Nchi ya Tanzania imepitia vipindi tofauti mpaka kufika hapa tulipo sasa. Tukianza na harakati za uhuru mpaka kuupata uhuru, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kufutwa kwa mfumo wa vyama vingi na hatimaye kuja kurejeshwa tena. Yote haya ni matukio ambayo yameleta mabadiliko makubwa kwenye nchi yetu.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, baba wa taifa la Tanzania ni mtu mwenye mchango mkubwa sana kwa hapa nchi yetu ilipofika. Alikuwa raisi wa kwanza wa Tanzania kuanzia uhuru na muungano mpaka mwaka 1985 ambapo aliamua kung’atuka kwenye uongozi.

Baada ya kung’atuka kwake, raisi aliyefuata alikuwa ni Ali Hassan Mwinyi, ambaye kwa wakati wake, yapo mambo yaliyofanyika, ambayo hayakumfurahisha Nyerere. Nyerere kwa uchungu aliokuwa nao kwa nchi hii, aliona kukaa kimya ni hatari kubwa, ndipo alipoandika kitabu hichi cha Uongozi Wetu Na Hatima Ya Tanzania.

uongozi wetu

Kitabu hichi ni kama maonyo, ushauri na wosia wa Nyerere kwa viongozi wa Tanzania na maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, nikushirikishe yale niliyojifunza, ambayo yanatuwezesha kuijua vizuri nchi yetu na kuweza kupiga hatua.

 1. Changamoto ya ukomo wa uongozi.

Wakati Mwalimu anaandika kitabu hichi mwaka 1994, ulikuwa umebaki mwaka mmoja kufika ukomo wa raisi  Mwinyi. Kulikuwa kumeanza kuwa na minong’ono kwamba raisi Mwinyi aendelee kuwa raisi. Hili lilimkera mwalimu na kuona iwapo halitasemwa waziwazi na kuandikwa kwenye katiba kwamba ukomo wa raisi ni vipindi viwili, basi litakuja kuleta shida mbeleni.

Tumekuwa tunaendelea kuona hili, tangu uongozi wa Mkapa, Kikwete na sasa Magufuli, kila uongozi, kumekuwa na minong’ono ya raisi kuongezewa muda.

Mwalimu anatukumbusha kwamba lazima pawepo na ukomo wa uongozi, kwa sababu ndivyo katiba yetu inavyotaka. Kwenda kinyume na hilo, ni kutengeneza matatizo baadaye.

 1. Tishio la kuvunjika kwa muungano wa Tanzania.

Katika kitabu hichi, Mwalimu amejadili matukio mawili makubwa ambayo yalikuwa yanatishia muungano wa Tanzania.

Tukio la kwanza ni Zanzibar kujiunga na umoja wa nchi za kiisilamu. Hili lilikuwa kinyume na katiba na kupelekea watu kuona Zanzibar ina uhuru mkubwa ndani ya muungano.

Tukio la pili lilikuwa vuguvugu lililoanzishwa na kundi la wabunge 55 maarufu kama G55 kutaka muundo wa muungano utengenezwe upya na kuwe na muungano wa shirikisho la serikali tatu. Kitu ambacho Mwalimu alikikemea sana na kusema kuifufua Tanganyika ni kuua Muungano.

 1. Vuguvugu la kubadili muungano lilikuwa ni ajenda ya vingozi.

Katika kitabu hichi, Mwalimu anatuonesha namna gani vuguvugu la kudai serikali ya Tanganyika lilikuwa ajenda ya viongozi na siyo ya wananchi. Anatuonesha kwamba hakukuwa na uhitaji mkubwa wa wananchi kuhusiana na muundo wa muungano. Badala yake ilikuwa ni ajenda ya baadhi ya viongozi ambao walikuwa wanataka madaraka zaidi.

 1. Utaratibu mpya wa kumpata makamu wa raisi.

Wakati wa utawala wa Mwalimu, na hata utawala wa Mwinyi, uongozi wa juu ulikuwa ni raisi wa Muungano, waziri mkuu ambaye pia alikuwa makamu wa kwanza wa raisi na raisi wa Zanzibar ambaye alikuwa makamu wa pili wa raisi wa Muungano.

Nyerere alishauri hili libadilishwe kwa sababu nchi ilikuwa imeingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Hivyo iwapo chama kimoja kitaongoza serikali ya muungano na chama kingine serikali ya Zanzibar, ingetokea changamoto ya uongozi.

Hapa ndipo ulipopendekezwa mfumo wa kuwa na mgombea mwenza ambaye anatoka upande wa pili wa muungano, tofauti na ule anaotoka mgombea uraisi.

 1. Wanafalsafa ni viongozi wazuri, ila hawapendi uongozi.

Mwalimu anatuandikia kwamba, changamoto kubwa tunazopata kwenye uongozi, ni kwa sababu tunaowachagua kuwa viongozi ni wanasiasa. Mwalimu akimnukuu Plato anasema kwamba wanafalsafa ni viongozi wazuri, kwa sababu kwanza hawapendi kuongoza, hivyo wakipewa uongozi, watafurahia pale unapofikia ukomo. Tofauti na wanasiasa ambao hawataki uongozi wao ufikie ukomo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; On Becoming A Leader (Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuwa Kiongozi Bora Kwa Zama Hizi).

 1. Suluhisho ni kuwabana viongozi na siyo kuvunja muungano.

Mwalimu anatushirikisha mkutano wake na kundi la wabunge ambao walitaka mfumo wa muungano kutengenezwa upya. Walimpa sababu nyingi za kutaka hivyo, na Mwalimu alikubaliana nazo, lakini aliwaambia zote ni matatizo ya uongozi, ambayo yangeweza kutatuliwa kwa wabunge kuwabana viongozi na siyo kukimbilia kubadili muundo wa muungano.

Mwalimu aliamini kwa changamoto zilizokuwepo kwenye muungano wa serikali mbili, kwenda kwenye serikali tatu kungetengeneza changamoto kubwa zaidi na muungano huu usingepona.

 1. Kuongoza ni kuonesha njia.

Jambo moja kubwa lililomkera Mwalimu kwa wakati ule ni uongozi kukosa nafasi ya kuonesha njia na badala yake ukawa unafuata njia. Yaani viongozi hawakuwa watengeneza ajenda ambazo zinaleta mijadala, badala yake mijadala ilikuwa inaanzishwa na wengine na uongozi kulazimika kujitetea au kujinasua.

Mwalimu aliona huu ni udhaifu mkubwa ambao unaipeleka nchi kwenye matatizo makubwa.

 1. Mara ya kwanza Mwalimu Kulizwa na mambo ya siasa.

Vuguvugu la kubadili muundo wa muungano lilijadiliwa ndani ya chama, na chama kikakubali kwamba lipingwe. Mwalimu aliombwa kuwapa semina viongozi wa chama na serikali kuhusu madhara ya kubadili mfumo wa muungano.

Lakini muda mfupi baada ya makubaliano hayo, katika vikao vya chama, Mwalimu alisikitishwa sana pale aliposikia kwamba swala la muundo wa muungano limerudi tena na wakati huo chama ilibidi kifanye maamuzi mengine.

Mwalimu alishindwa kujizuia na kujikuta akilia, kwa sababu hakuelewa iweje jambo ambalo limeshakubaliwa na vikao vya juu vya chama linarudishwa tena kwa maamuzi tofauti.

 1. Kwa nini serikali tatu pekee?

Baada ya swala la kubadili mfumo wa muungano kuonekana kuendelea zaidi ya ilivyotegemewa, Mwalimu alihoji kwa nini wanaotaka muungano ubadilishwe wanataja serikali tatu tu?

Alieleza ipo miundo mbalimbali ya muungano, serikali moja, mbili na hata serikali tatu. Je kwa nini wananchi wasipewe nafasi ya kujua aina hizo mbalimbali za muungano, faida na hasara zake kisha wachague ipi inafaa?

Hapa ndipo Mwalimu alishawishika zaidi kwamba ajenda ya muundo wa muungano ilikuwa ya watu wachache wenye maslahi yao binafsi.

 1. Dhana ya uwajibikaji.

Moja ya mambo yaliyomkera zaidi Mwalimu ni kukosekana kwa dhana ya uwajibikaji. Kwa mfano kwenye swala la muungano, waziri mkuu alimshauri raisi akatae mapendekezo ya kujadili muungano, na raisi akafanya hivyo. Lakini miezi miwili baadaye, waziri mkuu yule yule alimshauri tena raisi kukubali mapendekezo ya kujadili muungano.

Mwalimu anasema hapa kunakosekana uwajibikaji, ni labda waziri mkuu angepaswa kujiuzulu yeye mwenyewe, au raisi alipaswa kumfukuza waziri mkuu. Lakini hayo yote hayakufanyika, na iliashiria udhaifu mkubwa kwenye uongozi.

SOMA; Hii Ndiyo Changamoto Kubwa Ya Kuwa Kiongozi, Ambayo Lazima Uijue Na Ujiandae Nayo.

 1. Raisi kukokotwa.

Moja ya vitu ambavyo Mwalimu aliviona ni hatari kwenye uongozi wa nchi, ni hali ya raisi kukokotwa na viongozi aliowachagua yeye mwenyewe. Ilionekana kama raisi hana kauli kwenye swala la muungano, na hivyo alikuwa akifanya kila anachoshauriwa kufanya.

Hii ilitokana na viongozi wale kujua udhaifu wa raisi na kuutumia vizuri. Walijua makosa aliyoyafanya kwa kufumbia macho swala la Zanziba kujiunga na umoja wa nchi za kiislamu. Hivyo walitumia mwanya huo kulazimisha hoja ya muungano.

 1. Raisi anawajibika kwa maamuzi yoyote anayofanya, hata kama ameshauriwa.

Mwalimu anatukumbusha kwamba kwa uongozi wa nchi yetu, raisi ni kiongozi ambaye ana mamlaka ya juu kabisa ya utendaji. Raisi anaweza kushauriwa, lakini halazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote. Anapaswa kufanya maamuzi sahihi na maamuzi yoyote anayofanya yeye ndiyo anawajibika nayo.

Alieleza kwamba hata kama raisi ameshauriwa na mtu, na akafanyia kazi ushauri huo na ukawa ni makosa, anayelaumiwa ni raisi na siyo aliyemshauri. Hivyo raisi anapaswa kufikiri kila jambo kwa kina, hata kama ameshauriwa na mtu gani.

 1. Kumtikisa raisi ni kuitikisa nchi.

Mwalimu aliona kilichokuwa kinaendelea kwa wakati ule ni kama raisi alikuwa anataka kutikiswa na watu, na hilo lingekuwa hatari sana kwa nchi.

Ilionekana kama viongozi waliokuwa chini yake, hasa waziri mkuu na mawaziri wengine, walikataa kuwajibika kwa makosa yao. Na raisi aliogopa kuwafukuza kazi.

Mwalimu alisema kumbadili waziri hata waziri mkuu siyo jambo la ajabu, anaweza kujiuzulu au kufukuzwa na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa raisi wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.

 1. Raisi Mwinyi kama kiongozi dhaifu.

Mwalimu alisema kwamba, raisi mwingi alikuwa mtu mwema na mpole, lakini akasema wazi kwamba alikuwa kiongozi dhaifu. Alionya kwamba upole na udhaifu wake ulikuwa unatumiwa na watu ambao si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu.

Aliona mipango ya watu hawa kutengeneza uongozi utakaofuata baada yake, na hapo alitaka utengenezwe mchakato mzuri la sivyo kuna watu watajijengea njia ya uongozi kwa hila.

 1. Mchakato mpya wa kumpata mgombea uraisi ndani ya chama.

Wakati wa chama kimoja, kamati kuu ya chama cha mapinduzi ilipendekeza jina moja la nani atagomea uraisi na hilo kupitishwa na halmashauri kuu na mkutano mkuu.

Mwalimu alitilia shaka mchakato huo wakati wa mfumo wa vyama vingi. Hivyo alipendekeza mchakato wa kura za maoni katika kupata mgombea wa chama kwa ngazi ya uraisi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; LEADING QUIETLY (Jinsi Watu Wanavyofanya Makubwa Bila Ya Kuwa Na Majina Makubwa).

 1. Muungano wa Tanzania ni wa kipekee duniani.

Mwalimu aliandika kwamba muungano wa Tanzania ni wa kipekee kabisa duniani. Alieleza kwamba huu ulikuwa muungano wa nchi mbili huru, kwa ridhaa yao wenyewe tofauti na ilivyokuwa awali kwamba muungano ulilazimishwa na mipaka ya wakoloni.

Mwalimu aliwahoji wale waliokuwa wanahoji uhalali wa muungano, kwa nini hawahoji uhalali wa mipaka ya nchi mbalimbali iliyotengenezwa na wakoloni?

 1. Lawama ni kwa Chama Cha Mapinduzi.

Mwalimu aliamini kwamba, chama imara kinazalisha serikali imara, hivyo iwapo serikali itashindwa kusimama vizuri, lawama zote ni kwa chama cha mapinduzi. Alionesha namna ambavyo chama kimekosa uongozi mzuri wa kuweza kuisimamia serikali katika sera za chama.

Kwa mfano mchakato wa kubadili muungano, ulikuwa kinyume na sera za chama, kitendo cha jambo hilo kuruhusiwa, ilikuwa udhaifu kwa chama.

 1. Uhitaji wa chama cha upinzani imara.

Mwalimu aliamini kwamba, bila ya upinzani imara, chama cha mapinduzi kitaendelea kuwa kibovu. Alieleza chama kinahitaji upinzani ambao utawaamsha viongozi na kusimamia misingi ya chama.

Yeye mwenyewe pamoja na kuwa mwasisi wa chama, alisema chama siyo baba wala mama yake, iwapo kitakuja chama kingine chenye misingi mizuri na uongozi imara, angeondoka ccm na kujiunga nacho.

 1. Woga unajenga udikteta.

Mwalimu alionesha namna ambavyo watu wanashindwa kusimamia viongozi kwa kuwa na woga. Mwalimu alisema woga siyo heshima, bali woga unazaa udikteta.

Pale watu wanapoanza kumwogopa kiongozi badala ya kumheshimu, hapo wanazalisha dikteta ambaye atawatawala atakavyo na asihojiwe kwa namna yoyote ile.

 1. Uhuru una gharama zake.

Mwalimu aliandika kwamba, uhuru hauji wala haudumishwi ila kwa kuwa tayari kulipa gharama zake. Vitu vyote vyenye thamani kubwa, gharama yake ni kubwa. Lazima watu wawe tayari kuingia gharama katika kutengeneza na kulinda uhuru wao kama wananchi wanaowasimamia viongozi waliowachagua.

Kitabu hichi cha Mwalimu Nyerere, kinatupa taswira ya changamoto kubwa ya uongozi iliyokuwepo wakati anaandika kitabu hichi. Ni changamoto ambayo imezalisha matatizo mengi kwa nchi yetu ambayo bado inaendelea kuwepo katika ngazi mbalimbali za uongozi wa vyama na serikali.

Kupitia kitabu hichi cha Mwalimu, tunaona hatua muhimu za kuchukua kama viongozi, wananchi na hata wanachama wa vyama mbalimbali katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama na kuwa na maendeleo. Ni kitabu muhimu kwa kila Mtanzania kusoma ili kuelewa jitihada za kuitengeneza Tanzania bora zilipotokea.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

fb instagram