Kama kuna kitu kimoja ambacho kila mtu anapaswa kujifunza hapa duniani, basi ni jinsi ya kuuza. Hii ni muhimu sana kwa sababu, maisha yetu yote, kuna vitu tunauza, hata kama hatupo kwenye biashara.
Kwenye kazi, unauza muda na utaalamu au uzoefu wako. Kwenye uongozi unauza maneno na sera. Kwenye mahusiano unauza maono na mapenzi. Kwenye biashara unauza bidhaa na huduma.

Sasa wengi wanafikiri kuuza tunayosema hapa ni ile ya nauza kitu hichi, bei ni hii. Huko siyo kuuza, huko ni kuchuuza.
Kuuza ni pale unapoweza kumshawishi mtu, na kumwonesha uhitaji wake kwenye kile ulichonacho, na yeye akashawishika kuchukua hatua, bila ya shaka yoyote.
Kuuza tunakosema hapa ni ile hatua ya kutengeneza uhitaji wa kile ulichonacho, kwa wale ambao wanakihitaji kweli, na wanapokipata kikawa na msaada kwao.
Kuuza ni muhimu mno, kwa sababu kupitia kuuza ndiyo tunaweza kutoa thamani yetu kwa wengine, na wao wakatunufaisha pia.
Sasa kwa bahati mbaya sana, hatuwezi kujifunza kuuza kupitia wengine, kwa sababu wengi, hata waliopo kwenye biashara, hawajui jinsi ya kuuza. Wengi wanajua kuchuuza, kumwambia mteja bei na kuanza kupunguzana.
Unapojifunza kuuza, mteja hatajali sana kuhusu bei, kwa sababu ataona uhitaji wake mkubwa na namna ananufaika na kile unachotaka kumpa. Ukiweza kuuza vizuri, yule unayemuuzia anaona kama amechelewa sana kujua kile unachomwambia, na hivyo kutaka kukipata haraka, muda huo huo. Unaweza kuwa unakazana kumwambia bei yeye anakuambia nataka sasa, kwa maana bei inakuwa siyo muhimu tena kwake.
SOMA; Tabia Tano (5) unazohitaji ili kuwa muuzaji bora.
Unaweza kujifunza kuuza kwa kusoma vitabu vinavyohusu kuuza, kushiriki mafunzo ya kuuza na muhimu zaidi, kujifunza kwa kuanza kuuza. Chagua kitu chochote, iwe ni bidhaa au huduma, ijue kwa undani kabisa, inafanyaje kazi na inawasaidia watu wa aina gani. Chagua mtu ambaye bidhaa hiyo inaweza kumsaidia, kisha mweleze kuhusu bidhaa hiyo, ukikazia kwenye matatizo aliyonayo na namna bidhaa hiyo inayatatua.
Kwa kufanya hivi, utaanza kuona majibu mazuri ya namna watu wanashawishika na kile unachowaambia na kuweza kuchukua hatua.
Jifunze kuuza na siyo kuchuuza. Kuuza kunakupa ushawishi na kuweza kufanikiwa kwenye jambo lolote unalofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Asante sana Kocha nimejua tofauti ya kuuza na kuchuuza nilikuwa naijua tofauti Kabisa
LikeLike
Karibu sana Jilala
LikeLike