Sehemu muhimu sana ya biashara ni mauzo, bila ya mauzo, biashara yoyote inakufa, hata kama ni nzuri kiasi gani.
Pamoja na maeneo yote ya biashara kuwa muhimu, eneo la mauzo linahitaji mtazamo wa kipekee ili kuhakikisha biashara inaendelea kwenda.
Katika kuuza, watu wengi hufanya makosa, ya kujiangalia wao wenyewe badala ya kuwaangalia wateja. Wengi huangalia wanatoa nini, na kusahau kuangalia wateja wanahitaji nini.

Leo nakwenda kukushirikisha maeneo mawili muhimu sana kwenye mauzo, ambayo yanamhusisha mteja wako.
Eneo la kwanza ni kabla ya mteja kununua.
Mteja haji kununua kwa sababu unauza, bali anakuja kununua kwa sababu ameshawishika kununua. Na kabla hajafanya maamuzi hayo ya kununua, lazima kwanza akuamini wewe kama mfanyabiashara.
Lazima mteja awe na hakika kwamba, fedha yake anayoitoa, ambayo huenda ameitafuta kwa jasho sana, inakwenda kumfanya apate kitu ambacho anakihitaji kweli, ambacho kitamsaidia kulingana na changamoto zake na hata uhitaji wake pia.
Hivyo jijenge kibiashara kwa namna ambayo utaaminika na wateja wako. Mara zote timiza kile unachoahidi, hata kama ni kidogo kiasi gani. Uza bidhaa na huduma zenye ubora wa hali ya juu na hivyo wateja kutokuwa na shaka juu ya kile unachouza.
Kwanza wateja wanakupenda, pili wanakuamini halafu ndiyo wananunua kwako.
SOMA; BIASHARA LEO; Ni Mapenzi Na Kujali, Siyo Bei…
Eneo la pili ni baada ya mteja kununua.
Kumbuka huendeshi biashara ya pata potea, kwamba mteja akishanunua ndiyo imetoka.
Pia kumbuka mteja ambaye ameshanunua kwako na akaridhishwa na kile ulichomuuzia, ni mteja mzuri sana, kwa sababu atarudi tena na pia kuwaalika wengine nao waje kwenye biashara yako.
Hivyo baada ya kumuuzia mteja, unahitaji kujenga naye mahusiano mazuri. Unahitaji kuendelea kumkaribisha kwenye biashara, kumkumbusha pale vitu vipya vinapopatikana na hata kumsaidia pale anapopata changamoto kwenye kutumia kile alichonunua kwako.
Katika kujenga mahusiano pia mwezeshe mteja wako kusambaza habari zako kwa ndugu, jamaa na marafiki zake ili uweze kupata wateja zaidi kwenye biashara yako.
Biashara ni urafiki, ambao unaanza na mteja kukuona au kusikia kuhusu wewe, akapenda biashara yako na namna unavyoiendesha, akakuamini, akanunua halafu akawa rafiki yako wa maisha. Hivi ndivyo biashara za zama hizi zinavyokwenda. Fanyia kazi mzunguko huo wa biashara ili kuwahudumia vizuri wateja wako na hata kupata wateja wengi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog