Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza hazina kubwa kuliko zote duniani. Je unaijua ni hazina gani hiyo? Karibu tujifunze

Dunia ni watu na vitu vyote vinavyotafutwa vinapatikana kwa watu. Na hata mafanikio tunayotafuta pia yanapatikana katika watu. Kuna wale wanasema kuwa wao ni jeshi la mtu mmoja kauli kama hii ni ya uongo kabisa hata ukisema wewe jeshi la mtu mmoja bado utahitaji watu wakusaidie.

Tunasahau ya kuwa kujitegemea siyo kujitosheleza kwa kila kitu. yule mtu ambaye anadharau watu basi hataki kufanikwa tena. Mafanikio makubwa hapa duniani ni kuwa na mahusiano mazuri na rasilimali watu.

Mpendwa msomaji, hazina kubwa kuliko hazina zote hapa duniani ni watu. Watu ndiyo hazina katika maisha yetu. Watu ndiyo biashara zetu, watu ndiyo kazi zetu watu ndiyo hazina katika maisha ya watu. Hata leo huduma unayotoa unategemea watu ili iweze kuwa na uhai wa kuendelea kuwepo. Kama tunavyosema biashara ni wateja vivyo hivyo maisha ya binadamu ni watu.

Chochote unachotaka katika hii dunia utakipata kwa watu. Watu ndiyo wanaijua dunia na watu ndiyo wanaifanya dunia kuwa sehemu bora lakini salama kuishi kwa kila mmoja. 

Ukipoteza watu umepoteza mafanikio makubwa.

Rafiki, haijalishi una kipato kikubwa ua kidogo lakini katika swala kuwa na mahusiano mazuri na watu ni la kila mtu. Na kadiri unajuana na watu wengi ndivyo utakavyofanikiwa, kama huna mtandao mkubwa watu unakuwa unajiwekea mipaka mwenyewe ya kufanikiwa. Watu ndiyo huamua juu ya vile tunavyofanya kwani watu ndiyo rasilimali au kiini cha mafanikio yetu hapa duniani.

Tunaalikwa kuwajali watu na kushirikiana nao vizuri. Mahusiano bora yaliyojaa uaminifu ndiyo nguzo ya watu. Niliwahi kuandika kuwa ishi maisha yako lakini usisahau kuishi vizuri na jamii inayokuzunguka. Ukitaka kukosea kuwa na mahusiano mabovu na watu, hata kama unauza kitu unategemea watu ndiyo waje wanunue na bila watu hakuna dunia.

Watu ndiyo wanafanya hii dunia iendelee kuwepo. Jenga urafiki na watu chanya na ambatana nao na tanua wigo wa watu katika maisha yako. kikomo cha kuwa na mtandao wa watu wa chache ndiyo kikomo cha mafanikio yako. watu wengi mafanikio mengi.

Hatua ya kuchukua leo, hazina kubwa kuliko zote ni watu. Je unawapenda watu na kuwajali? Unagusa maisha ya watu na kuyafanya kuwa bora? Una mahusiano bora na ndugu, jamaa, marafiki na jamii iliyokuzunguka? Mafanikio ya mtu yanatoka katika watu hivyo ni vema kuheshimu hazina hii muhimu. Kila mtu ana sababu ya kipekee katika maisha yako hivyo ni muhimu kulitambua hilo.

Kwa kuhitimisha, watu ndiyo dunia wanayofanya izidi kukua. Je kama wewe ni sehemu ya dunia unafanya nini kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa kila mmoja. Kama umepokea tokea unazaliwa je umefikiria kutoa kwa dunia pia ili nayo ifaidike na wewe? 

Ukiishi na watu vizuri utaweza kuifurahia dunia lakini vinginevyo utateseka tu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi. Asante sana.