Habari rafiki?
Hongera kwa siku hii nzuri na ya kipekee sana ambapo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi zaidi ili tuweze kupata matokeo bora kabisa.
Karibu kwenye makala ya leo ya NYEUSI NA NYEUPE ambapo nimekuwa nakuandikia kuhusu ukweli ambao watu tunachagua kutokuuangalia au tunauangalia halafu tunajifanya kama hatujauona.
Kwenye makala la leo nakwenda kuzungumzia kuhusu fedha, na tabia zetu kwenye fedha ambazo zinatutenganisha na fedha zetu jambo ambalo linachangia watu wengi kuwa masikini.
Lakini kabla sijaingia kwa undani kuhusu tabia hizo za kifedha, nakwenda kukupa mfano ambao utatuweka sawa, ili tuweze kujifunza kwa kina.
Mfano huu unatokana na kichekesho kimoja ambacho ni maarufu sana ma kichekesho hicho ni kama ifuatavyo;
Mtu mmoja alikuwa anaongea na rafiki yake ambaye anavuta sigara, akamwambia unajua hela ambayo unanunulia sigara ingeweza kukufanya kuwa tajiri mkubwa?
Mvutaji yule akamwambia ingewezaje?
Mtu yule akamuuliza, kwa siku unavuta pakiti ngapi za sigara? Mvutaji akamjibu navuta pakiti moja.
Akamuuliza tena, umevuta sigara kwa miaka mingapi sasa? Akamjibu miaka 20.
Akamwambia sasa piga mahesabu, pakiti moja ya sigara ni shilingi elfu 2 kwa mwezi ni shilingi elfu 60 kwa mwaka ni shilingi laki saba na elfu 20
Kwa miaka 20 ambayo umevuta, umepoteza shilingi milioni 14 na laki 4, kama fedha hii ungeiweka akiba au kuiwekeza, ungekuwa umepiga hatua kubwa sana.
Mvutaji yule akatafakari kwa kina jambo hilo, kisha akamuuliza mtu yule, wewe unavuta sigara? Akamjibu hapana, sivuti. Mvutaji akamuuliza, umeweka akiba kiasi gani na kiasi gani umewekeza kwenye miaka hiyo 20 ambayo hujavuta sigara na mimi nimevuta? Mtu yule hakujibu chochote, aliondoka.
Huu ni mfano, ambao umekuwa unatumika kama kichekesho, lakini umebeba funzo kubwa sana kuhusu fedha, ambalo nataka leo tujifunze kwa kina, ili uweze kuchukua hatua.
Ili miaka 10 au 20 ijayo, useme hii ndiyo ile hela ya sigara, hela ambayo wewe umeiokoa na wanaovuta sigara au wanaofanya chochote kisicho muhimu, wameipoteza.
Tuanze kuangalia ukweli, ambao huenda utakuumiza, lakini sitajali sana, kwa sababu ukweli haujifichi.
Ukweli ni kwamba, kila mtu anapoteza fedha. Ndiyo, wewe hapo unapoteza fedha, na unafanya hivyo kila siku.
Najua utashangaa na kuanza kubisha, kwamba upotezeje fedha wakati kipato chenyewe hakikutoshi, mishahara haikutani, una madeni mengi, kama kuna kitu uko makini nacho basi ni fedha. Sasa nataka kukuambia kwamba, haupo makini na fedha kama unavyofikiri.
Huenda pia huna kazi, huna shughuli yoyote inayokuingizia kipato, halafu nakuambia kwamba unapoteza fedha, huelewi kabisa.
Bado naendelea kukuambia kwamba, unapoteza fedha, bila ya kujali ulipo na hali uliyonayo, unapoteza fedha.
Na fedha unayopoteza, ni manunuzi yoyote yale ambayo unafanya, ambayo hata usingefanya kusingekuwa na hatari yoyote kwenye maisha yako, yaani kama ungeacha kununua, usingekufa.
Hivyo chochote unachonunua, hata kama unaona ni muhimu kiasi gani, kama usiponunua hutakufa, basi umepoteza fedha.
Kwa mfano, kama umewahi kununua soda kwenye maisha yako, umechagua kupoteza fedha, ni nani amewahi kufa kwa sababu hajanywa soda?
Kama umewahi kununua kilevi chochote kwenye maisha yako, umechagua kupoteza fedha, nani amewahi kufa kwa sababu hajapata kilevi? Labda kama ameshakuwa mteja, kitu ambacho ametengeneza yeye mwenyewe.
Kama umewahi kutoa fedha kununua maji ya kunywa ya chupa, umechagua kupoteza fedha, maji yanapatikana kwa asili kabisa, ungeweza kutafuta maji kwa njia za kawaida, ukayafanya kuwa safi na salama na ukaweza kuyanywa, bila ya kuingia gharama kubwa.
Sasa hayo ni maeneo machache sana ambayo nimeyagusia ambayo unapoteza fedha, lakini yapo mengi na makubwa zaidi, hilo nitaliacha liwe jukumu lako, la kuangalia kila eneo unalopoteza fedha.
Kwa mfano mkopo wowote ambao umewahi kuchukua na unalipa kwa riba, halafu mkopo huo hauzalishi faida, umechagua kupoteza fedha.
Nguo yoyote ambayo umewahi kununua, kwa sababu tu umekutana na muuza nguo na ghafla ukaipenda, umechagua kupoteza fedha.
Vifurushi mbalimbali unavyolipia, kuanzia kwenye simu, programu za tv na kadhalika, kote ni kuchagua kupoteza fedha.
Endelea mwenyewe kuangalia kila aina ya matumizi unayofanya, unayoamini ni muhimu kabisa, na uangalie je usingefanya hayo matumizi, maisha yangefika tamati? Kama jibu ni hapana, basi umechagua kupoteza fedha hiyo.
SOMA; USHAURI; Hatua Muhimu Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Madeni Na Kuongeza Kipato Chako.
Lakini mtu anapaswa kuwa na maisha bwana!
Nakubaliana na wewe, unapaswa kuwa na maisha, huwezi kuwa upo tu, hujiburudishi, huvai nguo nzuri, huli vyakula vizuri kwa sababu unaepuka kupoteza fedha.
Lakini ninachosema hapa ni kwamba, watu wengi wanapoteza fedha, kwa vitu ambavyo hata hawajali. Yaani mtu anaweza kuwa ananunua kitu, wala asijue kwa nini ananunua.
Watu wengi tumelelewa na kutengenezwa kama mashine za matumizi, yaani fedha ikishatua tu kwenye mikono yako, unaanza kufikiria ununue nini. Wapo watu mpaka wanasema kwamba wakipata fedha akili zao hazitulii mpaka ile fedha iishe.
Hivyo yale mambo muhimu kwa maisha yako yafanye, lakini yafanye kwa kiasi, kulingana na uwezo wako wa kifedha. Usijilazimishe kufanya jambo ambalo kipo nje ya uwezo wako, kila kitu kinaweza kusubiri, hata kama unafikiri ni muhimu kiasi gani.
Chagua sigara yako kwenye maisha, kisha hesabu fedha yake kwa miaka 20 ijayo.
Lengo langu kwenye makala ya leo, ni kukuwezesha wewe kutambua na kuchagua sigara yako kwenye maisha, ambayo utaacha kuivuta, halafu kuhakikisha hela yake unaiona, na unajua inaenda wapi.
Kwenye maisha yako, chagua kitu ambacho umekuwa unaingia gharama kila siku, lakini siyo muhimu sana kwako, halafu chagua kuacha kununua kitu hicho kila siku, ila ile fedha ambayo ulikuwa unanunulia, usiitumie kwa jambo jingine lolote.
Kama umekuwa unavuta sigara, amua kuacha kununua sigara, na ile fedha ikusanye kila siku na kila wiki.
Kama umekuwa unakunywa pombe, acha kununua pombe na fedha ile iweke kila siku.
Kama umekuwa unanunua maji ya kunywa kila siku, tengeneza utaratibu wa kuwa na maji ya kunywa na ile fedha unayotumia kununua maji ikusanye.
Kama kila ukikutana na wauza vitu vidogo vidogo unanunua, acha kununua, na fedha hiyo unaiweka pembeni.
Je fedha hiyo unaipeleka wapi?
Hapa sasa ndipo unapaswa kujitofautisha na yule ambaye havuti sigara lakini hawezi kuonesha ule utajiri anaompigia mtu anayevuta sigara. Kwa sababu fedha ina tabia moja, ukiwa nayo haikosi matumizi. Hivyo unahitaji kutengeneza mfumo wa kutokuwa na fedha ile uliyoiokoa. Badala yake iweke mbali na wewe kabisa.
Na kwa kuwa unakusanya fedha ndogo ndogo ambazo unaziokoa kwenye matumizi yako madogo madogo, usikae nazo, kwa sababu utazitumia kwa urahisi sana.
Zifuatazo ni njia ninazokushauri uzitumie kuhakikisha fedha hizo ndogo ndogo unaziweka mahali ambapo unaweza kuziona na kuziwekeza zaidi.
- Fungua akaunti ya uwekezaji kupitia UTT.
UTT ni mpango wa uwekezaji wa pamoja, ambapo unaweza kuwekeza kwa kununua vipande. Uwekezaji huu ni rahisi na unaweza kuwekeza kiasi kidogo sana cha fedha, kuanzia elfu tano, kumi na kuendelea.
Unachohitaji kufanya ni kupiga ile fedha unayookoa kwa siku ni kasi gani, kisha zidisha kwa wiki, na kile kiwango unachopata, hakikisha kila wiki unakiwekeza. Hivyo ikifika mwisho wa wiki, wekeza kiasi cha fedha ambacho umeokoa kwa wiki nzima. Unaweza kuwekeza kwa kutuma fedha kwa njia za simu.
Kujua zaidi kuhusu UTT na mawasiliano yao, tembelea www.uttamis.co.tz
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
- Fungua akaunti maalumu ya kuweka fedha hizo unazookoa.
Unaweza kufungua akaunti benki, tofauti na akaunti yako ya kawaida ya akiba. Akaunti hii iwe unaweka fedha pekee, lakini hutoi. Hivyo usiombe ATM kadi wala usiombe huduma za simu za kibenki, wewe unaweka tu, ukitaka kutoa basi uende ndani ya benki.
Kama kiasi unachookoa ni zaidi ya elfu 50 kwa mwezi, kuna benki zina akaunti nzuri, zenye riba kubwa ambapo kila mwezi unapaswa kuweka siyo chini ya elfu 50, na huruhusiwi kutoa mpaka miaka mitatu ipite. Unaweza kutembelea benki za CRDB, NMB, NBC na nyingine, kila benki ina mfumo wa aina hiyo wa akaunti.
- Weka akiba kwenye huduma za kifedha za simu.
Unaweza kuchukua fedha ile unayookoa na kuiweka kwenye huduma za kifedha za simu, labda MPESA, TIGO PESA na mitandao mingine. Lakini ili kufanya iwe vigumu kuitoa na kuitumia, nakushauri usajili namba mpya, kisha kwenye kuweka namba ya siri, chagua mtu unayemwamini ambayo ataweka sehemu ya namba ya siri. Yaani kwa kuwa namba ya siri ni tarakimu nne, wewe unaweka tarakimu mbili, na yeye anaweka tarakimu mbili, lakini kila mtu asimwambie mwenzake tarakimu alizoweka. Hapo sasa wewe utakuwa unaweka fedha zako na huzitoi. Kama una namba unayotumia sasa, unaweza kubadili namba ya siri kwa mpango huo wa kutafuta mtu wa kuweka nusu ya namba ya siri, ili isiwe rahisi kwako kutoa fedha hiyo.
- Tengeneza kibubu.
Ipo njia ya asili ambayo zamani ilitumika kuweka fedha, ambayo ni kuwa a kisanduku kidogo maarufu kama kibubu na kuweka fedha zako. Unaweza kutumia njia hii, lakini sishauri sana, maana siyo salama. Unaweza kuwa unaweka kwa muda, labda unaweka kila siku, halafu mwisho wa mwezi unazitoa na kupeleka benki. Ili kuepuka kuvunja na kutengeneza kila mara, unaweza kutengeneza cha chuma, ambacho kina sehemu ya kufunga na kufuli, ukafunga na kumkabidhi funguo mtu unayemwamini, lakini ambaye hajui kibubu kipo wapi, ni vyema akawa anaishi sehemu tofauti na wewe, akawa anakupa ufunguo mwisho wa mwezi tu.
- Vikundi vingine vya kuwekeza vyenye malengo mazuri.
Fedha unazookoa pia unaweza kuziwekeza kwenye vikundi vingine vya uwekezaji ambavyo vina malengo mazuri, vikundi hivyo vinaweza kuwa kama SACCOSS, na jumuia nyingine zinazoendeshwa vizuri. Usijiunge kwenye vikundi vya kukusanya hela na kurudishiana, au vicoba visivyo na mpango mzuri.
Muhimu sana kwenye yote haya, lazima ujenge nidhamu ya kutokutumia fedha kwenye kile ulichoacha kufanya, na pia lazima ujenge nidhamu ya kuwekeza fedha ile uliyookoa na siyo kuitumia kwa matumizi mengine.
Je ni sigara gani unachagua kuacha kuvuta? Ni kitu gani umekuwa unaingia gharama kila siku, ambacho unaweza kuacha na kuokoa fedha hiyo? nijibu kwa kuweka maoni yako hapo chini nione hatua unazokwenda kuchukua. Karibu sana uchukue hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog