Tumekuwa tunajifunza kila mara umuhimu wa biashara kujitofautisha.

Kwamba ili biashara iweze kufanikiwa, lazima iwe tofauti na biashara nyingine, lazima mteja ajue kuna kitu anakipata kwenye biashara hiyo, ambacho hawezi kukipata sehemu nyingine yoyote.

Lakini hili pia ni muhimu mno kwa wamiliki wa biashara. Ni muhimu kila mmiliki wa biashara akawa na kitu cha tofauti ambacho anakipeleka kwenye ulimwengu wa biashara.

Kwa kuwa tabia za biashara huendana na tabia za mmiliki wa biashara ile, basi kile cha tofauti ambacho mtu anacho, kinaifanya biashara kuwa tofauti.

Na cha tofauti tunachozungumzia hapa ni tabia ambazo wewe kama mfanyabiashara unakuwa nazo. Zipi ambazo ni tofauti kabisa, ambazo wafanyabiashara wengine hawana?

Je unaweza kufanya kazi muda mrefu zaidi ya wengine? Unaweza kufungua biashara yako mapema kabla ya wengine na kuchelewa kufunga kuliko wengine wote? Hii ni tabia ambayo itakutofautisha sana na wengine, kwani wale wateja wanaowahi na kuchelewa, wanajua kwako watapata huduma.

Je unapenda kujaribu mambo mapya zaidi ya wengine? Una ubunifu tofauti na wa kipekee ambao unaweza kuweka kwenye biashara yako? Hii itakusaidia kwa sababu utaweza kufanya mambo kabla wengine hawajayajua na hivyo kuweza kufanikiwa.

Je unaweza kujifunza kuhusu biashara yako na biashara kwa ujumla zaidi ya wengine? Unaweza kusoma vitabu zaidi kuhusu biashara, watu, mafanikio, fedha na hata mikakati mbalimbali ya kibiashara zaidi ya wengine wanavyofanya. Hiyo inakusaidia kuweza kupata mbinu zinazokuwezesha kupiga hatua kubwa kwenye biashara yako.

SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Yako Inavyozidi Kukua, Unahitaji Kubadili Mikakati…

Chochote ambacho unaweza kukifanya kwa ubora zaidi ya wengine, angalia namna ya kukiweka kwenye biashara yako. Haitakuwa ngumu kwako kufanya, kwa sababu ni kitu unaweza, na pia itakusaidia sana kwa sababu unakwenda hatua kubwa zaidi ya wengine.

Kila siku jiulize ni kwa namna gani tabia zako binafsi zinaweza kuinufaisha zaidi biashara yako. Kisha boresha zaidi, weka tabia zako nzuri kwenye biashara yako, zile ambazo hakuna mfanyabiashara mwingine anaweza kuzitumia kwenye biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog