Tunaishi kwenye dunia ya wingi, kila mtu anapenda kuwa na vitu vingi. Kwa sababu dunia inachanganya wingi na mafanikio. Kwamba mwenye vingi ndiye aliyefanikiwa, asiyekuwa na vingi basi ameshindwa. Hii ni falsafa mbovu sana kwenye kila eneo la maisha.

Lakini inakuwa mbovu zaidi inapoingia kwenye biashara. Wapo watu wanapima mafanikio ya kibiashara kwa wingi wa biashara ambazo wanazo. Siyo kitu kibaya, ila pale mtu anapokuwa na biashara nyingi halafu zote zinakufa, siyo jambo zuri.

Wapo watu ambao wanaanza biashara moja, haijasimama vizuri wanaanzisha nyingine na nyingine tena. Baadaye wanajikuta kwenye changamoto kubwa na biashara zote kuelekea kufa.

IMG-20170314-WA0003

Ninachotaka kukukumbusha leo mfanyabiashara ni kwamba kabla hujakimbilia kufungua biashara nyingine, tengeneza kwanza mfumo mzuri wa biashara uliyonayo sasa. Ielewe vizuri biashara hiyo, elewa changamoto zake na kuwa na njia ya kuzitatua. Kisha tengeneza mfumo mzuri, ambao hata unapokuja kuanzisha biashara nyingine, hutarudia makosa na changamoto ulizofanya awali.

Ni bora kuwa na biashara moja au mbili ambazo unaziendesha vizuri na kwa faida, kuliko kuwa na biashara tano ambazo zote zina changamoto na nyingi zinajiendesha kwa hasara.

SOMA; BIASHARA LEO; Kosa Kubwa Wanalofanya Wanaoanza Biashara…

Ipo faida kubwa ya kuwa na biashara nyingi, lakini kama zote zinajiendesha kwa hasara na bado hujaweza kutengeneza mfumo mzuri wa kuziendesha, hilo linakuwa mzigo mkubwa kwako.

Unapokuwa kwenye biashara, kuna wakati utaona fursa nzuri sana na kuona usipochukua hatua zitakupita. Lakini napenda nikuambie kwamba kama biashara unayofanya sasa hujaweza kuisimamia vizuri, ni bora uache fursa hiyo mpya ipite kwanza. Wewe kazana kusimamisha biashara yako vizuri.

Fursa moja ikikupita leo, kuna fursa nyingi zaidi zitakuja kesho na siku zijazo. Hivyo hilo lisiwe wasiwasi kwako.

Usitake kufanya kila biashara wakati bado hujaweza kuisimamia vizuri hata biashara moja. Usiwe na haraka ya kuwa na biashara nyingi kwa wakati mmoja, hakuna mashindani ya mwenye biashara nyingi. Piga hatua sahihi kwa wakati sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog