikia hadithi za kushindwa. Pamoja na kuweza kuwa tajiri namba moja duniani, Bezos pia ameshindwa kwenye mambo mengi.

Kwa mfano;

Mwaka 2000 alipoteza mamilioni ya dola kupitia uwekezaji ambao haukuwa na faida.

Mwaka 2004 uuzaji wa madini kupitia Amazon ulishindikana.

Mwaka 2014 alipoteza dola bilioni 6.3 kupitia kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni yake.

Ipo mipango na uwekezaji mwingi ambao amefanya na ukashindwa.

SOMO; Hakuna mafanikio bila ya kushindwa.

10. Kupanda kwa thamani ya hisa kunamfanya kuwa tajiri namba moja.

Bezos alianza mwaka huu 2017 akiwa katika nafasi ya nne ya utajiri duniani. Lakini imemchukua muda mfupi kufika namba moja baada ya hisa za kampuni yake ya Amazon kupanda thamani kwa silimia 40. Yaani alilala akiwa na utajiri wa dola bilioni 80 na, akaamka asubuhi akiwa na utajiri wa dola bilioni 90.

SOMO; zile hadithi za kulala masikini na kuamka tajiri, ni za kweli kabisa, ila itakuchukua miaka zaidi ya 20 ya kufanya kazi mpaka ufikie hatua hiyo.

Naamini kwa mambo hayo kumi, utaweza kujifunza na kuchukua hatua. Siyo lazima uwe bilionea, na wala siyo lazima uwe tajiri namba moja duniani, ila unapofanya makubwa na kuboresha kipato chako, maisha yako na ya wanaokuzunguka yanakuwa bora.

NYONGEZA; Nafasi yake ya tajiri namba moja imedumu kwa masaa.

Nafasi ya Bezos kuwa tajiri namba moja duniani ilidumu kwa muda mfupi baada ya thamani za hisa zake kushuka. Hii ilipelekea kuwa mtu tajiri namba mbili duniani, namba moja akiwa Bill Gates.

Nikutakie kila la kheri rafiki yangu,

Endelea kupambana.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

One thought on “Mambo Kumi (10) Usiyojua Kuhusu Tajiri Mpya Namba Moja Duniani (Jeff Bezos).

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: