Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Leo tutafakari KUWA KAMA WENGINE….

Kwenye maisha ya kawaida, kila mtu anapenda kuwa kama wengine. Ndiyo maana ukienda eneo fulani, utakuta watu wana maisha yanayofanana. Nenda hata maeneo ya kazi, utakuta aina ya watu walioko pale hawatofautiani sana kimaisha, hasa waliopo kwenye ngazi moja.

Kwenye maisha ya kawaida, kuwa kama wengine ni kujisikia vizuri, kuona na wewe maisha yako siyo mabaya sana, kama kile ambacho wengine wanacho na wewe unacho pia.

Lakini kwenye kazi na biashara, kuwa kama wengine ni KIFO. Ni shimo ambalo mtu anajichimbia kisha anaingia mwenyewe na kujifukia.

Kuwa kama wengine kwenye kazi ni kuchagua kubaki nyuma na kutokupiga hatua kabisa. Ni kuamua nafasi yoyote inayojitokeza ya kupiga hatua isikuhusu kabisa wewe.

Kuwa kama wengine kwenye biashara ni kuwaruhusu wateja wakupuuze, wasiwe na kitu kikubwa cha kufuata kwako kwa kuwa kila unachotoa wanaweza kukipata kwa wengine.

Usikubali kabisa kuwa kama wengine, hasa kwenye kazi na biashara. Nenda hatua ya ziada, weka ubora na ubunifu wa hali ya juu. Na hakikisha kila unachofanya, unaweka nembo yako, ambayo hakuna mwingine anayeweza kuiweka.

Na hata kwenye maisha ya kawaida, kuwa kama wengine ni chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo, hasa pale wengine wanapopiga hatua na wewe hupigi. Chagua maisha ambayo yana maana kwako na ishi hayo.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz