Kila mtu anapaswa kuwa kiongozi kwenye maisha yake. Hii ni kauli ambayo watu wengi wamekuwa hawaielewi kwa sababu mtazamo wao linapokuja swala la uongozi basi ni wale watu ambao wamechaguliwa au kuteuliwa kuongoza watu au kitu fulani.



Hivyo wengi wanaposikia kiongozi, moja kwa moja wanafikiria maraisi, mawaziri, wabunge, madiwani, viongozi wa makampuni, viongozi wa dini na kadhalika. Lakini wanasahau kwamba kila mmoja wetu ana fursa ya uongozi kwenye maisha yake, kuanzia kuongoza maisha yako mwenyewe, maisha ya familia, kikundi cha watu na nafasi nyingine nyingi.

Kwa kifupi, huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote kama hutakuwa kiongozi mzuri, kuanzia kwenye familia, kazi na hata biashara.

Kwa mfano, ili biashara iweze kufanikiwa, itahusisha watu wengi, kuanzia wafanyakazi, washirika na hata wateja. Kuweza kwenda vizuri na watu wote hao, lazima biashara iwe na uongozi mzuri.

Kiongozi anabeba maono, kiongozi anatoa hamasa na matumaini kwa wengine, kwa kuwaonesha kitu ambacho hawakioni na kuwapa matumaini kwamba inawezekana kukifikia.

Ni katika jukumu hili kubwa la uongozi, ndipo changamoto kubwa ya uongozi inapotokea.

Changamoto kubwa kabisa ya uongozi ni kwamba UTAPINGWA NA KUKOSOLEWA.

Haijalishi utafanya kitu kizuri na kikubwa kiasi gani, wapo watu ambao hawatakosa cha kukupinga na kukukosoa.

Utakuwa na watu ambao wataona mabaya kwenye kila unachofanya au kusema.

Utakuwa na watu ambao watakuwa na wasiwasi juu ya kile unachofanya.

Na mbaya zaidi, wapo ambao watakusingizia mambo ya uongo, watakutabiria mambo ambayo hata hujapanga kufanya.

Ni mambo ya kusikitisha na kuumiza, lakini ndiyo sehemu ya uongozi.

Lazima ujiandae sana kwa hayo, kwa sababu bila hivyo, unaweza kukata tamaa mapema, au kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri kwako na hata kwa wengine.

Kiongozi lazima ukubali kwamba siyo kila mtu atakubaliana na wewe, hata kama utaamua kugawa fedha kwa kila mtu, wapo watakaosema kwa nini umegawa na usingepeleka sehemu nyingine.

Kiongozi lazima uwe tayari kufanya kazi na watu wote, hata wale wanaokupinga na kukukosoa wazi wazi, kwa sababu hawa ndiyo watu wazuri zaidi kwako wewe kama kiongozi. Unaweza kuwa na nia nzuri kabisa kwenye jambo unalofanya, lakini kukawa na mahali ambapo unakosea, watu hawa wanaokukosoa watakufanya uwe makini zaidi.

Kiongozi lazima ujue kwamba wanaokupinga na kukukosoa siyo kwamba wanakuchukia wewe kama mtu, bali wanapingana na kile ambacho unafanya au kusimamia. Hivyo usichukue hili kama chuki binafsi na kuanza kutumia nguvu yako ya uongozi kuwadhuru wale wanaokupinga na kukukosoa.

Na wakati mwingine, viongozi wenye mafanikio makubwa, wamekuwa wanawakosesha watu sababu ya kukosoa na kupinga. Iko hivi, ni tabia ya binadamu kupenda mashindano. 

Hivyo mtu anapokupinga na wewe ukampinga, unamchochea kupinga zaidi mpaka ashinde, lakini wewe kama kiongozi ukaamua kumpa ushindi, mashindano yanaishia pale pale, kwa sababu yanakuwa hayana raha tena.

Uongozi ni kazi nzito, lakini ndiyo kazi pekee itakayomwezesha kila mmoja wetu kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa kama utashindwa kuongoza kikundi cha watu kufanya kitu ambacho ni kikubwa, ambacho hakuna hata mmoja anakiona na kukiamini ila wewe mwenyewe.

Kubali kupingwa na kukosolewa na boresha ushirikiano wako na boresha ushirikiano wako na kila mtu, utaweza kufanya makubwa popote pale ulipo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.