Kuendesha biashara kuna changamoto nyingi sana. Changamoto hizi zimewazuia wengi kuweza kukuza biashara zao na kufikia mafanikio makubwa.
Changamoto hizi za biashara tunaweza kuzigawa kwenye makundi makuu mawili. Changamoto za kibiashara na changamoto za watu.
Changamoto za kibiashara hizi ni zile za kawaida, mauzo, mzunguko wa fedha, mwenendo wa uchumi, kodi na kadhalika.

Lakini changamoto za watu hizi ndiyo kubwa zaidi na ndiyo zinaua biashara nyingi. Hizi ni changamoto ngumu zaidi kwa sababu watu wana changamoto zao na ni vigumu sana kutabiri watu au kuwapeleka vile unavyotaka.
Kadiri biashara inavyokua, ndivyo watu zaidi wanahusika kwenye biashara hiyo. Kuanzia wanaokusaidia kwenye biashara yaani wafanyakazi, unaoshirikiana nao kibiashara, na hata wateja wa biashara.
SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Yako Ina Pumzi?
Kadiri watu wengi wanapokuwa pamoja, ndivyo inavyoongeza nafasi ya msuguano, kutokuelewana, kugombana na hata kushindana. Yote haya ni hatari sana katika ukuaji wa biashara yoyote ile.
Kadiri watu wanaohusiana na biashara wanavyokuwa wengi, ndivyo wengi wanaokuja wanakuwa hawaielewi biashara vizuri. Kwa mfano unapoanza biashara mwenyewe, wewe ndiye unajua kila kitu kuhusu biashara yako na hivyo kuweza kuisimamia vizuri. Unapoajiri watu wachache ambao unawasimamia moja kwa moja, unaweza kuwaonesha vizuri kule biashara inapoenda. Lakini inapofika hatua kwamba uliowaajiri nao wanaajiri, au waajiriwa wapya wanakuwa chini ya watu wengine na siyo wewe moja kwa moja, ni vigumu kwao kuielewa biashara kama unavyotaka wewe.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa upande wa wateja. Mwanzoni unapokuwa na wateja wachache, wanakuwa ni wale ambao wanaielewa biashara yako kweli, wale wenye uhitaji na wapo tayari kufanya biashara na wewe. Lakini kadiri wateja wanavyokua wengi, wanakuja na wengine ambao hawaielewi biashara vizuri, wengine wanataka kukutapeli, wengine wanataka kujaribu kuona nini wanapata.
Hivyo mfanyabiashara, hakikisha unajipanga vizuri sana kwenye eneo hili la changamoto za watu kwenye biashara yako.
Na kwa kuanza, hasa kwa wale unaowaajiri kwenye biashara, ambao changamoto zao zina ukali zaidi kwenye biashara, unahitaji kuwa na mpango mzuri wa watu wote kwenye biashara kuufuata.
Lazima watu wote waheshimiane bila ya kujali cheo au daraja. Lazima watu washirikiane na tengeneza ufanyaji wa mambo katika timu. Tengeneza njia ya kutatua misuguano na kutokuelewana baina ya watu kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.
Na muhimu zaidi, tengeneza maono ya biashara ambayo kila mfanyakazi kwa nafasi yake atayaishi na kuyafanyia kazi kila siku anapokuwa kwenye biashara.
Yapo mambo ambayo hayaongelewi wazi wazi kama mahusiano baina ya wafanyakazi, ambayo yasipochukuliwa vizuri yanaweza kuharibu sana ufanisi wa wahusika katika biashara yako. Hili ni eneo ambalo unahitaji kulifanyia kazi vizuri ili kuweza kuzuia madhara yake kuharibu biashara yako.
Changamoto hazitakoma kuwepo, muhimu ni kuzifanyia kazi mapema ili zisilete madhara kwenye biashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog