Unapokuwa na wateja ambao wanalalamikia mambo mengi kwenye biashara yako, ni vyema ukajihakikishia kwamba ni wateja sahihi kabla hujachukua hatua.

Kwa sababu wapo watu ambao wamepewa ushauri wa namna ya kuboresha biashara zao na watu ambao siyo wateja wa biashara hizi.

Yaani mtu anakuja na kukuambia ungefanya hivi ungepeta wateja kweli yaani, unafanya lakini kumbe yeye mwenyewe siyo mteja na hata ukifanya hanunui.

Taaluma

Ushauri wa biashara ni muhimu, lakini siyo kila ushauri unaifaa biashara yako. Ushauri mwingine unaweza kuwa mzuri kwa maelezo, lakini utekelezaji wake usiwe mzuri.

Hivyo pamoja na ushauri mzuri unaoweza kupata, hakikisha unaangalia eneo hili muhimu, tabia za wateja wako kwenye biashara yako.

Ukiwa mfuatiliaji makini wa biashara yako, kuna tabia za wateja wako utaanza kuziona, utawaona wakipendelea vitu fulani zaidi, au kama umeweka machaguo, kuna chaguo ambalo litapendelewa na wengi.

Kwa kuona tabia hizo, unaweza kuboresha zaidi biashara yako kuhakikisha unawatimizia wateja kile ambacho wanahitaji, na siyo unachofikiri wewe wanahitaji.

SOMA; BIASHARA LEO; Kabla Hujafanya Maamuzi Kutokana Na Maoni Ya Watu, Fikiria Hili…

Hakuna sehemu unayoweza kupata ukweli kuhusu biashara yako kama kuangalia tabia za wateja wako. Wakati mwingine hata ukiwauliza wateja wako, wanaweza kukupa majibu fulani, lakini unapowaangalia tabia zao, unagundua ni tofauti na yale waliyosema.

Makampuni na taasisi kubwa za kibiashara wanawekeza sana kusoma tabia za wateja, kuanzia maneno wanayotumia, upangaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na hata namna ya kuwaaga.

Waangalie wateja wako, wafuatilie wateja wako na simamia biashara yako kwa makini, kila unachotaka kujua kuhusu ukuaji wa biashara yako, tayari kipo hapo kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog