MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine nzuri sana ya leo ambapo tumepata nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KAZI NZURI NA ISIYOCHOSHA…
Katika kazi moja, ambapo watu wanalipwa sawa na majukumu yao yanafanana, yupo mfanyakazi mmoja anakuwa anaona kazi hiyo kama mzigo na anafurahi kweli muda wa kazi unapoisha. Jumatatu anakuwa na simanzi kubwa, huku ijumaa akiwa na furaha ya hali ya juu. Kwenye kazi hiyo hiyo unakutana na mfanyakazi mwingine ambaye ana hamasa kubwa kwenye kazi hiyo, anatamani hata kuendelea kuifanya licha ya muda kuisha. Jumatatu inapofika anakuwa na hamasa ya kuanza kazi.
Tofauti hii kwenye kazi, haitokani na kazi yenyewe, bali inatokana na wafanyakazi. Uwezo wa mtu na mtazamo wake, unachangia kazi kuwa nzuri na rahisi kwake au kuwa ngumu na mbaya kwake.
Kazi nzuri na rahisi kwako, ni ile ambayo inakuhitaji wewe kutumia uwezo wa kipekee ulipo ndani yako, ambao wengine hawana. Unakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo, kuliko wengine wanavyoifanya. Hili linakupelekea wewe kupata matokeo mazuri na matokeo hayo mazuri yanakuhamasisha kufanya vizuri zaidi.
Kama kazi haikuhitaji wewe kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, haitakuwa kazi nzuri kwako, hata kama malipo ni makubwa na majukumu ni rahisi.
Japokuwa kwa nje huwa tunaonekana tunapenda vitu rahisi, lakini kwa ndani tunapenda changamoto. Tunapenda kitu cha kutusukuma, ili tufanye zaidi ya tulivyozoea.
Hivyo unapopata kile ambacho kinakusukuma kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, utakipenda na kukithamini zaidi.
Ni muhimu ujue uwezo mkubwa uliopo ndani yako ni upi na jinsi gani unaweza kuutumia kwenye kazi na mambo yote unayoyafanya.
Ni makosa makubwa tunafanya kwenye jamii zetu, kurahisisha kila kitu ili kiweze kufanywa na kila mtu.
Ili kua bora na kuongeza thamani yako, lazima uweze kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, kufanya mambo ya tofauti na wengine wanavyofanya.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.