Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni siku mpya ya wiki mpya ambapo tumepata fursa nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, tufanyie kazi msingi huu ili tuweze kupata matokeo bora leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UHALISIA VS MATARAJIO…

Kila mtu huwa na matarajio fulani kabla hajafanya jambo lolote…

Kabla mtu hajaanza kazi huwa na matarajio makubwa kwenye kazi husika, kuanzia kipato, kazi anazofanya na namna anavyochukuliwa na wengine.

Lakini anapoanza kazi, anakutana na uhalisia, ambao unaweza usiendane na matarajio aliyokuwa nayo. Labda kipato siyo kama alichotarajia, kazi anazofanya ni za kawaida sana na watu hawampi uzito aliokuwa anategemea mwanzo.

Mtu kabla hajaanza biashara, huwa na matarajio makubwa. Kwamba sasa yeye ni bosi, hakuna wa kumpangia muda gani aamke, hakuna wa kumzuia wala kumpangia kipato na utajiri ni nje nje.

Lakini anapoingia kwenye biashara uhalisia unakuwa tofauti, anajikuta siyo bosi kama alivyofikiri, badala yake anakuwa mtumwa zaidi. Anagundua hawezi kuamua aamke saa ngapi, lazima aamke mapema sana kukamilisha majukumu yake. Na kwenye fedha sasa, mambo yanakuwa magumu, kipato hakitabiriki, siku chache kipato juu, siku nyingine kipato kidogo au hakuna kabisa.

Kadhalika kwenye mahusiano, watu wanaingia wakiwa na matarajio makubwa mno. Lakini wanachokutana nacho, kinawakatisha tamaa na kuona labda wanakosea au mambo siyo mazuri.

Ukweli ni kwamba, matarajio hayawezi kwenda na uhalisia, kwa sababu picha unayotengeneza wewe ni kwa namna unavyofikiria, lakini uhalisia unajiendesha siyo kwa fikra zako zilivyo, bali kwa mambo yalivyo.

Hivyo, kwa jambo lolote ambalo huwezi kulidhibiti, usiweke matarajio makubwa. Ingia ukijua kwamba unachokwenda kukuta ni tofauti na unachotegemea, lakini panga kujifunza na kukazana kuwa bora zaidi kwa hali yoyote utakayokutana nayo.

Mwisho kabisa, matarajio na uhalisia vinaathiri furaha zetu, pale matarajio yanapokuwa makubwa kuliko uhalisia, furaha inakuwa ndogo. Na pale matarajio yanapokuwa madogo kuliko uhalisia, furaha inakuwa kubwa. Hivyo kwa yale ambayo huwezi kudhibiti, usiwe na matarajio makubwa.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz