MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WATU-SUMU…
Tuanze kwa kujikumbusha haya muhimu sana….
Je umewahi kuwa na wazo fulani zuri sana ambalo unaona kabisa linakwenda kuyabadili maisha yako, ukamshirikisha mtu ambaye ni wa karibu kwako na unayemwamini sana, lakini baada ya mazungumzo na mtu huyo ukajikuta unaachana kabisa na wazo hilo? Unatoka pale hamasa yote ikiwa imeisha, ukiwa umekata tamaa na kuona haiwezekani kama ulivyopanga?
Je yupo mtu ambaye kila ukikutana naye, unaondoka ukiwa na hofu, ukiwa umekata tamaa, na kuona mambo yanakwenda kuwa mabaya zaidi.
Hawa ndiyo watu ambao tunawaita WATU-SUMU.
WATU-SUMU ni watu ambao wanaona kosa kwenye kila kitu kizuri kinachofanywa na wanaona changamoto kwenye kila fursa. Hawa ni watu ambao huwa hawakosi baya la kuongea kwenye kitu chochote. Na huwa na ushahidi mkubwa sana wa kutetea kile wanachosema.
Watu hawa ni hatari sana kwenye maisha ya wengine, pia ni hatari kwenye maisha yao. Ni watu ambao ukiwachunguza kwa karibu unagundua wao wenyewe hakuna makubwa wanayofanya, hivyo wanahakikisha wengine nao hawafanyi. Kutimiza hilo wanafanya kazi ya kusambaza sumu kwenye kila jambo.
Wajue watu hawa kwenye maisha yako na waepuke haraka sana. Hata kama ni watu wa karibu, chagua sana ni mambo gani unawashirikisha, hasa wakati ambao ndiyo unaanza.
Epuka sana watu wote ambao wanaona mabaya pekee kwenye kila jambo. Watu ambao hawawezi kukushauri vizuri halafu wanakuwa na nguvu kubwa ya kukuambia nini ufanye au usifanye.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.