MAKIRITA AMANI
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku mpya ya juma jipya ambapo ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambao unatuwezesha kupata matokeo bora sana leo.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MUDA NA PESA…
Ni mara nyingi sana tumekuwa tunasema muda ni pesa, kwamba ukipoteza muda umepoteza pesa.
Lakini je hilo ni kweli?
Kwa hakika hilo halina ukweli, na watu kutojua hili, wamepoteza muda mwingi na fedha pia.
Muda una ukomo wakati fedha haina ukomo. Kuna masaa 24 pekee kwa siku, huwezi kuongeza hata kidogo, lakini fedha hazina ukomo, unaweza kuongeza kadiri utakavyo.
Poteza fedha na utazipata tena, lakini poteza dakika moja pekee na imetoka hiyo, huji kuipata tena kwenye maisha yako.
Ukiwa huna fedha unaweza kukopa, lakini hakuna aliyewahi kufanikiwa kukopa muda, kwamba kwa sababu leo upo ‘bize’ sana, una mengi ya kufanya na muda huna, ukope masaa kadhaa ya kesho uyatumie leo na uje kuyalipa kesho. Hilo halipo!
Hivyo basi, ni dhahiri ya kwamba muda ni zaidi ya fedha, muda una thamani kubwa sana ambayo hatuwezi kuulinganisha na fedha.
Kwa kujua hili, kutatufanya tuuangalie muda kwa mtazamo mwingine kabisa.
Badala ya kuona tukipoteza muda tunapoteza fedha, tuone wazi ya kwamba tukipoteza muda tunapoteza zaidi ya fedha.
Kwa hakika, tunapopoteza muda, tunakuwa tumechagua kupoteza maisha.
Je upo tayari kupoteza sehemu ya maisha yako? Kama jibu ni hapana, linda muda wako sana leo na kila siku. Fanya yale muhimu na kuwa na vipaumbele.
Usipoteze hata dakika yako moja leo, pangilia muda wako vizuri na fuata mpango wako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.