Habari za leo rafiki?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kuwa na maisha ya mafanikio. Changamoto ni nyingi, zipo zinazotokea kutokana na mazingira na pia zipo ambazo tunatengeneza sisi wenyewe, kwa kujua au kutokujua. Kwa vyovyote vile, tunapaswa kutatua changamoto zozote tunazokutana nazo ili kuweza kufanikiwa.Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya madeni na kipato kuwa kidogo. Hivyo tutaangalia ni jinsi gani mtu unaweza kuondoka kwenye madeni na kuweza kuongeza kipato chako ili kuondokana na changamoto za kifedha.

Kabla hatujaingia ndani na kuona hatua za kuchukua, tusome maoni ambayo msomaji mwenzetu ametuandikia;

Nashukuru kwenye makala ya leo uliyoonesha njia ya kuepukana na kujipa presha na wakopaji wasio waaminifu. Umetoa ushauri ambao nimewahi kuutumia, jirani alikopa kwangu sh.20,000/= akaanzisha meza ya nyanya, hajanirudishia pesa hadi sasa lakini ni kweli kuwa sasa haombi kitu kutoka kwangu tena.

Lakini kocha mimi nina tatizo kinyume na mwenzangu, mshahara wangu take home ni ndogo sana. Nilikopa kila nilipopata shida ya pesa hata iwe ndogo. Nimekopa crdb, abc banc, faidika na bayport. Tulitaraji mshahara kupanda tangu mwaka wa jana labda tungeongeza kipato, lakini hata mwaka huu hakuna nyongeza, maisha magumu kuishi kwa 1/3 ya mshahara. Nipe ushauri, nifanye nini kuondokana na madeni? – M. K. Masanja.

Kama ambavyo ametuandikia Bwana Masanja, wapo watu wengi ambao wamejikuta kwenye changamoto kubwa kifedha kwa kufanya makosa makubwa kama aliyofanya hapo juu.

Japo siyo lengo letu kujadili makosa hapa ila suluhisho, lakini ni vyema tukajikumbusha makosa ambayo amefanya na wengi wanaendelea kufanya, ili kuweza kuzuia changamoto hii kabla haijatengenezwa.

Hivyo Bwana Masanja na wengine wanaojikuta kwenye hali kama yake wanafanya makosa haya matatu makubwa ambayo yanawatengenezea changamoto kubwa mno.

1. Kuwa na chanzo kimoja pekee cha kipato ambacho ni mshahara, na kama ilivyo ukweli, mshahara haujawahi kumtosha mtu yeyote.

2. Kufunika moshi badala ya kuzima moto, baada ya mshahara kuwa hautoshi, wanachofanya siyo kutatua tatizo lao la fedha, bali kukopa, na hapo tatizo linakuwa kubwa zaidi.

3. Kupiga mahesabu ya hela ambayo bado hawajaipokea. Kama hapo unaona Masanja anasema alitegemea mshahara uongezwe. Kuweka matumaini kwenye kitu ambacho huwezi kudhibiti ni kutengeneza changamoto.

Katika kuhakikisha mtu anaondoka kwenye madeni na kuongeza kipato, nitakwenda kushauri mambo matano muhimu ambayo yanapaswa kufanywa kwa pamoja. Siyo hatua kwamba uanze moja ukikamilisha ndiyo uende mbili, badala yake unahitaji kufanya yote kwa pamoja.

1. Upo kwenye shimo, acha kuchimba.

Kwa hali ya kawaida tu ukishajikuta kwenye shimo, hatua muhimu unayopaswa kuchukua ni kuacha kuchimba mara moja. Lakini wengi wamekuwa wanakazana kuendelea kuchimba, kitu ambacho kinawadidimiza zaidi.

Ndiyo kama hivyo mtu ana matatizo ya kifedha, halafu anaenda kukopa fedha kuyatatua, hapo ina maana anaongeza matatizo zaidi, na siyo kuyapunguza.

Hivyo acha kukopa, acha kabisa, usiweke tena wazo la kukopa kwenye akili yako. Acha maisha yawe magumu, acha upitie mateso lakini usikimbilie kukopa. Kwa sababu kukopa kunakudanganya, kunakufanya uone mambo siyo mabaya sana, wakati ni mabaya mno. 

Acha kukopa na hata uwe na wakati mgumu kiasi gani, wazo la kukopa lisiingie kwenye akili yako.

2. Tangaza hali ya hatari, na panga upya maisha yako.

Kuna wakati mataifa huwa yanatangaza hali ya hatari, kutokana na sababu mbalimbali, inaweza kuwa njaa au vita. Katika hali hiyo ya hatari, maisha huwa yanabadilika kabisa, watu hawaendeshi maisha kama walivyozoea, watu wanafanya yale muhimu tu, yale yasiyo muhimu hayaruhusiwi kabisa.

Sasa unapokuwa kwenye madeni makubwa na kipato hakitoshelezi, ni wakati wa kutangaza hali ya hatari kifedha, na kupanga upya maisha yako. Hapa unahitaji kupitia matumizi yako yote, na kuangalia yapi ambayo ni ya msingi kabisa, ambayo usipoyapata maisha yatakuwa hatarini zaidi. Na hayo pekee ndiyo yanapata kipaumbele. Pia katika hayo muhimu, angalia njia rahisi zaidi ya kuyapata ili kuepuka gharama zisizo za msingi.

Hivyo katika hali hii ya hatari, utaushangaza umma kama utaendelea kutumia fedha kununua vinywaji kama soda au vileo, vitu ambavyo havina manufaa yoyote kwako. Au unanunua nguo, kuchangia kila harusi na kununua vitu ili tu kuonekana. Huu ni wakati wa kuweka matumizi yako chini kabisa, na kutumia muda mwingi kwenye kuzalisha zaidi.

3. Anza sasa, yaani leo hii kuwa na njia nyingine ya kipato.

Hili usikae chini na kujidanganya utapanga halafu uone unaanzia wapi, wewe huna anasa hiyo, upo kwenye hali ya hatari, unahitaji fedha na unazihitaji haraka ili kurudi kwenye maisha yako. Lakini hazitakuja haraka kama unavyotaka na ndiyo maana unahitaji kuanza leo hii.

Usianze kujiuliza uanze na nini au uanzie wapi, badala yake jiulize ni thamani gani unaweza kuongeza kwa wengine na wao wakakupa hata elfu moja tu. Elfu moja, ni kubwa, kwa sababu kwa sasa huna. Sasa kama utawapata watu kumi wa kukupa elfu moja, au watu 10 wa kukupa mia kila mmoja, ni hatua nzuri.

Anza na huduma au bidhaa yoyote ndogo unayoweza kuwapatia watu wanaoihitaji. Iwe ni eneo lako la kazi, pale unapoishi au eneo jingine. Kama kipo kitu unaweza kuwasaidia wengine kulingana na uzoefu na taaluma yako, watafute unaoweza kuwasaidia na anza kufanya hivyo. Kama kuna kitu watu wanahitaji lakini hawapati, au wanapata lakini hawaridhishwi, anza kukifanyia kazi.

Unachohitaji wewe ni mahali pa kuanza hata na mtu mmoja, na kuanza leo hii, kisha kusonga mbele zaidi. Najua wapo watu wengi ambao unaweza kuwasaidia kwa hapo ulipo, kulingana na mazingira yako, anza kuangalia kwa mtazamo chanya, utawaona.

4. Usichague cha kufanya, huna anasa hiyo kwa sasa.

Kama upo kwenye madeni makubwa, kipato chako hakitoshelezi, tafadhali usije ukaniambia kwamba kwa hadhi yako huwezi kufanya shughuli fulani. Hadhi ipi? Ya madeni na maisha magumu ambayo huna mpango wowote mbadala? Hapana, nakataa hiyo hadhi.

Na ninachokuambia rafiki yangu, usichague cha kufanya sasa, hasa kwenye hali yako ya hatari. Kumbuka haya ni maisha halisi, siyo maigizo. Unapaswa kuyaishi vile yalivyo, lazima utoke hapo ulipo na laima uanzie chini kabisa katika kutoka hapo.

Ukijidanganya na hadhi, utazidi kuumia, huku kukiwa hakuna anayejali sana kuhusu maisha yako.

5. Kila kipato unachoingiza sasa, kipangilie na kutenga mafungu kabla hujatumia.

Tatizo kubwa la watu inapokuja kwenye kipato ni moja, wakishapokea, wanawaza watumieje. Yaani mtu akishika tu fedha, akili inahama kabisa, anaanza kufikiria anunue nini na nini. Ni mpaka fedha ile unapoisha ndiyo wengi hurudiwa na akili zao na kuanza kuona kuna mambo muhimu zaidi wangeweza kufanya.

Sasa wewe unahitaji kubadili hili, kwanza unapopokea fedha yoyote ile, swala la kutumia lisiingie kabisa kwenye akili yako. Yaani ukishika fedha, futa kabisa mawazo ya unaitumiaje. Badala yake angalia unaelekea wapi kifedha.

Kwa sasa unahitaji kuwa na akiba ya kujilipa wewe mwenyewe kwanza na kuwa na dharura itakayokusaidia pale unapokutana na dharura ambayo hukutegemea.

Hivyo kila kipato unachopokea wakati huu, usikitumie, endelea kuwa kwenye hali ya hatari na kipato hicho peleka kwenye mfuko wa kujilipa wewe mwenyewe kwanza na kwenye mfuko wa dharura. Utahitaji kuwa na akaunti maalumu ambazo zinakuzuia kutumia fedha hizo kwa urahisi.

Sehemu pia ya kipato hicho irudi kukuza zaidi ile shughuli ambayo inakuingizia kipato.

Sehemu ya kipato chako pia unahitaji kuiweka kwenye fungu la kulipa madeni. Kama madeni uliyonayo yanalipwa kwa makato kwenye mshahara basi acha makato hayo yaendelee. Lakini kama unayalipa kwa fedha zako mwenyewe, basi tengeneza mfuko wa kulipa madeni na weka sehemu ya kipato kwenye mfuko huo. Anza kuwalipa wale wanaokudai, kulingana na kiasi unachodaiwa na ukali wa madeni hayo.

Haya ni mambo matano ya kuanza kufanya leo, ndiyo, namaanisha leo hii baada ya kusoma hapa, ili uweze kuondoka kwenye madeni na kuongeza kipato chako. Kama utajidanganya kwamba utaanza kesho, endelea kujidanganya. Kama utajishawishi kwamba kwa sasa hujajipanga utaanza ukijipanga, nikuambie tu umeridhika na hapo ulipo sasa.

Kama una hasira kweli, umechoka kuishi maisha yasiyo na mbele, umechoka na hali hiyo na huwezi kuvumilia tena, basi hatua ni sasa, hatua ni leo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog