Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambao unatuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tunatafakari kuhusu MIPANGO SI MATUMIZI…
Japokuwa unahitaji kuwa na mipango mikubwa ya maisha yako, kuanzia kwenye siku yako, wiki yako, mwezi, mwaka na hata miaka, usisahau kwamba mipango si matumizi. Siyo lazima kila unachopanga kitokee kama ulivyopanga.
Kuna wakati utapata tofauti na ulichotegemea kupata,
Kuna wakati hutapata kabisa,
Kuna wakati utapoteza,
Na kuna wakati utachelewa kupata.
Yote hayo yanawezekana, hivyo unapoweka mipango, fikiria hayo na uone ni namna gani hayataathiri mipango yako mingine.
Chochote unachopanga, kipe nafasi ya kutokea au kutokutokea, hii siyo kuwa na fikra hasi, bali kujiandaa vyema kwa lolote linaloweza kutokea.
Kwa mfano kama yupo mtu anayemdai na akakuhakikishia kabisa ya kwamba atakulipa fedha yako kesho, usiende mahali na kuahidi kwamba una uhakika kesho utapata fedha hiyo. Jua inawezekana akakupa au asikupe, na hapo sasa ujiandae, iwapo atakupa utafanya nini na asipokupa utafanya nini.
Kuweza kufikia ngazi hii ya kifikra hasa kwenye mipango ndiyo kunatofautisha watu waliokomaa na wale ambao bado hawajakomaa.
Watu ambao hawajakomaa, wana tabia kama za watoto, wanataka kitu na wanakitaka sasa. Wakikosa watanuna, kukasirika, kulia, kulaumu wengine na hata kung’ang’ana na mambo ambayo hayawezekani.
Ila watu waliokomaa, wanapopanga kupata kitu, huweka nafasi ya kutokukipata na kuwa na njia mbadala iwapo hawatapata. Na siyo kwamba wanachukulia poa, ila wanakuwa na njia mbadala kuhakikisha hawakwami kwa lolote.
Ni mara chache sana kila unachopanga kitatokea kama ulivyopanga, hivyo mpango wowote unaoweka, jua kuna uwezekano usiende kama ulivyoweka, je unafanya nini katika hali hiyo?
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.