MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine nzuri kwetu, nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambao utatuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.
Asubuhi ya leo tutafakari LEO KAMA JANA…
Leo naanza na swali lifuatalo…
Kama leo ungeishi kama jana, na ukaishi kila siku yako kama ulivyoishi jana, je ungefikia yale maisha ya ndoto zako?
Ungefika kweli kule ambapo unataka kufika, kwenye mafanikio?
Iwapo kila siku ya maisha yako, ungeiishi kama ulivyoishi jana, miaka 20 ijayo ungekuwa wapi?
Watu wengi wamekuwa hawajiulizi swali hili muhimu kwa kusahau kwamba siku moja ni kipimo kizuri sana cha mafanikio. Kwa sababu mafanikio makubwa kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku ambazo mtu ameziishi vizuri.
Siku moja ni kipimo kizuri sana iwapo unaelekea kwenye mafanikio au la. Hivyo jinsi unavyoziishi siku zako, ni kiashiria kizuri cha kule unakoelekea.
Kaa chini na utafakari jinsi unavyoziishi siku zako, jiulize kama kwa njia hiyo utaweza kufika kwenye mafanikio unayotaka kufika.
Iwapo unapoteza muda kila siku, kuna madhara makubwa unatengeneza kwenye maisha yako. Unaweza kuona muda unaopoteza ni mdogo kwa siku, lakini zinapokuwa siku nyingi, unakuwa umepoteza sehemu kubwa ya maisha yako.
Kazana sana kuimiliki siku yako, pambana na siku yako moja uende vizuri, uweze kufanya makubwa na kutumia muda wako vizuri. Ukiiweza siku yako moja na kila siku, hutakuwa na wasiwasi kuhusu mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kila mwisho wa siku tafakari, iwapo nitaishi kila siku kama nilivyoishi leo, maisha yangu yatakuwaje? Kama hayatakuwa unavyotaka yawe, badili kile ambacho hakipo sawa.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.