Kila mtu kuna vitu vingi ambavyo anataka kwenye maisha yake. Ili maisha yaweze kwenda vizuri, na kuwa bora, kuna vitu vingi ambavyo tunavihitaji, kuanzia kwetu wenyewe na kwa wengine pia.

Lakini pia kila mtu kuna kitu kikubwa anachokitaka kwenye maisha yake. Hiki ni kitu kikuu, ambacho mtu anapambana kukipata. Kitu ambacho anakifikiria kwa muda mwingi wa maisha yake. Ambacho anajua akikipata basi maisha yake yanakuwa yamekamilika.

Ni watu wachache sana ambao wanaonekana kuweza kupata kile kikubwa wanachokitaka. Huku wengi wakihangaika maisha yao yote wasikipate, na mwishoni kupata msongo wa mawazo na kuona maisha yao hayakuwa na maana.

Zipo sababu nyingi sana zinazowazuia watu kupata chochote wanachotaka, sababu zinazoanzia ndani yao binafsi na sababu nyingine za kimazingira.

Lakini ipo sababu kubwa moja ambayo ndiyo imebeba sababu nyingine zote zinazopelekea mtu kukosa kile anachotaka. Na sababu hii wengi huwa hawaijui, na wala hawajui kama ipo ndani yao.

Hii ndiyo sababu ambayo tunakwenda kuijadili kwa kina leo, na tuweze kuona njia sahihi za kuiondoa kabisa sababu hii ili iache kuwa kikwazo kwetu.

Sababu kubwa ambayo inawazuia watu kupata kile hasa wanachotaka kwenye maisha yao ni KUKOSA UHALISIA.

kuwa wewe

Watu wengi wanataka makubwa kwenye maisha yao, lakini wanakosa uhalisia. Wanachoishi na wanachotaka ni vitu viwili tofauti. Mawazo yao yanawaza kitu kingine huku matendo yao yakifanya kitu kingine. Kwa kifupi, ukichukua mawazo na matendo yao, hayashabihiani, na wala hayaonekani kuweza kuleta kitu kimoja.

Hali hii inaleta mkanganyiko ndani ya nafsi ya mtu na ndiyo chanzo kikuu cha msongo na hata kujiona hakuna kikubwa ambacho mtu amefanya.

Watu wengi wanaishi maisha ambayo siyo uhalisia wao. Wanafanya hivi kwa sababu wanataka kuonekana kwa namna fulani kwa wengine, au wanataka kuwafurahisha watu fulani, au hawataki kuonekana kama wanaanzia chini. Na hili limewatesa na kuharibu watu wengi.

Kwa sababu kwa nje unaweza kuwadanganya watu, kwa nje unaweza kutengeneza picha ambayo watu watafikiri upo namna fulani. Lakini kwa ndani huwezi kujidanganya. Wewe pekee ndiye utakayeishi na wewe wakati wowote. Mchana utawadanganya watu lakini usiku unapolala, utalala na wewe, na utajisuta na kujiumiza kwa namna unavyoishi maisha ambayo hayaendani na kile unachotaka.

Wakati mwingine watu wamekuwa wakikwepa hali hiyo ya kukutana na wao wenyewe pale wanapojisuta kwa kutokufanya kile hasa ambacho wanataka kufanya. Lakini wao wamekuwa wakizuia hali hiyo kutokea kwa kuhakikisha wanajisumbua ili wasipate muda wa kuona kile ambacho wanakosa. Wanaweza kufanya hivyo kwa kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kusoma magazeti, kuangalia tv au hata kutumia vilevi.

Lakini hili haliondoi uhalisia ambao mtu ameacha kuuishi, badala yake unasogeza tatizo mbele na kulifanya kuwa kubwa zaidi. Kadiri mtu anavyozidi kupoteza muda kwa kukwepa kufanya kile hasa anachotaka, ndivyo anavyozidi kutengeneza tatizo kubwa.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Hii Ndiyo Ile Hela Ya Sigara (Jinsi Unavyoweza Kuweka Akiba Kidogo Kidogo Mpaka Kufikia Utajiri).

Ushauri muhimu kwako rafiki yangu ni huu, kama umeshajua kipi ambacho unakitaka hasa kwenye maisha yako, kama una ndoto kubwa za maisha yako unataka yafike wapi, usijidanganye wala kupoteza muda wako kukwepa ndoto hizo. Badala yake anza kuziishi. Acha kabisa kufanya mambo ili kuwafurahisha wengine, au ili ukubalike na wengine. Fanya kile ambacho ni sahihi kwako, na jua kwamba kilicho sahihi kwako hakiwezi kuwa sahihi kwa kila mtu.

Na kama bado hujajua kipi hasa unachotaka, kama umekuwa unaenda na maisha kama upepo, unagusa hiki unaacha na kugusa kingine unaacha, ni wakati umefika sasa ukae chini na kujifanyia tathmini, kuangalia ni kipi hasa unataka kwenye maisha yako, alama gani unataka kuiacha hapa duniani. Na kama ungekuwa na muda mchache wa kuendelea na maisha hapa duniani, ambao unao, je kipi muhimu zaidi ungekipa kipaumbele kwenye maisha yako.

Ukishajua unachokitaka kwenye maisha yako, anza kukiishi, kufanya kingine cha tofauti ni kuchagua kupoteza maisha yako, kitu ambacho utakijutia sana baadaye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

MIMI NI MSHINDI