Unapoanzisha biashara, kitu kikubwa ni kuangalia matatizo au changamoto ambazo watu wanazo, kisha unakuja na suluhisho la matatizo na changamoto hizo.

Hilo ndilo ambalo kila mfanyabiashara anafanya. Na kwa kuwa huna cha kuwazuia watu kufanya unachofanya wewe, kutegemea hilo pekee hakukuwezeshi kuwa na wateja waaminifu kwa biashara yako.

Wateja waaminifu wa biashara wanatengenezwa, na ili kuwatengeneza, lazima kwanza uende zaidi ya mahitaji na matatizo yao.

IMG-20170321-WA0000

Lazima uwajali wao kama wao, pamoja na suluhisho unalowapatia, watu wanafurahi sana pale wanapoona wanajaliwa. Pale wanapoona wao ni wa muhimu kwa biashara husika, wanakuwa waaminifu.

Watu wanapenda matatizo na changamoto zao zitatuliwa, lakini wanataka zaidi kujaliwa, kuoneshwa kwamba wao ni wa muhimu mno. Unapoweza kutimiza hilo kwenye biashara yako, hasa kwa zama hizi za ushindani mkali, unakuwa umejipa faida ya ushindani ambayo haiwezi kuigwa.

SOMA; BIASHARA LEO; Ni Mapenzi Na Kujali, Siyo Bei…

Kujali hakuwezi kuigwa, kwa sababu kujali hakuna kanuni, kujali hakufundishwi kwenye mafunzo yoyote ya biashara na pia kujali hakuwezi kupimwa. Hichi ni kitu ambacho unafanya kwa sababu ni muhimu kwako kufanya. Unafanya kutoka ndani yako na siyo kwa sababu unataka kupata kitu fulani.

Ukitengeneza kujali kwa ajili ya kuwahadaa wateja kwa muda mfupi, wataliona hilo na utawapoteza kabisa. Jenga tabia ya kujali, iwe ni maisha yako na biashara yako. Yeyote anayehusika kwenye biashara yako abebe hilo, kwamba kumjali mteja ni kipaumbele cha kwanza kabisa cha biashara.

Faida ya ziada ya kujali ni wateja kuwaleta wateja wengine zaidi kwenye biashara yako. Mtu anayejaliwa, hatokaa kimya, atawaambia na wengine pia, ambao watakuja na kupata huduma ile nzuri waliyopata.

Jali sana wateja wa biashara yako, wafanye kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye biashara yako, hili litakulipa maradufu kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog