MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwa kila mmoja wetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Kama jana ulisema kesho, basi jua kesho yenyewe ndiyo leo au haitakuja kufika kamwe. Chukua hatua leo ili uweze kupata kile unachotaka.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari UNAONA NINI?
Unapoyatafakari maisha unayoishi sasa, unaona nini?
Unapoangalia kule unakokwenda, unaona nini?
Unapofanya chochote unachofanya, unaona nini?
Ni muhimu kujiuliza maswali haya, kwa sababu kile tunachoona, ambacho wengine hawaoni kinaathiri sana matokeo yetu na maisha yetu kwa ujumla.
Mara zote huwa tunaishia kupata kile tunachoona, tunayaweka mazingira ili kuendana na kile tunachoona.
Hivyo kama unachoona ni hasi, kibaya na mambo kuwa hovyo, hakika hayo ndiyo yatakayotokea kwenye maisha yako.
Muhimu kabisa ni kwamba, unachoona kinaanzia kwenye unachofikiria. Hivyo kama hupendi unachoona sasa, ni vyema ukabadili unachofikiri kwa sasa, kwa kuwa unachofikiri ndiyo kinaamua uone nini.
Uzuri ni kwamba, una uwezo wa kubadili fikra zako na unaweza kubadili mtazamo wako wakati wowote unapoamua kufanya hivyo.
Hebu fanya sasa, ili uweze kutengeneza picha bora ya maisha yako na kuweza kuiishi.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.